Tafuta

Vatican News
Huduma ya afya inapaswa kuzingatia: usawa, haki, utu na heshima ya binadamu! Huduma ya afya inapaswa kuzingatia: usawa, haki, utu na heshima ya binadamu! 

Huduma kwa wagonjwa: Zingatieni: Usawa, haki, utu na heshima!

Huduma hii inapaswa kujikita katika usawa na haki, kwa kuzingatia utu na heshima ya wagonjwa wote, hata kama wako kufani! Vatican kwa sasa imeweka sera na mkakati wa kuendelea kuwekeza zaidi katika vifaa tiba na tafiti kama sehemu ya maboresho ya huduma ya upendo kwa watoto wadogo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 21 Desemba 2018 ametembelea Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya  Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2018. Uwepo wake, umekuwa ni ushuhuda endelevu wa huduma ya Injili ya upendo inayotolewa na Mama Kanisa. Katika mahubiri yake, amewapatia salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayewatakia heri na baraka, ili waweze kupona haraka na kurejea tena kwenye familia zao.

Kwa wazazi, walezi na wafanyakazi wa Hospitalini hapo, amewatakia matumaini katika huduma bora inayotolewa hospitalini hapo, kwa kuendelea kujiaminisha na kujinyenyekesha mbele ya Mungu sanjari na kutimiza mapenzi yake kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kwa njia hii, hata wao katika shida na mahangaiko yao, wataweza kuadhimisha kwa imani na matumaini, Fumbo la Umwilisho. Kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, watambue na kuthamini wajibu na dhamana yao inayofumbatwa katika kanuni maadili na utu wema; tunu msingi za maisha ya kiroho, na daima wasukumwe  kutenda kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu na wala si kadiri ya taaluma na teknolojia ya tiba ya mwanadamu.

Kardinali Parolin anawakumbusha wafanyakazi katika sekta ya afya kwamba, wao  ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa. Kwa wafanyakazi wa Hospitali ya Bambino Gesù wanamsaidia Baba Mtakatifu kutangaza na kushuhudia Injili huduma ya upendo kama sehemu ya utume wake kwa watu wa Mungu. Baada ya maadhimisho ya Misa Takatifu, Kardinali Parolin, amewatembelea na kuwabariki watoto wagonjwa kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ambao wanahudumiwa hospitalini hapo kwa utashi wa Baba Mtakatifu Francisko baada ya kutembelea Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na kuzindua huko maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka wa Huruma ya Mungu.

Kardinali Parolin amekazia umuhimu wa wafanyakazi wa Hospitali ya Bambino Gesù kufanya tafiti ili kuboresha tiba kwa watoto wagonjwa wanaotibiwa ndani na nje ya Hospitali hii. Huduma hii inapaswa kujikita katika usawa na haki, kwa kuzingatia utu na heshima ya wagonjwa wote, hata kama wako kufani! Vatican kwa sasa imeweka sera na mkakati wa kuendelea kuwekeza zaidi katika vifaa tiba na tafiti kama sehemu ya maboresho ya huduma ya upendo kwa watoto wadogo.

Hospitalini hapa ni mahali pa kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo na huruma ya Mungu; mahali ambapo wahudumu wa sekta ya afya wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa ajili ya huduma kwa watoto wagonjwa. Kila mfanyakazi katika nafasi na dhamana yake, ajivike fadhila ya unyenyekevu katika huduma; kwa kukuza na kudumisha nia njema inayomwilishwa katika huduma ya upendo mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Fumbo la Umwilisho ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake!

Kardinali Parolin anakaza kusema, upendo ni kielelezo cha Fumbo la Umwilisho linalotoa upendeleo wa pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kumbe, Hospitali ya Bambino Gesù inapaswa kutoa upendeleo wa pekee kwa maskini na watoto wanaotoka pembezoni mwa jamii. Hii ni hospitali kadiri ya mawazo ya Baba Mtakatifu Francisko ya watoto wote wa ulimwengu huu!

Bambino Gesù: Watoto
23 December 2018, 15:29