Tafuta

Vatican News
Kardinali Parolin: Fumbo la Umwilisho ni chachu ya mabadiliko na upyaisho wa maisha ya binadamu! Kardinali Parolin: Fumbo la Umwilisho ni chachu ya mabadiliko na upyaisho wa maisha ya binadamu!  (AFP or licensors)

Fumbo la Umwilisho ni chachu ya mabadiliko na upyaisho wa maisha

Kipindi cha Noeli, ni muda wa kupandikiza Habari Njema ya Wokovu, kwani “Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu”. Huyu ni Neno wa upendo, upatanisho, haki na amani inayozima kiu na matamanio halali ya binadamu. Neno wa Mungu amefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake, hiki ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu, kwani Kristo Yesu aliyezaliwa ni Mwana wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 25 Desemba 2018, Sherehe ya Noeli yaani: kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, Mwanga wa Mataifa; Emmanueli, yaani Mungu pamoja na watu wake, Mfalme wa Amani na chemchemi yaa furaha na matumaini ya watu wake, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Wakristo wa Madhehebu ya Kilatini, Jimbo kuu la Baghdad na kuhudhuriwa na umati mkubwa waamini, viongozi wa Serikali na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao huko Iraq. Fumbo la Umwilisho ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu!

Kardinali Parolin anasikitika kusema kwamba, katika miaka ya hivi karibuni, Iraq na hata sehemu mbali mbali za dunia, imeendelea kusikia habari mbaya kuhusu: vita, vitendo vya kigaidi na kwa hakika watu wengi wameteseka sana. Lakini, Kipindi cha Noeli, ni muda wa kupandikiza Habari Njema ya Wokovu, kwani “Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu”. Huyu ni Neno wa upendo, upatanisho, haki na amani inayozima kiu na matamanio halali ya binadamu. Neno wa Mungu amefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake, hiki ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu, kwani Kristo Yesu aliyezaliwa ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa ulimwengu.

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwa kusema, ukuu na utukufu wa Mungu umefunuliwa katika hali na unyenyekevu wa mtoto mchanga. Kwa njia ya utimilifu wake, wote wamepokea neema juu ya neema! Fumbo la Umwilisho ni chachu ya mabadiliko na upyaisho wa maisha ya binadamu, kwani Mungu yu pamoja na watu wake; sasa anafahamika na watu wanaweza kujenga mahusiano na mafungamano ya karibu. Kwa njia ya Mtoto Yesu, waamini wanaalikwa kutafakari huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, tayari kumpokea Mtoto Yesu na kumkaribisha katika maisha, ili hata wao pia waweze kufanyika kuwa ni watoto wa Mungu, kwa kuguswa na wema na huruma ya Mungu inayookoa!

Uzuri wa Noeli ni pale waamini wanapotambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, uwepo wake endelevu unapyaisha undani wa maisha yao, ili kuishi kama watoto wa Mungu, kwa kukita maisha yao katika upendo, msamaha na kuheshimiana; kwa kukuza na kudumisha amani na utulivu. Maadhimisho ya Noeli ni changamoto ya kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa Iraq mpya; kwa kuendeleza mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Kardinali Parolin anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, wakristo huko Mashariki ya Kati, wanapaswa kuwa ni vyombo na wajenzi wa upatanisho, haki na amani; upendo na msamaha; umoja na udugu; huduma na upendo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, mara nyingi, umekuwa ni chanzo cha mateso, dhuluma na nyanyaso kiasi hata cah kupelekea kifo. Ushuhuda huu ni amana na utajiri wa Kanisa, jambo la msingi ni kwa waamini ni kuendelea kuwa thabiti katika imani na mapendo.

Kardinali Parolin: Noeli 2018

 

26 December 2018, 15:15