Vatican News
Tamko la haki msingi za binadamu ni nguzo ya haki zote! Tamko la haki msingi za binadamu ni nguzo ya haki zote!  (AFP or licensors)

Tamko la Haki Msingi za Binadamu: Nguzo ya haki zote!

Tamko la Kimataifa la Kaki Msingi za binadamu ni matokeo ya kukutana kati ya tamaduni za kidini na mila kati ya watu, pande zote zikiwa zinasukumwa na nia ya pamoja ya kumuweka mwanadamu kuwa ndiye kiini cha taasisi, sheria, matukio ya kijamii, tamaduni, dini na sayansi.

Na Padre Celestine Nyanda, - Vatican.

Katika kumbukumbu ya miaka 70 ya Tamko la Jumuiya ya Kimataifa juu ya haki msingi za binadamu, Professa Vincenzo Buonomo, Mkuu wa chuo kikuu cha Kipapa cha Lateran, anaandika kuhusu mamlaka ya Tamko hilo kama nyenzo inayobaki kati ya bawaba za sheria za kimataifa. Tamko hilo bado ni kiini cha maisha ya kila taifa na kwa Jumuiya ya kimataifa. Hata hivyo Professa Vincenzo Buonomo analeta changamoto ya kufikirisha iwapo Tamko hilo bado linajibu kikamilifu muono na mahitaji ya ya mahusiano kimataifa.

Tamko la Kimataifa la Haki Msingi za binadamu ni matokeo ya kukutana kati ya tamaduni za kidini na mila kati ya watu, pande zote zikiwa zinasukumwa na nia ya pamoja ya kumuweka mwanadamu kuwa ndiye kiini cha taasisi, sheria, matukio ya kijamii, tamaduni, dini na sayansi (Rej., Benedikto XVI, Hotuba kwa Umoja wa Mataifa, 18 Aprili 2008). Kwa hakika Tamko la kimataifa la haki msingi za binadamu ni jiwe la msingi lililowekwa katika historia ndefu na ngumu kwa Familia ya binadamu. Hivyo kama anavyosema Mt. Yohane Paulo II kwamba, maendeleo ya mwanadamu yanapaswa kupimwa kwa kuzingatia sayansi, teknolojia, lakini zaidi sana kwa kuzingatia maendeleo ya mtu kiroho na kimaadili (Rej., Yohane Paulo II, Hotuba kwa Umoja wa Mataifa, 2 Oktoba 1979).

Haki msingi za binadamu zinachota  uhalali wake kutoka katika kanuni asilia inayojumuisha wanadamu wote. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Tamko la kimataifa la haki msingi za binadamu lina lengo la kuangusha kuta za utengano na zinazoigawanya Familia ya binadamu, na kisha lisaidie maendeleo fungamani ya kila binadamu. Iwapo mwanadamu hatatazamwa katika upamoja wake na kwa kuzingatia hadhi yake, ndipo huwa chanzo cha ukosefu wa haki, kutokuwepo usawa wa kijamii na kufumuka kwa rushwa na nyanyaso za kila aina (Rej., Francisko, Hotuba kwa Wanadiplomasia mjini Vatican, 8 Januari 2018).

Professa Vincenzo Buonomo anasema kwamba, Tamko la kimataifa la haki msingi za binadamu halikuwekwa kama ishara tu au tangazo fulani, bali ni nyenzo ya kutetea uhuru wa binadamu dhidi ya uonevu, umoja wa Familia ya binadamu dhidi ya utengano wa kinadharia, kisiasa, ama ubaguzi wa rangi, jinsia, lugha na kidini. Tamko hili tangu awali limelenga kumlinda na kumtetea mwanadamu dhidi ya tabia ya kuabudu taifa na kumpotezea raia. Tamko limelenga pia kushinda hatari za uhalifu kutokana na makosa ya uhaini na matokeo mabaya ya vita, mauaji ya kimbari ili kulinda na kutetea thamani ya uhai, uhuru na hadhi ya binadamu. Swali la kujiuliza ni je!, nini maana ya haki na nini maana ya usawa! Sababu leo hii, kila kukicha kunashuhudiwa utengano mkubwa kati ya haki za binadamu na thamani ya haki hizo. Mfano haki ya kuishi, inaachwa kwa kila mmoja au taifa kujifanyia namna wanayodhani inafaa kulinda haki hiyo na wakati huo huo inatetewa haki ya uhuru wa kuukatisha uhai huo, kiasi kwamba thamani ya uhai haizingatiwi tena.

