Papa Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume huko Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, Februari 2019 Papa Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume huko Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, Februari 2019 

Papa Francisko: Hija ya Kitume Falme za Kiarabu: Ratiba elekezi

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu ataondoka mjini Roma, Jumapili jioni tarehe 3 Februari na kuwasili majira ya saa 4:00 za usiku kwa saa za Abu Dhabi. Jumatatu, tarehe 4 Februari, atafanyiwa mapokezi ya kitaifa; atamtembelea Mfalme Mrithi Mohammed bin Zayed Al Nahyan. Jioni, Baba Mtakatifu atafanya mkutano wa faragha na Baraza Kuu la Wazee wa Kiislam.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, kuanzia tarehe 3 hadi 5 Februari 2019, anatarajia kufanya hija ya kitume ya ishirini na saba huko Abu Dhabi, kwenye Falme za Kiarabu, ili kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini unaoongozwa na kauli mbiu "Udugu wa kibinadamu". Akiwa huko kwenye Falme za Kiarabu, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa mahubiri yake pamoja na hotuba kwenye mkutano wa majadiliano ya kidini.

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu ataondoka mjini Roma, Jumapili jioni tarehe 3 Februari na kuwasili majira ya saa 4:00 za usiku kwa saa za Abu Dhabi. Jumatatu, tarehe 4 Februari, Baba Mtakatifu atafanyiwa mapokezi ya kitaifa na hatimaye, kumtembelea Mfalme Mrithi Mohammed bin Zayed Al Nahyan. Jioni, Baba Mtakatifu atafanya mkutano wa faragha na Baraza Kuu la Wazee wa Kiislam, katika Msikiti mkuu wa Sheikh Zayed na baadaye kushiriki katika mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa kuhusu udugu wa kibinadamu, ulioandaliwa na Mfuko wa Kumbu kumbu ya Mwanzilishi wa Ghuba ya Uajemi.

Hatimaye, tarehe 5 Februari 2019, Baba Mtakatifu Francisko atafanya ziara binafsi ya kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu Abu Dhabi ambalo liko karibu na Kanisa la Mtakatifu Paulo katika eneo la Musaffah. Baadaye, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa Zayed na baadaye, ataaga na kuondoka kurejea tena mjini Vatican kuendelea na shughuli zake za kitume!

Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, ameshiriki katika uzinduzi wa Kanisa lililojengwa kwa heshima ya Mtume Paulo huko Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii inayojikita katika misingi ya maridhiano, haki, umoja na mshikamano wa kidugu, licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza. Kardinali Parolin aliwashukuru viongozi wa Falme za Kiarabu kwa kuonesha utayari wa kushirikiana katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; kwa kuimarisha uhuru wa kidini; haki na amani; maridhiano na udugu kati ya watu wa Mataifa, ili waweze kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kwa upande wake Askofu Paul Hinder, Mwakilishi wa Kitume katika Falme za Kiarabu anasema, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko ni tukio muhimu sana katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini kati ya Waislam na Wakristo; ili kusimamia haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo ya wananchi wengi huko Mashariki ya Kati. Hii ni hija ya kihistoria kwani kwa mara ya kwanza katika historia na maisha ya Kanisa, Khalifa wa Mtakatifu Petro anatembelea Falme za Kiarabu. Wanapenda kumpokea na kumkaribisha kwa moyo mkunjufu katika hija hii ya kitume inayoongozwa na kauli mbiu “Nifanye chombo cha amani”. Wananchi wa Falme za Kiarabu wanamwona Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni kielelezo cha amani, maridhiano na udugu; mambo msingi yanayoweza kuimarisha majadiliano katika ukweli na uwazi; amani na utulivu kati ya watu wa Mataifa.

Papa: Abu Dhabi

 

 

 

15 December 2018, 15:06