Tafuta

Utume wa Kanisa katika Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu: Katiba ya Kitume: Furaha ya Ukweli! Utume wa Kanisa katika Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu: Katiba ya Kitume: Furaha ya Ukweli! 

Utume wa Vyuo vikuu katika mwanga wa ukweli!

Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kuanzia tarehe 3-4 Desemba 2018 limeadhimisha Semina ya Kimataifa kuhusu utume wa shughuli za kichungaji kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, kama sehemu ya mchakato wa huduma ya ukweli. Wataalam na mabingwa wa shughuli za kichungaji walishirikishana: mang’amuzi, fursa, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katiba ya Kitume “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” iliyoidhinishwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Desemba 2017, na kuchapishwa rasmi tarehe 29 Januari 2018 ni mwongozo makini unaovihusu vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, kama sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa yanayowagusa na kuwaambata watu wa Mungu, katika mwelekeo mzima wa utekelezaji wa utume wa uinjilishaji mpya.

Hii ni dhamana inayojikita katika mang’amuzi, utakaso na mageuzi ya dhati yanayopania kupyaisha mfumo mzima wa elimu inayotolewa na Mama Kanisa, katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu. Katiba hii ni mwongozo na mbinu mkakati katika mageuzi ya elimu inayopania kumpatia mwanadamu furaha ya ukweli katika maisha yake. Hii ni “Furaha ya ukweli” unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Neno wa Mungu ambaye ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu; ni njia, ukweli na uzima. Ni kiungo muhimu cha umoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na umoja kati ya watoto wa Mungu, kwani Roho Mtakatifu ni: Roho wa ukweli na upendo; uhuru, haki na umoja.

Uinjilishaji na utamadunisho ni chanda na pete katika maisha na utume wa Kanisa unaojikita pia katika majadiliano na tamaduni mbali mbali kwa kusoma alama za nyakati, ili kuliwezesha Kanisa kujipyaisha zaidi kama walivyokazia Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wao wa “Optatam totius” yaani “Mwongozo wa Malezi ya Kipadre” kwa kuzingatia uhamasishaji wa miito na majiundo makini ya Mapadre, ili kuwawezesha kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa, kwa kumfuasa Kristo Mchungaji mwema anayewapatia: utambulisho, tasaufi na utume wanaopaswa kuutekeleza katika mwanga wa “Furaha ya ukweli”.

Kwa mara ya kwanza, katika historia ya Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kuanzia tarehe 3-4 Desemba 2018 limeadhimisha Semina ya Kimataifa kuhusu utume wa shughuli za kichungaji kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, kama sehemu ya mchakato wa huduma ya ukweli. Wataalam na mabingwa wa shughuli za kichungaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, walishirikishana: mang’amuzi, fursa, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika kutangaza na kushuhudia furaha ya ukweli katika taasisi hizi ambazo kimsingi kwa sasa zinakabiliana na mageuzi makubwa na yanayofanyika kwa haraka. Wajumbe wanasema kwamba, licha ya tofauti msingi za mahali wanakotoka na kufanyia utume wao, lakini wote wanaunganishwa na Roho Mtakatifu, ili kutangaza na kushuhudia Ukweli mfunuliwa ambao ni Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kumbe, kuna umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, kiekumene, kitamaduni na kisayansi, kama kielelezo msingi cha huduma ya uaminifu katika ukweli.

Kati ya changamoto zilizojitokeza katika semina hii ni pamoja na jinsi ya kuwasindikiza wanafunzi, waalimu na watafiti, ili kuweza kujiweka wazi na hatimaye, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukweli. Wajumbe wanasema, wanapata taabu sana kuweza kuamsha karama na miito mbali mbali kutoka kwa wafanyakazi katika sekta ya elimu, ili kweli huduma hii iweze kuacha chapa ya kudumu na maana katika maisha yao, kwa kujikita katika fadhila zinazopania kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; haki na amani; usawa, udugu, upendo na mshikamano; sanjari na kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha mazingira nyumba ya wote.

Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kama sehemu ya mbinu mkakati wa utekelezaji wa dhamana na majukumu yake, linataka kuhakikisha kwamba, utume wa shughuli za kichungaji unamwilishwa vyema katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, kama jukwaa la kubadilishana mawazo na changamoto za maisha. Lengo ni kudumisha mchakato wa uinjilishaji wa pamoja, endelevu na fungamani unaopania pamoja na mambo mengine ni: kujenga na kudumisha ulimwengu ambao unajikita katika haki, umoja na udugu. Kwa siku za mbeleni, kutakuwepo na mikutano pamoja na semina mbali mbali zinazopania kukoleza mchakato wa majiundo fungamani, ili cheche za “furaha ya ukweli wa Injili” ziweze kumwilishwa katika mila, desturi na tamaduni mbali mbali duniani!

Utume: Vyuo Vikuu
08 December 2018, 16:39