Tafuta

Papa Francisko, tarehe 15 Desemba 2018 amekutana na kuzungumza na Giuseppe Conte, Waziri Mkuu wa Italia. Papa Francisko, tarehe 15 Desemba 2018 amekutana na kuzungumza na Giuseppe Conte, Waziri Mkuu wa Italia. 

Papa Francisko akutana na Waziri Mkuu wa Italia, Conte!

Papa Francisko na Wziri mkuu Conte wamejadili: athari za mabadiliko ya tabianchi; huduma ya ukarimu na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji mintarafu Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018 pamoja na Mkutano 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP 24 Katowice, pamoja na umuhimu wa kulinda na kudumisha amani duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 15 Desemba 2018, amekutana na kuzungumza kwa faragha na Giuseppe Conte, Waziri mkuu wa Italia aliyekuwa ameandamana na Bwana Pietro Sebastiani, Balozi wa Italia mjini Vatican. Baba Mtakatifu na Waziri mkuu wa Italia, katika mazungumzo yao, wamejielekeza zaidi katika masuala ya kimataifa hususan athari za mabadiliko ya tabianchi; huduma ya ukarimu na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji mintarafu Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018 pamoja na Mkutano 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP 24 Katowice, Poland pamoja na umuhimu wa kulinda na kudumisha amani duniani.

Mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na Waziri mkuu wa Italia Bwana Conte, yamedumu kwa takribani dakika 45, ambamo wamejadili masuala tete kati ya Vatican na Serikali ya Italia na kwamba, pande zote mbili zitaendelea kufanya mageuzi ya kina kadiri ya mamlaka yake. Hivi ndivyo alivyoandika Bwana Conte katika ukurasa wake wa Facebook baada ya mazungumzo yake na Baba Mtakatifu Francisko. Anakaza kusema, wamepembua kwa kina na mapana ukosefu wa usawa na haki jamii; wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na umuhimu wa kukuza na kudumisha amani.

Waziri mkuu Conte anakazia kwamba, mkutano wake na Baba Mtakatifu umekuwa na umuhimu wa pekee katika maisha yake, kwani umemsaidia kupyaisha dhamana na nafasi yake katika siasa, kanuni maadili na utu wema pamoja na umuhimu wa kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maboresho ya: ustawi, maendeleo na familia ya Mungu nchini Italia katika masuala ya kijamii na kiuchumi.

Baadaye, viongozi hawa wamebadilishana zawadi, kwa Waziri mkuu Conte kumtakia heri na baraka, Baba Mtakatifu Francisko ambaye, tarehe 17 Desemba 2018 anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 82 tangu alipozaliwa. Baba Mtakatifu amemzawadia Waziri mkuu Conte Waraka wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ambao ulizinduliwa kunako mwaka 2015. Waraka huu unakazia utunzaji bora wa mazingira kuwa ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo endelevu na fungamani kwa sababu, mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu amempatia pia medali yenye picha ya majani ya mti wa mzeituni, alama ya amani na upatanisho.

Papa: Waziri Mkuu Conte
17 December 2018, 07:46