Tafuta

Caritas Intenationalis: Majilio na hatimaye Noeli ni muda wa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo! Caritas Intenationalis: Majilio na hatimaye Noeli ni muda wa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo! 

Kipindi cha Majilio na Noeli, iwe ni fursa ya kushuhudia upendo!

Kipindi hiki kuelekea maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu, iwe ni fursa ya kutafakari kwa undani: Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka kwa kutumia “miwani ya watu wa nyakati hizi”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Majilio ni kipindi cha kumbukumbu na matumaini kwa Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake, ili kuweza kuinua utu na heshima yao, iliyokuwa imechakaa kutokana na dhambi, ili hatimaye, kuwakomboa kutoka katika dhambi na mauti. Hii ni hija ya maisha ya imani, matumaini na mapendo; inayowakumbusha waamini, Fumbo la Umwilisho na Siku ya ile ya mwisho, Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu; kama Kanisa linavyokiri na kufundisha kwenye Kanuni ya Imani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kila mwaka, Sherehe ya Noeli ni mpya kwa sababu inapyaisha imani, inafungua matumaini na kuwasha moto wa mapendo na kwa namna ya pekee mwaka huu 2018, jicho la huruma na upendo wa Mungu linaelekezwa kwa wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia!

Kardinali Luis Antonio Chito Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anasema kampeni ya “Shiriki Safari” inalenga kujenga umoja na mshikamano kwa kuwaondolea wananchi mahalia hofu, mawazo mgando na maamuzi mbele ambayo yamekuwa ni kikwazo katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Kumbe, kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo na ukarimu unaowakutanisha watu katika medani mbali mbali za maisha. Kipindi hiki kuelekea maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu, iwe ni fursa ya kutafakari kwa undani: Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka kwa kutumia “miwani ya watu wa nyakati hizi”.

Yesu alizaliwa katika pango la kulishia wanyama na baada ya miaka thelathini na tatu, aliteswa na hatimaye, kufa Msalabani, kama mhalifu wa watu wa nyakati zake. Licha ya Kristo Yesu kuzaliwa katika mazingira duni na kufariki dunia katika mateso makali na kifo cha aibu, ameleta mwelekeo mpya wa jinsi ya kuwaangalia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, badala ya kuwapotezea kwa kuwaangalia kama “nyanya mbichi”. Huu ndio mwaliko wa kushiriki safari katika hija ya maisha ya Kristo Yesu, tangu akiwa tumboni mwa Bikira Maria, wakati wa maisha yake ya hadhara, wakati wa Njia ya Msalaba, mateso, kifo na ufufuko wake! Huu ni mwaliko na changamoto kwa kila mwamini kupambana na hali katika maisha yake ya kiroho, hadi kieleweke!

Kardinali Tagle anakaza kusema, Kipindi cha Majilio, kiwe ni fursa ya kuwaonjesha wakimbizi na wahamiaji furaha ya Injili, kwa kuwaonea huruma na mapendo; kwa kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Kama ilivyokuwa kwa Malaika Gabrieli kwa Bikira Maria alipoambiwa “Usiogope”, ni fursa kwa waamini kuonesha moyo wa upendo na ukarimu. Ikumbukwe kwamba, hata Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ilionja adha ya kukimbilia uhamishoni na kufanikiwa kumlinda Mtoto Yesu kutokana na nguvu ya imani, uvumilivu, utu, busara, hekima na ujasiri.

Leo hii, kuna kundi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ambao hawajui mustakabali wa maisha yao, changamoto na  mwaliko kwa waamini kujitaabisha kufahamu historia na matamanio yao halali katika maisha, tayari kuwasaidia na kamwe wasiwe kama Mfalme Herode aliyetumia madaraka na nguvu zake za kijeshi kusambaza hofu na utamaduni wa kifo! Maskini, wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaohitaji kushuhudiwa Injili ya matumaini, huruma na mapendo!

Caritas Internationalis inasema kampeni ya “Shiriki Safari” na wakimbizi na wahamiaji, ni mchakato unaopania kutambua: haki msingi, utu na heshima ya wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia badala ya kuwaangalia kwa “jicho la kengeza”, hofu, mashaka pamoja na kuwa na maamuzi mbele; chuki na uhasama. Kipindi cha Majilio, iwe ni fursa ya kupanua wigo wa ufahamu wa mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji, tayari kuwasaidia kwa hali na mali kama chachu ya mageuzi inayopania kudumisha amani, upendo na ukarimu kwa kuwapatia hifadhi, usalama na kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Caritas Internationalis

 

 

15 December 2018, 16:14