Bwana Paolo Ruffini, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano akihutubia katika Mkutano wa siku za kimataifa za Mtakatifu Francisko wa Sale huko Lourdes Bwana Paolo Ruffini, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano akihutubia katika Mkutano wa siku za kimataifa za Mtakatifu Francisko wa Sale huko Lourdes  

Dhamana na utume wa waandishi wa habari duniani!

Huu ni mchakato wa kujenga na kudumisha jumuiya inayofumbatwa katika mawasiliano, kwa kukazia ukweli na mafungamano ya kijamii; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano na kusikilizana; kwa kuunganisha na kamwe mawasiliano yasiwe ni kwa ajili ya kuwatenganisha na kuwasambaratisha watu. Mitandao ya kijamii iwe ni madaraja ya kuwakutanisha watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya 23 ya Siku za Kimataifa za Mtakatifu Francisko wa Sale huko Lourdes nchini Ufaransa ni fursa kwa Baraza la Kipapa la Mawasiliano kukuza na kudumisha tasnia ya upashanaji habari ndani ya Kanisa kwa kutambua kwamba, hii ni sehemu muhimu sana ya utume wake. Jambo la kupea msukumo wa pekee ni kwa wanahabari wakatoliki ni kudumisha umoja, mshikamano na upendo.

Baraza la Kipapa la Mawasiliano linapania pamoja na mambo mengine, kuendeleza mikutano kama hii, ili kushirikishana weledi, uzoefu na mang’amuzi katika tasnia ya mawasiliano ya jamii. Mwaka 2018 Siku ya Kimataifa za Mtakatifu Francisko wa Sale zilihudhuriwa na waandishi wa habari 250 kutoka katika nchi 26 duniani. Mwaka 2019, idadi hii imeongezeka maradufu kwa uwepo na ushiriki wa  waandishi wa Habari 8 kutoka katika vyombo vya mawasiliano vinavyoendeshwa na kumilikiwa na Vatican. Umoja na mshikamano ni kati ya changamoto zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ili kuhakikisha kwamba, mitandao ya kijamii inasaidia kujenga umoja na mshikamano, utu na heshima ya binadamu.

Hii ni sehemu ya hotuba elekezi iliyotolewa na Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, Jumatano, tarehe 30 Januari 2019 huko Lourdes, Ufaransa wakati wa ufunguzi rasmi wa maadhimisho ya 23 ya Siku za Kimataifa za Mtakatifu Francisko wa Sale. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka 2019 itakayoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 2 Juni 2019 inawahamasisha wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kuuvua uongo, kusema ukweli kwa maana wao ni viungo, kila mmoja kiungo cha mwenzake.

Huu ni mchakato wa kujenga na kudumisha jumuiya inayofumbatwa katika mawasiliano, kwa kukazia ukweli na mafungamano ya kijamii; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadilia na kusikilizana; kwa kuunganisha na kamwe mawasiliano yasiwe ni kwa ajili ya kuwatenganisha na kuwasambaratisha watu. Mitandao ya kijamii anakaza kusema Baba Mtakatifu inapaswa kuwa ni madaraja ya kuwakutanisha watu hata katika imani. Mawasiliano yawe ni nyenzo ya kudumisha upendo na mshikamano; na ukweli unaorutubishwa kwa njia ya majadiliano. Waandishi wa habari wawe ni watu wanaochakarika kutafuta ukweli katika hali ya unyenyekevu, ili kuueneza kwa watu wengi zaidi.

Ukweli usaidie kujenga umoja na mafungamano ya kijamii, kwa kutangaza na kuenzi wema na upendo badala ya chuki na uhasama, changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo. Hii ndiyo dhamana ya wanatasnia ya mawasiliano ya jamii katika ulimwengu mamboleo wanaotakiwa kutangaza na kushuhudia: Ukweli, uzuri na wema; mambo msingi katika mchakato wa mawasiliano; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Bikira Maria hakuwa maarufu sana kwenye mitandao ya kijamii, lakini ni mwanamke wa shoka aliyeleta mageuzi makubwa katika historia ya maisha ya binadamu.

Mawasiliano Lourdes
30 January 2019, 16:36