Hija ya Kitume ya Kardinali Pietro Parolin nchini Iraq. Hija ya Kitume ya Kardinali Pietro Parolin nchini Iraq. 

Kardinali Parolin: Iweni mashuhuda wa msamaha na upatanisho!

Uwanda wa Ninawi una historia ndefu katika maisha ya Wakristo, kielelezo cha imani na mateso mbali mbali. Hata leo hii watu wanaoishi katika eneo hili wamejaribiwa; wakasalitiwa; nyumba zao za ibada zikaharibiwa na kunajisiwa! Yote haya yalijitokeza kunako mwaka 2014. Huo ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, yamekuwa ni alama ya imani, umoja na matumaini kwa familia ya Mungu nchini Iraq kama kielelezo cha muungano wao na Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, akawa ni chemchemi ya amani na wokovu kwa ulimwengu. Uwanda wa Ninawi una historia ndefu katika maisha ya Wakristo, kielelezo cha imani na mateso mbali mbali. Hata leo hii watu wanaoishi katika eneo hili wamejaribiwa sana; wakasalitiwa hata ndugu zao wenyewe; nyumba za ibada zikaharibiwa na kunajisiwa!

Yote haya yalijitokeza kunako mwaka 2014. Huo ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kutoka huko Mashariki ya Kati, lakini kutokana na imani thabiti kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, watu wameanza kurejea tena katika makazi yao ya awali, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini. Hiki kimekuwa ni kipindi cha ushuhuda wa imani kutoka kwa mashuhuda wa imani, waliothubutu kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, kwani hakuna jambo lolote lile linaloweza kuwatenga waamini na upendo wa Kristo!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Wakatoliki wa Siria, Ibada ambayo imehudhuriwa na Patriaki Ignatius Joseph Younan wa III pamoja na viongozi wakuu wa Kanisa, Serikali na waamini katika ujumla wao. Kardinali Parolin amewaalika waaamini kutafakari huruma ya Mungu iliyomwilishwa katika tumbo la Bikira Maria, huruma na upendo wa Mungu unaodai majibu makini, kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Kristo Yesu kwa nyakati zote, daima wakiwa mstari wa mbele kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika vita, chuki na uhasama.

Kristo Yesu ni chemchemi ya upendo na msamaha unaobubujika kutoka katika imani kama chachu ya ujenzi wa ulimwengu mpya. Kwa njia ya msamaha wa dhambi, Mwenyezi Mungu amejifanya jirani na binadamu! Upendo, wema na ukarimu unavunjilia mbali nguvu za giza, chuki na uhasama, kiasi cha watu kubaki huru. Wale wanaopata msamaha kutoka kwa Mungu, wawe wa kwanza kusamehe na kusahau, ili kutoa nafasi ya upendo kuibuka na kuchanua kama “mwerezi wa Lebanon”. Yote haya yanawezekana kwa mwamini kukita maisha yake katika sala kama alivyofanya Stefano shemasi na shahidi, kwani msamaha unatakasa na upendo huvunjilia mbali minyororo ya chuki na uhasama.

Kardinali Parolin anasema, msamaha ni msingi wa upatanisho. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa msamaha na upatanisho; haki na upendo, kwa kutambua kwamba, msamaha ni chemchemi ya wema na baraka kwa wote; dhamana inayopaswa kupata chimbuko lake katika maisha ya waamini, jamii na taifa katika ujumla wake ili kujenga na kudumisha umoja, udugu na mshikamano wa kweli. Yote haya yanawezekana, ikiwa kama waamini wanayo imani thabiti inayomwilishwa katika upendo. Kanisa linawashukuru na kuwapongeza Wakristo wa Iraq kwa uaminifu wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na kwamba, daima Kanisa linasonga mbele kwa sala na huduma ya upendo.

Kanisa linawashukuru wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wahitaji zaidi wakati wa vita na mahangaiko ya maisha. Sasa wananchi wanapoanza kurejea katika makazi yao ya awali, inakuwa ni alama ya furaha na matumaini, lakini changamoto mbele yao ni kujenga umoja na mafungamano ya kijamii ili kuvuka kishawishi cha chuki, uhasa pamoja na usaliti uliojitokeza huko nyuma. Uwepo wa Wakristo huko Mashariki ya Kati ni muhimu sana kwani hiki ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Kardinali Parolin amewatia shime wananchi wa Iraq kusonga mbele kwa imani na matumaini kwa kutambua kwamba, ubaya wa moyo na mateso hayana sauti ya mwisho katika maisha yao! Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, iwasaidie kukuza na kudumisha imani, matumaini na upendo.

Parolin: Qaraqosh

 

 

28 December 2018, 14:04