Kanisa linao mtazamo wa haki stahiki inayofaa pote ili kuepuka hatari ya mifumo mamboleo ya utumwa na unyanyasaji inayopaliliwa na matajiri zaidi na wenye nguvu kwa kuwaonea maskini na wanyonge. Tamaduni za kitaifa zisichukue nafasi ya kutotilia maanani haki msingi za binadamu zilizotiwa mkwaju katika Tamko la Kimataifa. Haki za binadamu hazina mipaka kimataifa, hazigawanyiki, zinategemeana na zinamahusiano makubwa kati yake. Wajibu wa Jumuiya ya kimataifa ni kuhakikisha kwamba haki zinalindwa na kutetewa katika kila kona ya ulimwengu, huku zikipewa thamani yake stahiki. Wakati huo huo kila taifa lihakikishe haki hizi zinazingatiwa katika nyanja zote kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni.

Ulinzi na utetezi wa haki msingi za binadamu bado unakumbana na changamoto nyingi mpya kila kukicha, hivyo ni lazima kutafuta pia mbinu zinazoendana na wakati ili kukabiliana nazo, lakini bila kupoteza thamani yake na kwa kuzingatia kanuni asilia, kutogawanyika, kutegemeana na mahusiano kati yake. Iwapo kanuni hizi hazitatiliwa maanani, hatari ni kujikuta watu wanajiongezea haki na mifumo mipya kila siku vinavyopelekea mpasuko kati ya mtu na mpasuko katika jamii. Mtazamo wa Kanisa ni wa msingi kusimamiwa kwamba, haki msingi za binadamu zinatokana na hadhi na utu wa binadamu  mwenyewe ikiwa ni pamoja na thamani asilia ya haki hizo. Hivyo mwanadamu lazima awekwe kuwa ndiye kiini cha haki hizo katika nafsi ya kila mmoja na kisha katika upamoja kama jumuiya.

Mtazamo huu ndio unaokuza juhudi za pamoja za kulinda na kutetea haki za kila mmoja na kwa jamii kwa ujumla kuhusu afya, elimu, lishe, ajira, usalama, mapumziko na maisha ya familia.Haki nyingi za binadamu ziko mashakani leo hii kufuatia baadhi ya matajiri na wenye nguvu kuwatazama wengine kana kwamba ni vitu na sio watu tena, hivyo kuwatumia watu hawa kwa ajili ya kujinufaisha bila kujali kabisa utu na heshima yao kibinadamu. Kanisa limekuwa mstari wa mbele siku zote kulinda na kutetea haki za binadamu mmoja mmoja na pia katika jamii wanamoishi, kwani binadamu kaumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, na ni lazima kila shughuli izingatie na kuheshimu utu wa binadamu na haki zake katika uthamani wake.

Professa Vincenzo Buonomo anasema kwamba yawezekana mtazamo huu ukaonekana uko nje ya mitindo ya leo ya kujinufaisha na kupotezea wengine bila kujali wala kuangalia sura ya mtu, hata hivyo ni lazima kuendelea kuusimamia mtazamo wa Kanisa, kwani suala sio kuishi kwa kufuata mitindo ya kisasa ama kizamani, bali suala ni utu, heshima na thamani ya binadamu na haki zake.

Tamko: Haki za Binadamu

 

 

15 December 2018, 15:34