Tafuta

Vatican News
Kardinali Parolin: Ujumbe wa Noeli kwa Familia ya Mungu nchini Iraq kwa Mwaka 2018 Kardinali Parolin: Ujumbe wa Noeli kwa Familia ya Mungu nchini Iraq kwa Mwaka 2018  (AFP or licensors)

Ujumbe wa Noeli kwa Familia ya Mungu Iraq kwa Mwaka 2018

Mwenyezi Mungu anayo mawazo ya amani na wala si ya mabaya ili kuwapatia matumaini. Ujio wa Neno wa Mungu ni chemchemi ya furaha na amani ya kweli inayokata matarajio halali ya binadamu. Ni Mwenyezi Mungu peke yake anayeweza kutoa amani na furaha ya kweli inayoimarishwa katika misingi ya usawa na haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika ziara yake ya kikazi nchini Iraq, kama kielelezo cha mshikamano wa umoja na udugu wa watoto wa Mungu, hasa katika eneo hili ambalo limegeuka kuwa ni uwanja wa vita, tarehe 24 Desemba 2018 amekutana na kuzungumza na Bwana Adil Abdul Mahd, Waziri mkuu wa Iraq pamoja na viongozi wakuu wa Serikali ya Iraq. Amewasilisha ujumbe wa Noeli kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Iraq. Hapa ni mwanzo wa historia ya ukombozi inayokita mizizi yake kwa Abrahamu, Baba wa imani.

Wakristo katika kipindi cha Noeli, wanaadhimisha Sherehe ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, kwa maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu anayo mawazo ya amani na wala si ya mabaya ili kuwapatia matumaini. Ujio wa Neno wa Mungu ni chemchemi ya furaha na amani ya kweli inayokata matarajio halali ya binadamu. Ni Mwenyezi Mungu peke yake anayeweza kutoa amani na furaha ya kweli inayoimarishwa katika misingi ya usawa na haki.

Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, nguvu aliyo nayo Mtoto Yesu inafumbatwa katika upendo unaobubujikia katika maisha mapya; upendo unaosamehe dhambi na kuwapatanisha watu; kwa kubadili ubaya na kuanza kujikita katika wema. Nguvu ya Mtoto Yesu ni ushuhuda wa huduma inayosimika na kujenga Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika haki na amani. Noeli ni Sherehe ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoitwa na kuhamasishwa kutembea katika mwanga unaofukuzia mbali giza la hofu na mashaka; chuki na uhasama; hali ya kutowajibika barabara, ili kwa njia ya maneno na matendo yao; waweze kupandikiza mbegu ya amani, ukweli, uhuru na upendo wa dhati.

Kardinali Parolin anasema,  familia ya Mungu nchini Iraq inahamasishwa kukita mizizi yake katika fadhila ya unyenyekevu kwa kuheshimiana, kuthaminiana na kushirikiana kama ndugu, ili kuimarisha tofauti msingi zinazojitokeza kati yao kama amana na utajiri mkubwa na wala si chanzo cha kinzani na mipasuko, daima wakitafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kuna mambo mengi yanayowaunganisha kama ndugu nchini Iraq, ikilinganishwa na yale yanayowatenganisha.

Kardinali Parolin anahitimisha ujumbe wake kwa familia ya Mungu nchini Iraq kwa kusema kwamba, furaha na amani ya Kipindi hiki cha Noeli ni changamoto na mwaliko wa kushirikishana na wengine, ili kuwajibika katika mchakato wa ujenzi wa umoja, udugu, amani na utulivu. Mwenyezi Mungu asili ya amani, aliyefanyika Mwanadamu, ndiye mwandani mwa safari ya maisha ya mwanadamu, kwani anawakirimia furaha na matumaini, kwa ajili ya leo na kesho iliyo bora zaidi kwa familia ya Mungu nchini Iraq.

Ujumbe wa Noeli: Iraq

 

26 December 2018, 14:10