Cerca

Vatican News
Dhamana na utume wa Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Duniani! Ushuhuda wa mwanga wa ukweli! Dhamana na utume wa Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Duniani! Ushuhuda wa mwanga wa ukweli! 

Dhamana na Utume wa Vyuo Vikuu vya Kanisa Katoliki Duniani!

Wanafunzi wajifunze kupata ujuzi, maarifa na stadi za maisha kwa kujikita katika upendo na ukarimu, kwani ufanisi wao mwisho wa siku, utapimwa kwa kuzingatia nyenzo hizi. Wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, waweze kupata ufuo wa ukweli wote ambao ni Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Edgar Pèna Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican, Alhamaisi, tarehe 31 Januari 2019 amezindua rasmi mwaka wa masomo kwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Roma na kuwataka wanajumuia wa Chuo kikuu hiki kuwa ni wajenzi wa ufalme wa Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao. Watambue kwamba, Chuo kikuu ni mahali ambapo vijana wanapata mwanga wa kuweza kufukuzia mbali giza la ujinga, ili hatimaye, siku moja wanafunzi hawa wawe pia ni mashuhuda wa nuru ya ulimwengu ambayo ni Kristo Yesu!

Wanafunzi wajifunze kupata ujuzi, maarifa na stadi za maisha kwa kujikita katika upendo na ukarimu, kwani ufanisi wao mwisho wa siku, utapimwa kwa kuzingatia nyenzo hizi. Wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, waweze kupata ufunuo wa ukweli wote ambao ni Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Roho Mtakatifu awasaidie wanafunzi kukuza na kudumisha majadiliano kati ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake pamoja na tafiti za kisayansi, tayari kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa linalohimizwa kwenda ulimwenguni kote kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu Ubora wa elimu unaotolewa na Kanisa, unadhihilishwa wazi na wingi wa wazazi wanaopenda kupeleka vijana wao katika shule na taasisi za Kanisa, hata inapowalazimu wazazi kujibana sana kiuchumi ili kufanikisha nia yao njema.

Ieleweke wazi kwamba, Chuo Kikuu cha Kikatoliki ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa. Ni zawadi inayopaswa kupokelewa kwa heshima kubwa na moyo wa shukrani, tayari kuimwilisha katika imani inayowajibisha daima. Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, kilichoanzishwa na Padre Agostino Gemelli pamoja na wasaidizi wake wa karibu, kimekuwa ni msaada mkubwa katika kutoa mafunzo ya kisayansi pamoja na kuendelea kuwa waaminifu kwa mafundisho ya Kanisa, kiasi kwamba, Chuo kikuu hiki, kimekuwa ni kimbilio la vijana na matumaini ya wazazi na walezi kwa watoto wao, kwani wana uhakika kwamba, vijana wao watapata majiundo kamili ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, kwa kufuata mafundisho na mfano wa Yesu Kristo, Bwana na Mwalimu, Kanisa limeendelea daima kutafuta maana ya maisha na ukweli ili kumwilisha utimilifu wake katika maisha ya vijana. Ni katika undani wa maisha ya Kanisa, vyuo vingi vya kikatoliki vimeanzishwa na vinaendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya jamii na Kanisa katika ujumla wake. Ukatoliki wa Chuo kikuu unapaswa kuangaliwa kwa mwanga wa Fumbo la maisha na utume wa Kristo Yesu unaojikita katika huruma na upendo kwa watu wote. Watambue kwamba, Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima. Ni mwanga unaoangaza na unapaswa kuonekana na wengine. Askofu mkuu Edgar Pèna Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican anawataka wanafunzi chuoni hapo kumwomba Roho Mtakatifu ili awasaidie kutekeleza vyema dhamana, wajibu na utume wao ndan na nje ya Kanisa.

Chuo Kikuu cha Kikatoliki 2019
31 January 2019, 17:16