Tafuta

Vatican News
Kardinali Pietro Parolin: imani, udumifu na upendo vifyekelee mbali ndago za chuki na uhasama nchini Iraq. Kardinali Pietro Parolin: imani, udumifu na upendo vifyekelee mbali ndago za chuki na uhasama nchini Iraq. 

Kardinali Parolin: Kiteni maisha yenu katika upendo na msamaha!

Kardinali Parolin anasema uwepo wa waamini katika mkesha wa Noeli ni kielelezo cha: imani, udumifu na upendo unaovunjilia mbali “ndago” za chuki, uhasama na ubaya wa moyo, tayari kuchota nguvu ya Mungu ili kuishi kama watoto wa Mungu; kwa kuendelea kujifunza kusamehe, kuganga na kuponya na kujipatanisha katika udugu unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican wakati wa hija yake ya kitume nchini Iraq, tarehe 24 Desemba 2018 ameshiriki katika maadhimisho ya mkesha wa Noeli kwenye Kanisa kuu la Babilonia ya Wakaldayo na baadaye pia ameshiriki katika Ibada ya Mkesha kwenye Kanisa kuu la Wasiria Wakatoliki huko Baghdad. Kardinali Parolin, akiwa kwenye Kanisa kuu la Babilonia ya Wakaldayo ametafakari kuhusu mateso, machungu na ushuhuda wa waamini waliopoteza maisha yao kunako mwaka 2010 kutokana na shambulio la kigaidi, kiasi hata cha kulinajisi Kanisa hili. Lakini, upendo wa Mungu unavuka mipaka ya chuki na kinyongo cha binadamu. Kuzaliwa kwa Mtoto Yesu ni kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake.

Kardinali Parolin anasema, uwepo huu ni chachu ya mabadiliko na upyaisho katika maisha, ili kufanana zaidi na sura na mfano wa Mungu, tayari kutangaza na kushuhudia uwepo wake wa karibu katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Kwa kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu ametekeleza ahadi na uaminifu wake katika historia nzima ya wokovu, ili kwamba, wale wote watakaomwamini waweze kufanyika kuwa ni wana wa Mungu.

Kardinali Parolin anakaza kusema, uwepo wa waamini katika mkesha wa Noeli ni kielelezo cha: imani, udumifu na upendo unaovunjilia mbali “ndago” za chuki, uhasama na ubaya wa moyo, tayari kuchota nguvu ya Mungu ili kuishi kama watoto wa Mungu; kwa kuendelea kujifunza kusamehe, kuganga na kuponya na kujipatanisha katika udugu ambao Mwenyezi Mungu anapenda kuuenzi kwa njia ya faraja na wema wake usiokuwa na kifani hata katika shida na mahangaiko ya mwanadamu, kiasi hata cha kuweza kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na woga wowote!

Bikira Maria ni chemchemi ya faraja inayowakirimia waamini amani na utulivu wa ndani. Ikumbukwe kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowashirikisha na kuwawajibisha binadamu, mwaliko na changamoto kwa waamini wote kuwa ni mashuhuda na vyombo vya uwepo wa Kristo, kwa kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa nchi yao, jamii na ulimwengu katika ujumla wake. Kwa hakika hii ni dhamana na wajibu mkubwa!

Kardinali Parolin katika Ibada ya Mkesha kwenye Kanisa kuu la Wasiria Wakatoliki huko Baghdad amekazia kuhusu utajiri wa Maandiko Matakatifu unaoshuhudia wema na upendo wa Mungu kwa binadamu. Kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, ni ufunuo wa wema na upendo wa Mungu kwa binadamu; ni amani ya Mungu inayotumwa ulimwenguni kama zawadi hai; kielelezo cha imani na matumaini ya watu wa Mungu, ili hatimaye, waweze kutembea katika mwanga angavu unaokita mionzi yake katika moyo wa mwanadamu ili kumkirimia mwanadamu amani na furaha ya kweli ili kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika usawa, haki na amani. Lakini, amani inayotolewa na Kristo Yesu ni tofauti kabisa na ile ambayo walimwengu wanapenda kutoa.

Amani ya walimwengu inakita mizizi yake katika nguvu ya silaha ili kupata ushindi; pamoja na nguvu ya kiuchumi ili kupata faida kubwa. Amani inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu inafumbatwa katika: upendo kwa Mungu na jirani; ni amani inayovunjilia mbali kuta za utengano na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Hii ni amani inayotakasa: vita, chuki na uhasama, ili kupandikiza mbegu ya upatanisho katika akili na nyoyo za watu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, nguvu ya Kristo Yesu inafumbatwa katika: Msamaha, upatanisho, huduma, haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Fumbo la Umwilisho linaloadhimishwa katika Kipindi cha Noeli ni mwaliko wa kufanya toba na wongofu wa ndani, kwa kujikita katika upendo, majadiliano, haki, amani, uhuru wa kweli, umoja na udugu. Hiki ni kipindi kinachofumbatwa katika imani, matumaini na mapendo, tayari kuanza upya kwa ari na moyo mkuu licha ya changamoto na magumu ya maisha yanayoendelea kumwandama mwanadamu!

Parolin: Mkesha Noeli
26 December 2018, 14:56