Tafuta

Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2019 kuadhimishwa mjini Calcutta, India. Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2019 kuadhimishwa mjini Calcutta, India. 

Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani 2019: Calcutta, India!

Kardinali Patrick D’Rozario, C.S.C, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dhaka, atakuwa mwakilishi maalum wa Papa katika maadhimisho ya Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2019, yatakayoadhimishwa kuanzia tarehe 9-11 Februari 2019 huko mjini Calcutta, nchini India. mchakato wa tiba na huduma kwa wagonjwa uzingatie: utu, heshima na mahitaji msingi ya mgonjwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Patrick D’Rozario, C.S.C, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dhaka, nchini Bangaladesh kuwa mwakilishi wake maalum katika maadhimisho ya Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2019, yatakayoadhimishwa kimataifa kuanzia tarehe 9-11 Februari 2019 huko mjini Calcutta, nchini India. Baba Mtakatifu Francisko anataka mchakato wa tiba na huduma kwa wagonjwa kuhakikisha kwamba, inazingatia kwanza kabisa utu, heshima na mahitaji msingi ya mgonjwa.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Siku ya 26 ya Wagonjwa Duniani, kwa mwaka 2018 anapembua kuhusu: wito wa Mama Kanisa wa huduma kwa wagonjwa na maskini; kumbu kumbu endelevu ya historia ya huduma kwa wagonjwa sanjari na nguvu ya uponyaji inayoonesha uhusiano uliopo kati ya utume wa uponyaji na mwamko wa imani kwa wagonjwa wanaokutana na Kristo Yesu, wakiomba huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huduma ya uponyaji inayotekelezwa na Kristo Yesu kwa wagonjwa mbali mbali inahitaji jibu la imani thabiti kutoka kwa wahusika.

Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuhakikisha kwamba, linaendelea kupyaisha huduma kwa wagonjwa sanjari na kujikita katika uaminifu kwa amri iliyotolewa na Kristo Yesu mintarafu mng’ao wa mwanga wa utukufu wa Fumbo la Msalaba. Kwani hili ni fumbo la matumaini, huruma na upendo usiokuwa na kikomo. Ikumbukwe kwamba, fadhila ya upendo ni msingi wa maisha ya kila mfuasi wa Kristo na Jumuiya za Kikristo zinapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upendo wa Kristo kwa waja wake.

Katika hija ya maisha yao hapa duniani, wafuasi wa Kristo watambue kwamba, wanasindikizwa, wanalindwa na kutunzwa na Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Huyu, ndiye Mama ambaye upanga ulipenya moyoni mwake, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. Ni Mama ambaye aliendelea kuandamana na Kanisa katika sala kama inavyojionesha kwenye Siku kuu ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume. Mtume Yohane, aliwasaidia wagonjwa wa mwili na roho kukutana na Kristo katika hija ya maisha yao na hivyo wakaonja huruma, upendo, msamaha wa dhambi zao na hatimaye, wakafutwa machozi machoni pao. Hii ndiyo changamoto ambayo Wakristo wanapaswa kuivalia njuga kwa kumwilisha Injili ya upendo inayowataka kuhudumiana kwa dhati! Kwa njia hii, wakristo wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji na ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mama Kanisa katika maisha na wito wake, daima amekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, historia ambayo kwa hakika inapaswa kuwa endelevu. Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yameendelea kutoa huduma kwa wagonjwa hasa vijijini ambako bado huduma za afya zinasuasua. Mashirika haya yamekuwa yakitoa huduma bora, daima mwanadamu na mahitaji yake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza. Hospitali na taasisi za afya zimeendelea kufanya tafiti mbali mbali ili kuboresha tiba na huduma kwa wagonjwa, lakini maadili ya kikristo yamepewa msukumo wa pekee.   Kanisa limeendelea kusimama kidete katika kuchangia maboresho ya afya ya mama na mtoto kwa kupunguza vifo vya watoto wadogo; kwa kukinga na kutibu magonjwa mbali mbali. Kwa maneno mafupi, Kanisa daima limekuwa mstari wa mbele katika uwanja wa mapambano dhidi ya magonjwa kwa kuwasaidia wale waliojeruhiwa katika maisha!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kumbu kumbu ya historia ya huduma kwa wagonjwa ni chemchemi ya furaha, sadaka na ukarimu wa waanzilishi mbali mbali wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanayoendelea kutekeleza dhamana na utume wao kwa ubunifu na uaminifu mkubwa, kwa kufanya tafiti na kutoa kinga na tiba ya magonjwa mbali mbali. Kutokana na changamoto mamboleo, gharama za uendeshaji na vifaa tiba, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, hospitali zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, hazigeuzwi kuwa na mwelekeo wa kibiashara zaidi, kwani Kanisa linataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya mgonjwa katika mchakato mzima wa huduma na tiba kwa wahusika. Hata Wakristo wanaofanya kazi katika hospitali za serikali na binafsi wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Injili.

Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwapatia pia mitume na waandamizi wao nguvu ya uponyaji na kwamba, Kanisa linaendeleza huduma hii kwa huruma na mapendo na kwamba, inapaswa kupyaishwa na kumwilishwa kutoka katika familia, parokia hadi kufikia taasisi za huduma ya afya. Wagonjwa wa muda mrefu, walemavu na wazee wanapaswa kuangaliwa zaidi kwa jicho la upendo na kwamba, kuna haja pia ya kuwa na sera makini za huduma kwa wagonjwa. Wadau wa huduma ya afya watambue kwamba, wanashiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa wagonjwa, changamoto kwao ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo kama ushuhuda unaotajirisha huduma kwa wagonjwa.

Siku ya Wagonjwa 2019

 

15 December 2018, 14:48