Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2018: Mkazo: Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu. Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2018: Mkazo: Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu. 

Sherehe za Noeli: Kipaumbele: Sakramenti ya Upatanisho & Ekaristi Takatifu

Fumbo la Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, anapata mwanga wa pekee katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho, ili Kristo Yesu anayezaliwa aweze kuwatakasa, kuwakomboa na kuwapyaisha, ili hatimaye aweze kuzaliwa tena katika nyoyo za waamini wanaotubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume katika barua yake kwa waungamishaji wa Makanisa makuu ya Jimbo kuu la Roma pamoja na waungamishaji sehemu mbali mbali za dunia wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa mwaka 2018, anawataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu kama sehemu muhimu sana ya maadhimisho ya Fumbo la kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Neno wa Mungu na kama ambayo Mama Kanisa anakazia katika mwaka mzima wa Liturujia ya Kanisa.

Kardinali Mauro Piacenza anaendelea kufafanua kwamba, Mama Kanisa katika maadhimisho ya Fumbo la Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, anapata mwanga wa pekee katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho, ili Kristo Yesu anayezaliwa aweze kuwatakasa, kuwakomboa na kuwapyaisha, ili hatimaye aweze kuzaliwa tena katika nyoyo za waamini wanaotubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Ingawa Kanisa ni takatifu, lakini daima linahitaji kutakaswa, kwa kumwangalia Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama asiye na doa “Tota Pulchra”, ambaye alibahatika kupata neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kuwafungulia watu, Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwili.

Kardinali Piacenza anakaza kusema, Mama Kanisa daima anafurahia utukufu wa Bikira Maria asiyekuwa na doa la dhambi, ambaye daima anawaombea watoto wake, ili waweze kupata neema kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, kwa kujichotea neema kutoka katika chemchemi ya huruma ya Mungu yaani ubinadamu wa Mwana wa Mungu, ambaye alimwaga Damu yake Azizi katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa njia ya Roho Mtakatifu. Maungamo ya dhambi ni ushuhuda wa pekee kabisa unaowapatia waamini nafasi ya kujipatanisha na Baba wa milele pamoja na jirani zao; kwa njia ya Kristo Yesu aliyewakomboa na kuwapyaisha tena kwa neema ya Sakramenti ya Ubatizo, inayowashirikisha waamini maisha ya Kristo Yesu na hivyo kuwa ni sehemu hai ya Fumbo la Mwili uliozaliwa na Bikira Maria “Verum Corpus natum de Maria Virgine”.

Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, Mama Kanisa anajipatia tena watoto wapya, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, aliyezaliwa kwenye Pango la kulishia wanyama mjini Bethlehemu, ambako watu wengi wanamsubiria ili waweze kumpokea tena katika maisha yao. Mtoto Yesu aliyezaliwa Pangoni, anaendelea kutawala katika moyo wa Padre muungamishaji, akiendelea kusubiria muungamaji anayekuja kutubu ili kumwonesha sura ya Mwana wa Mungu. Mtakatifu Yosefu na Bikira Maria ni kielelezo angavu cha uaminifu aliokabidhiwa; mlinzi wa Fumbo lililofunuliwa na Baba mlishi, anayependa bila kutaka kumiliki na kwa hakika, anapenda kwa moyo wake wote!

Bikira Maria kwa utayari na uhuru wake, amekubali kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake kwa njia ya Roho Mtakatifu, akamchukua mimba Mwana wa Baba wa milele katika moyo wake, hata kabla ya kumpokea katika tumbo lake! Bikira Maria ni Mama wa ubinadamu anayetoa kwa muhtasari kazi ya wokovu inayotekelezwa na Kanisa, kwa kuendelea kumwezesha Padre muungamishaji kuwa kweli ni chombo hai na cha muhimu katika kazi nzima ya wokovu, ili Kristo Yesu, aweze kuzaliwa na kufufuka tena katika kila moyo wa mwamini anayetubu!

Kardinali Mauro Piacenza anawataka waungamishaji katika Makanisa makuu ya Jimbo kuu la Roma, kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwawezesha waamini kupyaisha maisha yao ya kiroho. Watambue kwamba, hii ni huduma adhimu wanayomtolea Mama Kanisa na kwamba, anawatakia wote heri na baraka kwa Sherehe ya Noeli na Mwaka Mpya 2019. Anawataka wawe kweli ni vyombo vya furaha ya huruma ya Mungu, wajivike ndani mwao huruma ya Mungu na kuwagawia wale wote watakaokimbilia kwenye kiti cha huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho!

Kardinali Piacenza

 

 

21 December 2018, 11:20