Cerca

Vatican News
Madhabahu ni nyumba ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Madhabahu ni nyumba ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.  (AF_SantuarioFatima)

Madhabahu ni nyumba ya huruma na upendo wa Mungu!

Madhabahu ni daraja la kuwakutanisha watu katika maisha ya kiroho! Waamini wengi wameweza kung’amua miito ya maisha na utume wao kwa kutembelea madhabahu. Hapa pia ni mahali pa toba na wongofu wa ndani; mahali pa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani; ni mahali pa kukimbilia huruma ya Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, madhabahu ni mahali pa ushuhuda wa imani, mapendo na matumaini ya watu wa Mungu. Ni mahali ambapo waamini wanapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi; kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima! Hapa, waamini wanapaswa kujisikia kweli wako nyumbani, kwa kupata amani na utulivu wa ndani, tayari kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, kwa kukutana na waamini wengine wanaofanya hija ya maisha ya kiroho, tayari kutangaza na kushuhudia: ukuu, wema, huruma na utakatifu wa Mungu unaofumbatwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Madhabahu ni daraja la kuwakutanisha watu katika maisha ya kiroho! Waamini wengi wameweza kung’amua miito ya maisha na utume wao kwa kutembelea madhabahu. Hapa pia ni mahali pa toba na wongofu wa ndani; mahali pa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani; ni mahali pa kukimbilia huruma ya Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu! Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni sehemu ya familia kubwa ya watu wa Mungu, kumbe, daima wako chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Waamini ni sehemu ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kumbe, kama sehemu ya Kanisa, wanao wajibu na dhamana ya kuliombea Kanisa zima; kuwaombea watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali; watu wanaoogelea katika dimbwi la huzuni na machungu ya maisha; wagonjwa na wale wote walioko kufani; wakimbizi na wahamiaji bila kuwasahau watu wanaoteseka kutokana na athari za majanga asilia.

Upembuzi huu yakinifu umetolewa hivi karibuni na Kardinali Beniamino Stella Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Wakleri wakati wa kuadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, tarehe 8 Desemba 2018 kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, yaliyoko nchini Italia. Anakaza kusema, madhabahu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu; ni daraja la kuwakutanisha waamini na Mwenyezi Mungu, tayari kujenga mahusiano na mafungamano na jirani zao katika sala na huduma. Ni mahali pa utulivu, sala, tafakari ya Neno la Mungu, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na Ibada kwa Bikira Maria.

Kardinali Beniamino Stella anakaza kusema, waamini kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani, wanaweza kumpokea Kristo Yesu kwa moyo wa furaha, inayomwilishwa katika huduma ya mapendo katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Madhabahu yanapaswa kuangaliwa kama jukwaa la kujifunzia tunu msingi za maisha ya kifamilia; yaani: umoja na udugu; upendo na mshikamano; majadiliano, tayari mtu kuweza kujipokea jinsi alivyo na kuwapokea wengine walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, pamoja na kuwapatia nafasi ya kukua na kukomaa katika maisha na vipaumbele vyao. Baba Mtakatifu Francisko anasema madhabahu ni nyumba ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu mwaliko na changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutembelea mara kwa mara kwenye madhabahu ili kujipatia mang’amuzi mapya katika safari ya maisha yao!

Madhabahu Nyumba ya Sala
17 December 2018, 10:23