Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018 umridhiwa na nchi 164 Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018 umridhiwa na nchi 164 

Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018 waridhiwa!

Kuanzia tarehe 10 - 11 Desemba 2018, huko Marrakesh, nchini Morocco zaidi ya vyama 600 vya kiraia vimeshiriki kusikiliza tamko la viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu Mkataba wa Usalama wa Wahamiaji 2018 kutoka katika nchi 164. Vatican imechangia sana katika maboresho ya Mkataba huu na sasa ingependa kuona utekelezaji wake katika ngazi ya kimataifa na kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kimsingi “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unapania pamoja na mambo mengine: kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa, kiasi cha kutishia umoja na mshikamano wa kimataifa katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia!

Kuanzia tarehe 10 - 11 Desemba 2018, huko Marrakesh, nchini Morocco zaidi ya vyama 600 vya kiraia vimeshiriki kusikiliza tamko la viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu Mkataba wa Usalama wa Wahamiaji 2018 kutoka katika nchi 164. Vatican imechangia sana katika maboresho ya Mkataba huu na sasa ingependa kuona utekelezaji wake katika ngazi ya kimataifa kwa kukazia mambo makuu ishirini yanayopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa. Mambo yote haya yanafumbatwa katika amani, maendeleo fungamani na ushirikishwaji wa watu kama kielelezo cha utandawazi wa mshikamano wa upendo, unaoguswa na shida pamoja na mahangaiko ya wengine!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake amekazia umuhimu wa mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, badala ya kuwa na sera na mbinu mkakati unaojikita katika utengano na ubaguzi! Uwajibikaji na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa ni mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza wakimbizi na wahamiaji kwa kujikita katika usalama, kanuni na taratibu za uhamiaji.

Vatican inaunga mkono Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji, ingawa baadhi ya vipengele vyake vinasigana kimsingi na Mafundisho Jamii ya Kanisa! Huu ni Mkataba ikiwa kama utatekelezwa kikamilifu, utaisaidia Jumuiya ya Kimataifa kuratibu changamoto ya wakimbizi na wahamiaji duniani kwa ufanisi mkubwa. Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowakirimia; mambo yanayofafanuliwa kwa kina na mapana na Baba Mtakatifu Francisko.

Vipengele hivi vinaondoa vitendo vya ubaguzi ambavyo mara nyingi wakimbizi na wahamiaji wanakumbana navyo katika safari zao. Nchi wahisani zinapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuongozwa na busara, ili kupima na kuangalia uwezo wa kila nchi katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji pamoja na kuwashirikisha katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi! Kardinali Parolin amekazia pia umuhimu kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inadhibiti kikamilifu mambo yote yanayosababisha uhamiaji haramu na ule wa shuruti, kwani kila mtu anayo haki ya kubaki nchini mwake kwa amani na utulivu. Jambo hili linawezekana ikiwa kama mambo yote yanayochangia uhamiaji wa shuruti na haramu yatadhibitiwa kikamilifu.

Mambo haya ni kama vile: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; athari za mabadiliko ya tabia nchi; umaskini mkubwa wa hali na kipato. Kumbe, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, vita na mipasuko ya kijamii inapata suluhu ya kudumu pamoja na kuwekeza zaidi katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji msingi ya binadamu; utu na heshima yake.

Wakati huo huo, Kardinali Parolin, ameshiriki pia katika mkutano wa majadiliano ya kwanza kuhusu uragibishaji wa utekelezaji wa “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” kwa kukazia umuhimu wa utekelezaji wa maazimio yaliyomo kwenye Mkataba huo. Juhudi hizi za Jumuiya ya Kimataifa hazina budi kujikita katika utunzaji wa amani kwa kuzingatia sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani katika maisha ya binadamu! Haki msingi za binadamu; utu na heshima yake ni mambo msingi ambayo yanapaswa kuzingatiwa ili watu waweze kujisikia huru katika nchi zao na kwamba, hakuna sababu ya kuogopa kunyanyaswa, kudhulumiwa au kutengwa kwa sababu yoyote ile!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anakaza kusema, wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika maisha na mazingira ya nchi wahisani; kama sehemu ya mchakato unaoheshimu na kuzingatia utu wa binadamu. Wahamiaji wapewe fursa ya kuweza kuungana tena na familia zao hata pale wanapokuwa ugenini. Mchakato huu utasaidia kuondokana na maamuzi mbele, ubaguzi, nyanyaso na dhuluma dhidi ya wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Hadi sasa Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018 umekwisha ridhiwa na nchi 164. Baadhi ya nchi ambazo hazikuridhia Mkataba huu ni pamoja na Marekani, Poland, Hungaria, Jamhuri ya Watu wa Czech, Israeli, Australia, Slovakia, Austria na Latvia. Nchi ya Italia pamoja na Uswis, zimesema kwamba, Mkataba huu utapaswa kujadiliwa na Mabunge yao, kabla ya kuridhiwa!

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antònio Guterres amewahakikishia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kwamba, Mkataba huu hauingilii uhuru wa nchi husika, wala kuunda haki mpya za wakimbizi, bali jambo la msingi hapa ni kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, kwa kuwa na uhamiaji salama, unaozingatia kanuni na sheria za Jumuiya ya Kimataifa. Hii ni hatua kubwa dhidi ya biashara haramu ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo.

Kardinali Parolin

 

12 December 2018, 10:14