Tafuta

Vatican News
Vatican imeanzisha Kituo cha Kuangalia Mwenendo wa Familia Kimataifa. Vatican imeanzisha Kituo cha Kuangalia Mwenendo wa Familia Kimataifa. 

Kituo cha Kuangalia Mwenendo wa Familia Kimataifa: Umaskini!

Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha anasema katika kipindi cha miaka mitatu, “Kituo cha Kuangalia Mwenendo wa Familia Kimataifa” kitajikita hasa katika kupembua hali ya umaskini wa familia; mahusiano ya kifamilia pamoja na hali ya uchumi kifamilia. Huu ni utafiti utakaofanywa kwa kushirikiana na Vyuo Vikuu vya Kikatoliki na taasisi nyingine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anaendelea  kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Kanisa linatambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbali mbali za Kikristo, kiutu na kijamii!

Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Injili ya Kristo Yesu ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha anasema katika kipindi cha miaka mitatu, “Kituo cha Kuangalia Mwenendo wa Familia Kimataifa” kitajikita hasa katika kupembua hali ya umaskini wa familia; mahusiano ya kifamilia pamoja na hali ya uchumi kifamilia. Huu ni utafiti utakaofanywa kwa kushirikiana na Vyuo Vikuu vya Kikatoliki pamoja na taasisi za elimu ya juu kutoka nchini Italia, Hispania, Finland, Slovacchia, Jamhuri ya Watu wa Czech, Marekani, Mexico, Argentina, Cile, Hong Kong, Benin na Kenya kwa upande wa Bara la Afrika.

Askofu mkuu Paglia ameyasema, haya Alhamisi, tarehe 6 Desemba 2018 wakati akiwasilisha mpango kazi wa “Kituo cha Kuangalia Mwenendo wa Familia Kimataifa” kwa kukazia kwamba, Injili ya familia na umaskini ni kati ya vipaumbele vya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa! Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ameendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa Injili ya familia na ndoa mintarafu Mafundisho ya Kanisa.

Baba Mtakatifu ameendesha Katekesi ya kina kuhusu familia sanjari na kuitisha maadhimisho ya Sinodi mbili kwa ajili ya Maaskofu na matunda ya kazi hii ni Wosia wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko ni “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Injili ndani ya familia”. Baba Mtakatifu anawataka wanandoa wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia; tayari kutangaza na kushuhudia: ukuu, wema na utakatifu wa Sakramenti ya Ndoa katika maisha ya kifamilia sanjari na kusimama kidete kupambana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo!

Askofu mkuu Paglia anasema, “Kituo cha Kuangalia Mwenendo wa Familia Kimataifa” kitakuwa kinachapisha tafiti zake katika lugha kuu tatu: Kiingereza, Kihispania na Kiitalia katika anuani ifuatayo: www.familymonitor.net. Kituo hiki kinalenga kutoa huduma ya pekee kwa Injili ya familia, ili kukuza na kudumisha ule upendo wa dhati kati ya bwana na bibi, pamoja na kuendelea kuangalia athari za umaskini katika maisha ya ndoa na familia. Kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, hata leo hii, Mama Kanisa anataka kutoa kipaumbele cha pekee katika kukuza na kudumisha Injili ya familia na ndoa.

Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kutoka katika nchi kumi na tano kwa sasa zimejiunga na Kituo hiki, ili kukusanya takwimu kutoka katika nchi husika. Kuna vyuo na taasisi kadhaa zimeonesha nia ya kutaka kujiunga na kituo hiki. Taasisi zinazoshughulikia maisha ya ndoa na familia kama vile Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha pamoja na Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis yameonesha nia ya kujiunga.

Lengo ni kwa ajili ya kutoa huduma endelevu na fungamani kwa ajili ya Injili ya familia. Habari mbali mbali mbali kuhusiana na Injili ya familia zitaweza kutolewa na Kituo hiki cha Kimataifa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Hii ni kazi kubwa ya kukusanya habari na takwimu kuhusu hali ya maisha ya familia! Huu ni muhtasari wa wimbo ulio bora unaoonesha nguvu ya upendo katika maisha ya binadamu na udhaifu wake! Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu, Mwana wa Mungu amejitwalia hali ya ubinadamu, akaupenda na kuukomboa.

Kwa upande wake, Professa José Luis Mendoza Pérez,  Muasisi Rais wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mtakatifu Antonio, UCAM, kutoka Hispania anasema, hiki Chuo Kikuu kitatumika kama daraja la kuwaunganisha wadau mbali mbali; kwa kutumia rasilimali watu na fedha sanjari na kushirikiana na vitivo mbali mbali vya sayansi ya binadamu ili kufanikisha azma ya kutangaza na kushuhudia Injili ya familia na ndoa. UCAM itashiriki pia kutafsiri habari na takwimu ili ziweze kuwafikia wadau wengi zaidi.

Naye Dr. Francesco Belletti, Mkurugenizi wa Kituo cha Familia Kimataifa cha Milano, CISF anasema, hii ni fursa kukusanya, kusoma na kutafsiri takwimu, ili kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinazofumbatwa katika takwimu hizi mintarafu mwelekeo mzima wa Injili ya familia kimataifa. Tafiti katika kipindi cha miaka mitatu ya mwanzo, zitakusanywa na kuchapishwa na muhtasari wake kutolewa mwezi Mei, 2020. Itakumbukwa kwamba, umaskini wa familia ni kati ya changamoto zinazovaliwa njuga na “Kituo cha Kuangalia Mwenendo wa Familia Kimataifa”.

Dr. