Cerca

Vatican News
Kardinali Parolin: Miaka 130 ya Uinjilishaji ni fursa ya kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa upendo, haki na amani! Kardinali Parolin: Miaka 130 ya Uinjilishaji ni fursa ya kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa upendo, haki na amani! 

Miaka 130 ya Uinjilishaji Mali: Haki, amani, ustawi na maendeleo

Mazungumzo kati ya Kardinali Parolin na Rais Ibrahim Boubacar Keïta yalijikita zaidi kuhusu maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Mali; mchango wake katika kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Dhamana na utume wa Kanisa katika malezi na majiundo ya dhamiri nyofu ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya Jubilei ya Miaka 130 ya Uinjilishaji nchini Mali alikazia kwa namna ya pekee misingi ya haki na amani. Anasema karne ya kumi na tisa ilipambwa na juhudi za pekee katika mchakato wa uinjilishaji Barani Afrika, ulioziwezesha jumuiya za Kikristo kukua kwa haraka, ingawa tayari kuna Jumuiya ya Bamako ambayo tayari inaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji, kazi na utume uliofanywa kwa ari na moyo mkuu kutoka kwa Wamisionari wa Roho Mtakatifu kuanzia mwaka 1888.

Baba Mtakatifu katika maadhimisho haya aliwakilishwa kwa namna ya pekee na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na huko alibahatika kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa, viongozi wa Serikali na familia ya Mungu katika ujumla wake. Mazungumzo kati ya Kardinali Parolin na Rais Ibrahim Boubacar Keïta yalijikita zaidi kuhusu maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Mali; mchango wake katika kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Mali. Dhamana na utume wa Kanisa katika malezi na majiundo ya dhamiri nyofu ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Rais Ibrahim Boubacar Keïta kwa upande wake, amegusia uhusiano mwema uliopo kati ya Serikali na dini mbali mbali nchini Mali; changamoto kubwa ya misimamo mikali ya kidini na kiimani; vitendo vya kigaidi vinavyodhalilisha utu, heshima, ustawi na mafungamano ya kijamii miongoni mwa watu wa Mali; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Mali pamoja na ukosefu wa usalama na amani katika maeneo yaliyoko kati kati ya nchi na Kaskazini mwa Mali.

Kardinali Parolin katika mazungumzo haya, kwa niaba ya Kanisa amekazia kuhusu dhana ya maendeleo endelevu na fungamani ya watu wa Mali, kama jina jipya la amani na utulivu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kumbe, Kanisa na Serikali vinapaswa kushirikiana kwa ukaribu zaidi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza: kwa utu, heshima, ustawi na maendeleo ya binadamu. Rais Rais Keïta amekazia ushirikiano na umoja wa Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Baraza la Maaskofu Katoliki Mali, limeipongeza na kuishukuru Serikali kwa ushirikiano wake wa dhati katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 130 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya kwanza nchini Mali.

Kardinali Jean Zerbo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bamako nchini Mali, katika hotuba yake kwa Kardinali Parolin, alisema, Kanisa nchini Mali, limempokea kwa mikono miwili kama mjumbe wa amani, kwa kuwakumbuka na kuwaombea wamisionari wote waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini Mali. Kanisa linamshukuru Mungu kwa kumbu kumbu ya miaka 130 ya Uinjilishaji, uwepo wa amani na utulivu pamoja na baadhi ya watawa waliokuwa wametekwa nyara kuanzia mwezi Februari 2017 kuachiwa huru. Kardinali Parolin amewakumbusha kwamba, maadhimisho haya ni kumbu kumbu endelevu ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; ni muda wa toba na wongofu wa ndani; shukrani, imani na matumaini kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Mali.

Kardinali Parolin alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Mali lililomwelezea kwa ufupi kuhusu: historia, maisha, utume, changamoto na matumaini ya watu wa Mungu nchini Mali. Maaskofu wanasikitika kusema, kumekuwepo na tatizo la viongozi wa Kanisa kutekwa nyara na watu wasiojulikana; baadhi ya Makanisa yamekuwa yakinajisiwa na kwamba, kwa sasa changamoto kubwa ni ulinzi na usalama wa watu na mali zao nchini Mali.

Kardinali Parolin, katika mazungumzo yake na majandokasisi wanaoendelea na malezi pamoja na majiundo yao ya Kikasisi katika Seminari kuu ya Saint-Augustin, iliyoko Jimbo kuu la Bamako, amekazia umuhimu wa majiundo ya awali na endelevu, daima wakijitahidi kuiga mfano bora kutoka kwa Kristo Mchungaji mwema. Kardinali ameshiriki kikamilifu katika hija na mkesha wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 130 ya Uinjilishaji nchini Mali.

Kardinali Parolin katika mahubiri kwenye kilele cha maadhimisho ya Jubilei hii, amekazia umuhimu wa umoja, ushirikiano na mafungamano ya kijamii katika medani mbali mbali za maisha kama njia ya ujenzi wa utamaduni wa upendo, ambao kimsingi ni chemchemi ya: haki, amani na maridhiano kati ya watu. Amewataka waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa umoja na mshikamano wa dhati kati yao, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, tofauti zao, zisiwe ni chanzo cha kinzani, vurugu na mipasuko isiyokuwa na tija wala mashiko!

Kardinali Parolin: Mali
22 December 2018, 08:08