Mkutano wa Kanisa kuhusu nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo: Uwajibikaji, dhamana ya uwajibikaji; ukweli na uwazi. Mkutano wa Kanisa kuhusu nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo: Uwajibikaji, dhamana ya uwajibikaji; ukweli na uwazi. 

Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto: ukweli na uwajibikaji!

Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, mkutano huu utaongozwa na mambo makuu matatu: uwajibikaji, dhamana ya uwajibikaji; ukweli na uwazi. Kamati kuu imetuma barua kwa washiriki wa mkutano huu pamoja na maswali dodoso yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mbinu mkakati wa kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia unapania pia kuliwezesha Kanisa kujitakatifuza kwa kujikita katika maadili na utu wema, changamoto inayovaliwa njuga kwa wakati huu na Baba Mtakatifu Francisko, ambaye ameunda Kamati kuu itakayoratibu mkutano maalum wa Kanisa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia utakaofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019. Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, mkutano huu utaongozwa na mambo makuu matatu: uwajibikaji, dhamana ya uwajibikaji; ukweli na uwazi. Kamati kuu imetuma barua kwa washiriki wa mkutano huu pamoja na maswali dodoso yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu!

Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa familia ya Mungu inayoonesha masikitiko yake kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa anasema, kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho. Waathirika wa kashfa ya nyanyaso za kijinsia wanagusa maisha na utume wa Kanisa kwa kushindwa kuwashughulikia wahusika kikamilifu pamoja na kuwatelekeza watoto wadogo. Huko nyuma, Kanisa kwa kushindwa kutimiza wajibu wake, lilikuwa kama jibu, lakini kwa wakati huu, Kanisa linataka kuonesha mshikamano, katika undani wa maisha na utume wake, ili kujenga historia ya sasa na ile ijayo!

Mama Kanisa anataka kutoa majibu bayana na muafaka kama sehemu ya mchakato wa uponyaji wa waathirika wa nyanyaso za kijinsia pamoja na Kanisa kuendelea kujiaminisha katika dhamana na wajibu wa utekelezaji wa utume wake kwa walimwengu, vinginevyo kuna hatari kubwa! Hatia ya kwanza ni kutambua ukweli kwa yale yote yaliyotendeka. Kutokana na changamoto hii, Kamati kuu ya Maandalizi ya Mkutano maalum wa Kanisa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia inawataka Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kuwatembelea na kuzungumza nao, kabla ya kuhudhuria mkutano huo, ili kutambua shida na mahangaiko ya waathirika wa nyanyaso za kijinsia katika nchi zao!

Katika barua hii, Kamati kuu imeambatanisha pia maswali dodoso wanayopaswa kuyajibu kwa kina, kama njia ya kuwawezesha washiriki kutoa maoni yao, yatakayochangia mchakato mzima wa mkutano huu, ili kutambua mahali ambapo kunahitajika msaada wa dharura, ili kufanya marekebisho kwa sasa na kujiwekea sera na mikakati kwa siku za mbeleni; lakini zaidi ni kuliwezesha Kanisa kufahamu kwa kina na mapana ukubwa wa kashfa hii katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Kamati kuu inapenda kuwashukuru kwa kujibu kikamilifu maswali dodoso, tayari kuanza hija ya pamoja, kielelezo cha umoja na urika wa Maaskofu kama njia ya kujibu changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa.

Kila Askofu anapaswa kutambua changamoto hii, kwa kukutana katika mshikamano unaofumbatwa kwenye fadhila ya unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani, tayari kufanya malipilizi kwa kashfa zilizojitokeza; tayari kutenda katika ukweli na uwazi na kila mtu ndani ya Kanisa akiwajibika barabara. Majibu ya maswali dodoso yanapaswa kuifikia Kamati kuu kabla ya tarehe 15 Januari 2019. Barua hii imeandikwa na Kardinali Blase J. Cupich kwa niaba ya wanakamati wenzake, walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni.

Kamati hii inaundwa na Kardinali Blase J. Cupich na Kardinali Oswald Gracias; wengine ni Askofu mkuu Charles Jude Scicluna, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa pamoja na Padre Hans Zollner, Rais wa Kituo cha Kulinda Watoto Wadogo, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian kilichoko mjini Roma. Kamati kuu itawashirikisha wakuu wa Makanisa ya Mashariki pamoja na viongozi wakuu kutoka katika Sekretarieti kuu ya Vatican, chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko. Itakumbukwa kwamba, huu ni mkutano utakaohudhuriwa na Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia pamoja na wawakilishi wa wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume.

Barua ulinzi watoto
19 December 2018, 10:17