Kardinali Pietro Parolin akiwa mjini Erbil, nchini Iraq Kardinali Pietro Parolin akiwa mjini Erbil, nchini Iraq 

Kardinali Pietro Parolin: Ziara ya mshikamano na udugu Iraq!

Kardinali Parolin na ujumbe wake, wametembelea taasisi mbali mbali zinazoendeshwa na kumilikiwa na Kanisa huko Iraq. Amekagua Kituo cha Familia Takatifu; Kituo cha Mtakatifu Paul, Kituo cha Radio ya Jimbo, Mar Behman pamoja na kutembelea Monasteri ya Sarah. Akiwa Mosoul, Kardinali Parolin ametembelea Makanisa na kuzungumza na familia ya Mungu maeneo hayo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ziara ya Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican nchini Iraq kuanzia tarehe 24-28 Desemba 2018 imekuwa ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa udugu wa binadamu hasa huko Mashariki ya Kati ambako kwa miaka hivi karibuni, kumegeuka kuwa uwanja wa mapambano, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Tarehe 28 Desemba 2018, Kardinali Parolin ametembelea katika Uwanda wa Ninawi, huko Qaraqosh-Karamless-Bartalla na Mosoul na hatimaye, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Wakatoliki wa Siria huko Qaraqosh.

Kardinali Parolin na ujumbe wake, wametembelea taasisi mbali mbali zinazoendeshwa na kumilikiwa na Kanisa huko Iraq. Amekagua Kituo cha Familia Takatifu; Kituo cha Mtakatifu Paul, Kituo cha Radio ya Jimbo, Mar Behman pamoja na kutembelea Monasteri ya Sarah. Akiwa Mosoul, Kardinali Parolin ametembelea Makanisa na huko amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa na waaamini walei katika ujumla wao.

Tarehe 27 Desemba, Kardinali Parolin alitembelea Eneo la Kurdistan ya Iraq. Huko amekagua miradi mbali mbali ya maendeleo inayoendeshwa na Jimbo kuu la Erbil. Amekagua Kanisa la Watakatifu Petro na Paulo; Kituo cha Vijana pamoja na Kituo cha Papa Francisko, maalum kwa ajili ya wazee na familia changa. Amekagua Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Erdibil na kujionea mwenyewe ujenzi wa Hospitali ya Kanisa Katoliki huko Erdibil ambao kwa sasa uko katika hatua za mwisho.

Kardinali Parolin pamoja na ujumbe wake, wamemtembelea pia Bwana Masoud Brazan, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia cha Kurdistan na ambaye pia alikuwa ni Rais wa eneo hili. Amekutana na kuzungumza na Baraza la Usalama la Kurdistan, Masrous na Barzan na hapo wamepata chukula cha mchana. Majira ya jioni, Kardinali Parolin amefanya mazungumzo na Bwana Nechirvan Barzan, Waziri mkuu anayemaliza muda wake.

Jioni ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Watoto Mashahidi; ibada ambayo ilikuwa imesheheni waamini, waliotoa mwaliko kwa Baba Mtakatifu pale itakapowezekana kutembelea Iraq, ili kujionea mwenyewe jinsi imani inavyomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kawaida! Amehitimisha siku kwa kukutana na kusalimiana kwa kitambo kifupi na wafanyakazi na wawakilishi wa nchi mbali mbali wanaoishi huko Erbil.

Parolin: Ziara Iraq

 

 

28 December 2018, 13:47