Cerca

Vatican News
Utandwazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia vinawajengea watu tabia ya uchoyo na ubinafsi! Utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia vinawajengea watu tabia ya uchoyo na ubinafsi!  (AFP or licensors)

Usawa uzingatie: Utu, heshima na haki msingi za binadamu

Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hawana budi kuhakikisha kwamba, usawa, haki na amani ya kudumu vinapatikana kwa kuheshimu Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaendelea kuwajengea watu tabia ya uchoyo, ubinafsi na upweke hasi! hatari kwa mafungamano ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha na Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Ndoa na Familia ya Yohane Paulo II, ndiye aliyesoma ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa kuhusu Usawa wa Dunia, uliofunguliwa hapo tarehe 28 na kuhitimishwa tarehe 31 Januari 2019 huko mjini Havana, nchini Cuba. Mkutano huu umehudhuriwa na wajumbe 650 kutoka katika mataifa 65.

Askofu mkuu Paglia amezungumzia pia changamoto zinazotishia usawa na mafungamano ya Jumuiya ya binadamu, kiasi kwamba, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hawana budi kuhakikisha kwamba, usawa, haki na amani ya kudumu vinapatikana kwa kuheshimu Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia unaendelea kuwajengea watu tabia ya uchoyo, ubinafsi na upweke hasi, kiasi kwamba, kila mtu anataka kujiona na kubaki binafsi.

Maisha ya kijumuiya na kijamii hayana tena thamani kama ilivyokuwa kwa siku za nyuma. Maendeleo ya sayansi yanawaunganisha watu kwa njia ya mitandao ya kijamii, lakini yanashindwa kuwakutanisha na matokeo, kila mtu anaendelea kubaki na kuelea kwenye “ufalme wake”. Ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii, ubinafsi unapaswa kufyekelewa mbali na mabadala yake, umoja, upendo na mshikamano kupewa kipaumbele cha kwanza.

Askofu mkuu Paglia anasema, kuna haja ya kuwa na kanuni maadili ya kibayolojia kwa ajili ya wote kama njia ya kulinda, kutunza na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ni katika muktadha huu, watu wanaweza kushirikamana kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Mambo msingi ya kuzingatia hapa: kwanza kabisa mwanadamu anapozaliwa na pale anapoitupa mkono dunia. Haya ni mambo msingi yanayo mwandama mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani na waathirika wakuu hapa ni vijana wa kizazi kipya. Kumbe, kuna haja kwa dunia kujikita katika usawa unaozingatia uhai, utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kujenga na kudumisha familia ya binadamu!

Askofu mkuu Paglia
31 January 2019, 18:02