Tafuta

Papa Francisko kuanzia tarehe 3-5 Februari 2019 anatarajiwa kufanya hija ya kitume kwenye Falme za Kiarabu. Papa Francisko kuanzia tarehe 3-5 Februari 2019 anatarajiwa kufanya hija ya kitume kwenye Falme za Kiarabu. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Falme za Kiarabu: Niwe chombo cha amani

Kuanzia tarehe 3 hadi 5 Februari 2019, Baba Mtakatifu Francisko atatembelea huko Abu Dhabi, kwenye Falme za Kiarabu ili kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini utakaoongozwa na kauli mbiu "Udugu wa kibinadamu"

Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Kwa kupokea mwaliko wa Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, Mfalme mrithi wa Abu Dhabi, Baba Mtakatifu Francisko atatembelea Abu Dhabi  ambao ni mji mkuu wa Nchi za Falme za Kiarabu, kuanzia tarehe 3 hadi  5 Februari 2019, ili kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Mazungumzo kati ya Dini Mbalimbali. Ni Mkutano utakaoongozwa na kauli mbiu Udugu wa ubinadamu. Ni taarifa iliyotolea tarehe 6 Desemba 2018, kwa waandishi wa habari na Msemaji Mkuu  wa Vatican, Bwana Greg Burke. Ziara hii pia inatokana na kukukubali mwaliko wa Kanisa Katoliki katika Nchi za Falme za Kiarabu.

Kauli mbiu ya hija ya kitume:Nifanye chombo cha amani

Baba Mtakatifu Francisko amechagua jina la Mtakatifu Francis wa Assis, mtakatifu ambaye alikuwa mwanga na mfano katika kujikita kwenye matendo ya dhati ya maneno ya Yesu: Heri wapatanishi, maana wataitwa wana wa Mungu” (Matayo 5,9). Amani ya Mungu inaponya ubinadamu wa kila aina ya kizingiti na kusindikiza Habari njema iliyotangazwa na Yesu Kristo, ya Mungu anayetambua kujipatanisha na dunia.

Kauli mbiu nifanye chombo cha amani, imechukuliwa kutoka katika mwanzo wa Sala ya Amani ya Mtakatifu Francis wa Azizi na ambayo inafafanua nia ya maombi ambayo yatawakilishwa katika ziara ya Baba Mtakatifu, katika Nchi za Falme za Kiarabu na ili iweze kuenea kwa namna ya pekee, amani ya Mungu katika mioyo ya watu wote na hasa wenye mapenzi mema.

Nembo ya ziara ya Papa

Nembo iliyochaguliwa ni njiwa akiwa amebeba tawi la mzeituni alama ya amani. Rangi ya njiwa nyeupe, na rangi ya njano vinawakilisha rangi ya bendera ya Vatican. Rangi ya bendera ya Nchi za Kiarabu zimewekwa katika mabawa ya njiwa ili kuwakilisha ishara halisi ambayo Baba Mtakatifu Francisko anataka kutembelea nchi za Falme za Kiarabu kama mjumbe wa amani.

06 December 2018, 13:08