Cerca

Vatican News
Kardinali Parolin: Kanisa bado linaendelea kusikiliza kilio na matumaini ya wafanyakazi duniani. Kardinali Parolin: Kanisa bado linaendelea kusikiliza kilio na matumaini ya wafanyakazi duniani!  (ANSA)

Kanisa linaendelea kusikiliza kilio cha wafanyakazi duniani!

Kanisa bado linaendelea kusikiliza kilio, mateso na matumaini kutoka katika ulimwengu wa wafanyakazi! Kanisa linataka kuona sera na mikakati ya uchumi inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, haki na mahitaji msingi ya binadamu. Kamwe wafanyakazi wasigeuzwe kuwa ni vyombo vya kuzalisha mali na faida kubwa inayosigana na utu, heshima na haki zake msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipotembelea na kuadhimisha Mkesha wa Sherehe ya Noeli, Jimbo kuu la Taranto, Kusini mwa Italia, Jumapili, tarehe 23 Desemba, 2018, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ameadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa ajili ya tukio hili! Katika mahubiri, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Majilio, amekazia umuhimu wa waamini kujiandaa kikamilifu kwa kukesha katika sala; kwa kufurahi na kushangilia ujio wa Mwana wa Mungu pamoja na kuendelea kujikita katika utekelezaji wa matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani tendaji!

Kardinali Parolin anasema, hii inatokana na ukweli kwamba, imani ya Kikristo inafumbatwa katika mchakato wa kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria kumtembelea Elizabeth, ili kumsaidia binadamu yake, aliyekuwa ni mzee lakini zaidi, mjamzito aliyepata upendeleo mbele ya Mungu. Hiki ni kielelezo kwamba, hakuna jambo lisilowezekana mbele ya Mungu. Elizabeth, Mama wa Yohane Mbatizaji, Mtangulizi wa Kristo Yesu, Mwanga utokao juu, unaokuja kuwaangazia wakaao katika giza na uvuli wa mauti.

Hii ni fursa ya kushirikishana zawadi itokayo juu na mwendelezo wa utume wa Mama Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji na ushuhuda wa huduma unaotekelezwa na Mama Kanisa katika wa huduma, umoja na udugu miongoni mwa Wakristo, wanaofanyika wamoja katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa kama alivyokaza kusema, Mtakatifu Paulo VI, miaka 50 iliyopita. Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima, ujumbe makini kwa watu wote duniani kwamba, leo kwa ajili yenu, amezaliwa Kristo Mkombozi wa ulimwengu!

Kardinali Parolin anasema, kwa njia ya ushirikiano na mshikamano wake unaofumbatwa kwenye Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu amekuwa tabibu anayeganga na kuponya udhaifu wa binadamu; huyu ndiye yule anayesamehe na kuondoa dhambi za walimwengu; na tumaini kwa wale waliokata tamaa. Kristo Yesu ni ndugu na jirani; mwamba na chemchemi ya haki, upendo na kilele cha amani ya kweli. Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria kumtembelea Elizabeth, sauti ya Papa inapaswa kuwafikia wafanyakazi wote, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mama Kanisa kwa njia ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, anayetangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayopaswa kumwilishwa katika matendo!

Miaka 50 imekwishagota, tangu Mtakatifu Paulo VI alipotembelea na kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mkesha wa Sherehe ya Noeli ya mwaka 1968. Kanisa bado linaendelea kusikiliza kilio, mateso na matumaini kutoka katika ulimwengu wa wafanyakazi! Kanisa linataka kuona sera na mikakati ya uchumi inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, haki na mahitaji msingi ya binadamu. Kamwe wafanyakazi wasigeuzwe kuwa ni vyombo vya kuzalisha mali na faida kubwa inayosigana na utu, heshima na haki zake msingi. Kanisa linataka kuona Jumuiya ya Kimataifa inajikita katika ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwani madhara ya uchafuzi wa mazingira ni makubwa kwa watu wengi.

Hiki ndicho chanzo kikuu cha umaskini, magonjwa na ujinga, changamoto kwa watu wote ni kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira. Sera na mikakati ya kazi, izingatie utu wa binadamu; mazingira bora ya kazi, ili kuenzi afya ya wafanyakazi. Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu iendelee kuwaombea maskini, watu wasiokuwa na fursa za ajira, walemavu kazini na wale wanaoendelea kuteseka kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira.

Parolin: Taranto 50 Yrs
23 December 2018, 15:17