Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani tarehe 2 Januari 2019 limeanza mafungo kwa mwaka 2019 Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani tarehe 2 Januari 2019 limeanza mafungo kwa mwaka 2019  (AFP or licensors)

Maaskofu Katoliki Marekani waanza mafungo ya mwaka 2019

Mapambano dhidi ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia yanahitaji nguvu za maisha ya kiroho na rasilimali fedha ili haki iweze kutendeka na watoto kupata mazingira salama kwa malezi na makuzi yao. Maaskofu wanapaswa kuwajibika kikamilifu katika misingi ya haki na imani, ili “kufyekelea mbali ndago za kashfa za nyanyaso za kijinsia” ili kuwajengea watu matumaini na Kanisa kujitakatifuza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, kuanzia tarehe 2-8 Januari 2019 litakuwa “Mlimani” ili: kufunga, kusali na kufakari kama sehemu ya utekelezaji wa mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ili kutafakari kwa kina na mapana kashfa ya nyanyaso za kijinsia iliyoibuka mwaka, 2018 huko Marekani ni hivyo kuchafua maisha na utume wa Kanisa. Mafungo haya yanaongozwa na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Vatican News anasema,  kwa sasa Kanisa linajiandaa kwa ajili ya mkutano maalum dhidi ya nyanyaso za kijinsia, mwezi Februari, 2019. Mkutano huu utakaoongozwa na mambo makuu matatu: uwajibikaji, dhamana ya uwajibikaji; ukweli na uwazi. Ni mkutano ambao umeitishwa na Baba Mtakatifu Francisko na utashirikisha viongozi wakuu kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, ili kuimarisha mbinu mkakati wa kupambana na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo; kuganga na kuponya athari hizi pamoja na kuwasikiliza waathirika ili haki iweze kutendeka.

Lengo kuu ni kujenga mazingira salama kwa makuzi na malezi ya watoto wadogo sanjari na kuendelea kumwilisha sera na mbinu mkakati ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia kadiri ya mazingira ya Makanisa mahalia pamoja na kuhakikisha kwamba, tunu msingi za maisha ya Kiinjili zinatekelezwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa.

Kwa upande wake, Kardinali Daniel N. DiNardo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani katika hotuba yake elekezi kwenye Mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani alikazia umuhimu wa Maaskofu kuwajibika barabara katika kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia kwa kuzingatia misngi ya ukweli, uwazi, haki na wajibu ili kurejesha tena imani na matumaini kwa familia ya Mungu nchini Marekani, kwa kujikita katika mchakato wa kuganga na kuponya kashfa za nyanyaso za kijinsia, mchakato unaojikita katika toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho.

Mapambano dhidi ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia yanahitaji nguvu za maisha ya kiroho na rasilimali fedha ili haki iweze kutendeka na watoto kupata mazingira salama kwa malezi na makuzi yao. Maaskofu wanapaswa kuwajibika kikamilifu katika misingi ya haki na imani, ili “kufyekelea mbali ndago za kashfa za nyanyaso za kijinsia” na hivyo kuwajengea watu matumaini na Kanisa kuendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wakleri wanahamasishwa kujisadaka bila ya kujibakiza katika haki na upendo, ili kuendeleza Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, kwa kusimama kidete katika kanuni maadili na utu wema, kwa kukesha na kusali; kwa kufunga na kutubu, ili wasianguke tena katika kashfa na hatimaye kumezwa na malimwengu.

Wakati huo huo, Askofu mkuu Christophe Pierre, Balozi wa Vatican nchini Marekani katika hotuba yake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, aligusia changamoto kubwa zilizojitokeza katika kipindi cha mwaka 2018 katika maisha na utume wa Kanisa nchini Marekani; mambo yanayohitaji mabadiliko makubwa na uwajibikaji wa kina kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili kuwa watu wa wazi na wa kweli mbele ya Mwenyezi Mungu kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko, ili kujenga na kudumisha umoja na utakatifu wa Kanisa. Ikumbukwe kwamba, mageuzi ni sehemu ya vinasaba, maisha na utume wa Kanisa kama wanavyokaza kusema Mababa wa Kanisa “Ecclesia semper reformanda est”.

Malezi ya awali na endelevu kwa wakleri ni muhimu sana sanjari na kuhakikisha kwamba, familia yote ya Mungu inakuwa macho dhidi ya dalili za watu kukengeuka na kutopea katika nyanyaso za kijinsia. Lakini, ikumbukwe kwamba, huu ni wajibu wa kwanza wa Askofu mahalia. Matumizi mabaya ya madaraka kamwe hayataweza kuvumiliwa tena, kwani hiki pia kimekuwa ni chanzo cha kuficha maovu ambayo sasa yamegeuka kuwa ni kashfa kwa Kanisa. Kristo Yesu, ndiye njia, ukweli na uzima, awe ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wa Kanisa unajikita katika fadhila ya unyenyekevu.

Uongozi ndani ya Kanisa ni huduma inayowajibisha kujenga na kudumisha umoja wa urika wa Maaskofu kati yao pamoja na Khalifa wa Mtakatifu. Askofu anapaswa kuwa ni mtu wa sala, anayejitaabisha kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wake; katika maisha na utume wake, Askofu ni daraja linalowaunganisha watu wa Mungu katika Kanisa mahalia. Kumbe, ni wajibu wa Maaskofu kukuza na kudumisha sanaa na utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kujibu kilio na matamanio halali ya watu wa Mungu, tayari kujenga na na kudumisha: umoja, udugu, upendo na mshikamano.

Askofu mkuu Christophe Pierre anakaza kusema, changamoto za nyanyaso za kijinsia zinaweza kukabiliwa kikamilifu kwa viongozi wa Kanisa kujikita katika utekelezaji wa Mwongozo wa Malezi ya Kipadre “Ratio Fundamentalis” katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unaokazia umuhimu wa kuwafunda majandokasisi kiutu, ili waweze kukomaa, pili ni tasaufi ya maisha na wito wa kipadre unaowataka kujisadaka bila ya kujibakiza na hatimaye, watambue kwamba, wao ni watu wa huduma. Pili ni utekelezaji wa Mwongozo wa Malezi ya Kipadre nchini Marekani ili kweli majandokasisi waweze kufundwa kikamilifu kadiri maisha na utume wao ndani ya Kanisa.

Baraza Maaskofu Katoliki USA
02 January 2019, 09:06