Vaticano: Kardinali Parolin: Damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo mpya! Vaticano: Kardinali Parolin: Damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo mpya! 

Damu ya mashuhuda wa imani ni amana na utajiri wa Kanisa!

Wananchi hawa wamegeuza chuki na uhasama kwa kupandikiza ujirani mwema na mshikamano wa kidugu, dhana ambayo imeungwa mkono kwa hali na mali na Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa hakika hili ni jambo la kumshukuru Mungu. Tangu mwanzo, madhulumu dhidi ya Wakristo yamekuwa yakihusianishwa na mateso na kifo cha Kristo Yesu pamoja na mitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila Mwaka ifikapo tarehe 28 Desemba, anaadhimisha Siku kuu ya Watoto Mashahidi waliomshuhudia Kristo Yesu si kwa maneno bali kwa kuyamimina maisha yao kutokana na ukatili wa Mfalme Herode. Watoto hawa wanalikumbusha Kanisa kwamba, kifo dini ni zawadi kubwa kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa lake. Hawa ni watoto waliouwawa kikatili kwa upanga wa Mfalme Herode aliposikia kwamba, kuna Mfalme amezaliwa mjini Bethlehemu.

Maadhimisho haya kwa mwaka huu wa 2018 yamekuwa na uzito wa pekee huko Iraq kwa kuadhimishwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ambaye tangu tarehe 24-28 Desemba 2018 anafanya ziara ya kikazi nchini Iraq. Alhamisi, tarehe 27 Desemba 2018 majira ya jioni, Kardinali Parolin ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu huko Ankawa, kwa ajili ya kuwakumbuka Watoto Mashahidi waliouwawa kikatili na Mfalme Herode.

Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin, amekazia umuhimu wa utamaduni wa ukarimu na mshikamano wa kidugu; Mtoto Yesu ni jibu makini la upendo wa Mungu dhidi ya chuki, ubaya na uhasama; changamoto na mwaliko wa kujenga amani na kuendelea kuwasaidia wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kardinali Parolin ameishukuru familia ya Mungu nchini Iraq kwa mapokezi makubwa na ukarimu waliomwonesha tangu alipowasili nchini mwao na kwa namna ya pekee kwa upendo na mshikamano waliouonesha kwa wakimbizi na wahamiaji waliokimbilia hifadhi na usalama katika eneo hili kutokana na vita, dhuluma na nyanyaso kutoka Mosul, Uwanda wa Ninawi pamoja na maeneo mengine ya Iraq kuanzia mwaka 2014.

Wananchi hawa wamegeuza chuki na uhasama kwa kupandikiza ujirani mwema na mshikamano wa kidugu, dhana ambayo imeungwa mkono kwa hali na mali na Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa hakika hili ni jambo la kumshukuru Mungu. Tangu mwanzo, madhulumu dhidi ya Wakristo yamekuwa yakihusianishwa na mateso na kifo cha Kristo Yesu pamoja na wafuasi wake, walioyamimina maisha kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Kardinali Parolin anakaza kusema, Kristo Yesu ni mwanga wa Mataifa unaofyekelea mbali giza na ubaya wa moyo na kwamba, Kristo ni Mwokozi wa ulimwengu na kwamba, wale wote wanaompokea wanafanyika kuwa ni watoto wateule wa Mungu. Mtoto Yesu ni chemchemi ya furaha, utimilifu wa maisha, ukweli na ufunuo wa wema na huruma ya Mungu kwa waja wake na kwamba, Kristo Yesu ni amani ya waja wake! Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu, Neno wa Baba wa milele amekuwa karibu sana na binadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi. Katika maisha na utume wake, hakuondoa mateso na maumivu, bali ameyageuza kuwa ni nguvu ya upendo, kielelezo cha utimilifu wa maisha na chemchemi ya furaha ya kweli!

Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Watoto Mashahidi, waliouwawa kikatili kama njia ya kumshuhudia Kristo Yesu, hata kama hawakuwa wanamfahamu. Wameyamimina maisha yao, hata kabla ya kuanza kuzungumza, kiasi cha kupewa zawadi ya neema ya kumkiri Kristo na hivyo kupata ushindi. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutangaza na kushuhudia wema na upendo unaovunjilia mbali uhasama na ubaya wa moyo, kama walivyofanya Mashuhuda wa imani na wafiadini mbali mbali ndani ya Kanisa. Hawa sasa wamekirimiwa ushindi na maisha ya uzima wa milele.

Iraq ni Kanisa linalopambwa kwa damu ya mashuhuda wa imani, amana na utajiri mkubwa wa Kanisa na kwamba, damu yao ni mbegu ya Ukristo mpya! Kumbe, Wakristo huko Mashariki ya Kati, wanahamasishwa kuishi kwa furaha; kwa kutangaza na kushuhudia imani yao kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko, daima wakionesha upendo na msamaha; kwa kuendelea kuwa ni wajenzi wa umoja, na mshikamano wa kitaifa; kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Kwa njia hii, wataweza kuwa kweli ni wajenzi wa haki, amani na upatanisho, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya umoja na wokovu kwa watu wote. Kumbe, waamini wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa nchi yao.

Kardinali Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika ziara yake ya kichungaji nchini Iraq amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali ya Iraq na hivyo kugusia umuhimu wa ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Ametembelea taasisi mbali mbali zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa na kujionea mwenyewe hali ilivyo!

Watoto Mashahidi

 

28 December 2018, 10:02