Cerca

Vatican News
Parokia ni mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu! Parokia ni mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu!  (Vatican Media)

Parokia ni mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu

Neno Parokia, linapata asili yake kutoka katika lugha ya Kigiriki yaani “παρоικια” maana yake “Ujirani”. Kumbe, kwa maneno machache, Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Adhimisho la  Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa ni kiini cha Parokia. Kimsingi, Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa siku ya Bwana; Jumuiya ya waamini inapopata nafasi ya kusikiliza, kutafakari Neno la Mungu na hatimaye, kutumwa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo cha imani ntendaji! Neno Parokia, linapata asili yake kutoka katika lugha ya Kigiriki yaani “παρоικια” maana yake “Ujirani”. Kumbe, kwa maneno machache, Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu.

Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa mwaka 2018 wamekazia umuhimu wa Kanisa kupyaisha maisha na utume wa Parokia, ili kuleta mvuto na mashiko kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na waamini katika ujumla wao, ili kujenga familia ya Mungu inayowajibikiana katika: imani, matumaini na mapendo. Parokia ya Mtakatifu Anna iliyoko ndani ya Vatican, imekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wake, hasa kipindi hiki cha Majilio, kwa kuwasaidia waamini kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya Sherehe ya Noeli kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu, Maisha ya Sala na Matendo ya huruma kwa maskini na wahitaji zaidi.

Waamini parokiani hapo, wamekuwa mstari wa mbele kuchangia katika malezi na majiundo ya majandokasisi ambao wanatoka katika familia zenye uwezo mdogo wa kiuchumi, kwa kuwalipia ada ya shule na masomo. Wanawake wamekuwa mstari wa mbele kuwasaidia wenzao wanaopambana na hali ngumu ya maisha, kwa njia ya mshikamano wa upendo unaofumbatwa katika kanuni auni! Waamini kila mmoja kadiri ya taaluma, kipaji na uwezo wake, anashirikiana na wenzake katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.

Waamini wanasaidiana katika changamoto zinazohitaji watalaam wa sheria, kanuni na taratibu za Kanisa, msaada unaotolewa na wanataaluma Wakristo Parokiani hapo. Wao pia wamekuwa mstari wa mbele katika majiundo awali na endelevu kuhusiana na historia ya Kanisa, kanuni maadili na utu wema; mambo yanayofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa. Monsinyo Guido Marini, Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa, licha ya shughuli zake zote, yuko pia mstari wa mbele katika kufundisha maisha ya sala la liturujia ya Kanisa kwa ajili ya utukufu wa Mungu na wokovu wa mwanadamu!

Vyama na Mashirika ya Kitume, yameendelea kuwa mstari wa mbele katika maisha na utume wa Parokia, kiasi hata cha Baba Mtakatifu Francisko kuwapongeza kwa juhudi zao za kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Kardinali Prosper Grech, kila siku ya Jumatano jioni, anatoa kipindi kuhusu tasaufi ya Nyaraka za Mtakatifu Paulo, ili kuwajengea waamini hamu ya kufahamu na kupenda Neno la Mungu linalopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha yao kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, walei, kama washiriki wa huduma ya Kristo kuhani, nabii na mfalme, wanayo nafasi hai katika maisha ya Kanisa na katika utendaji wake. Ndani ya jumuiya za Kanisa matendo yao yanahitajika sana, kiasi kwamba pasipo haya hata utume wenyewe wa wachungaji huwa hauwezi kufikia mafanikio kamili. Maana walei wenye roho halisi ya kitume, kama wale wanaume na wanawake waliokuwa wakimsaidia Paulo katika kueneza Injili (taz. Mdo 18:18.26; Rum 16:3), wanawakirimia ndugu zao yale waliyopungukiwa, na wanaburudisha roho za wachungaji na za waamini wengine wa taifa la Mungu (taz. 1Kor 16:17-18).

Huku wakilishwa na mahudhurio hai katika maisha ya kiliturujia ya jumuiya yao, wanashiriki kwa bidii katika kazi zake za kitume; wanawaongoza watu ambao labda wako mbali na Kanisa, wapate kuliingia; wanasaidia kwa moyo katika kupasha Neno la Mungu, hasa kwa njia ya kufundisha katekisimu; wakichangia ubingwa wao wanaleta ufanisi zaidi katika uangalizi wa roho na usimamizi wa mali ya Kanisa.

Parokia ni mfano mwangavu wa utume wa kijumuiya; kwa kuunganisha pamoja tofauti za watu ambao wanaishi katika eneo lake na kwa kuziingiza uwepo wao. Waamini walei wazoee kufanya kazi parokiani bega kwa bega na mapadre wao, kuieleza jumuiya ya Kanisa matatizo yao wenyewe na ya ulimwengu, na masuala yanayohusu wokovu wa wanadamu, ili yachunguzwe na kutatuliwa kwa mchango wa wote; wazoee pia kujitoa kwa bidii, kulingana na uwezo wa kila mmoja, kwa tendo lolote la kitume na la kimisionari la jamaa yao ya kikanisa.

Parokia Kitovu Uinjilishaji
19 December 2018, 09:59