Kardinali Pietro Parolin kuanzia tarehe 24-28 Desemba 2018 anatembelea Iraq: mshikamano wa kidugu! Kardinali Pietro Parolin kuanzia tarehe 24-28 Desemba 2018 anatembelea Iraq: mshikamano wa kidugu! 

Kardinali Parolin: Mshikamano na familia ya Mungu nchini Iraq!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia mkesha wa Noeli, yaani tarehe 24 hadi tarehe 28 Desemba 2018 yuko nchini Iraq kama kielelezo cha mshikamano wa umoja na udugu wa watoto wa Mungu, hasa katika eneo hili ambalo limegeuka kuwa ni uwanja wa vita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Uso wa Mungu umefunuliwa katika uso wa mwanadamu, aliyezaliwa katika wakati na mahali. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwana wa Mungu amewafunulia walimwengu kwamba, wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu unafumbatwa katika: upendo, ukarimu, utu na heshima ya binadamu; utu ambao watu wote wanashirikishana licha ya tofauti zao za kikabila, lugha na tamaduni, lakini wote wanajisikia kuwa ni sehemu ya udugu wa binadamu! Ni kutokana na mshikamano wa kidugu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia mkesha wa Noeli, yaani tarehe 24 hadi tarehe 28 Desemba 2018 yuko nchini Iraq kama kielelezo cha mshikamano wa umoja na udugu wa watoto wa Mungu, hasa katika eneo hili ambalo limegeuka kuwa ni uwanja wa vita.

Kardinali Parolin katika ziara hii ya kikazi huko Iraq anaambatana na Kardinali Louis Raphaël I Sako, Patriaki wa Kanisa la Babilonia ya Wakaldayo. Katika mkesha wa Noeli, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kielelezo cha upendo na mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi hiki kigumu cha historia yao. Akiwa nchini humo, Kardinali Parolin atatembelea eneo ambalo kunako mwaka 2010, umati mkubwa wa Wakristo uliuwawa kutokana na vitendo vya kigaidi. Anakutana pia na viongozi wa Serikali pamoja na kutembelea Uwanda wa Ninawi na kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu huko.

Kwa upande wake, Askofu msaidizi Shlemon Warduni wa Jimbo kuu la Baghdad, Iraq katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, hija ya kikazi ya Kardinali Parolin nchini Baghdad wakati huu wa Noeli ni alama ya upendo na mshikamano, unaopania kuwatia shime Wakristo kuendelea kuishi huko Mashariki ya kati licha ya changamoto kubwa wanazokabiliana nazo, kiasi hata cha wengi wao kukimbia Iraq ili kutafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya Wakristo millioni moja wamekimbia kutoka Iraq kutokana na dhuluma, nyanyaso na vita. Jumuiya Ndogo ya Wakristo huko Iraq inaendelea kuwa ni shuhuda wa imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, anayewatia nguvu ya kuendelea kubaki huko Mashariki ya Kati mintarafu utashi wa Baba wa mbinguni! Wakristo wanaendelea kusali na kuombea amani huko Mashariki, wakiwa na matumaini kwamba, iko siku isiyokuwa na jina, Baba Mtakatifu Francisko atawatembelea.

Askofu msaidizi Shlemon Warduni anasikitika kuona kwamba, watu wamemezwa mno na malimwengu, kiasi kwamba, wameelemewa na uchu wa mali na madaraka; wanatafuta utajiri wa haraka haraka na matokeo yake ni uvunjwaji wa haki msingi za binadamu na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Wananchi wa Iraq wanatamani kuona amani ikitawala katika akili na nyoyo zao ndiyo maana wanapenda kuungana na Kardinali Pietro Parolin kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani, lakini zaidi huko Mashariki ya Kati.

Parolin: Iraq
25 December 2018, 16:32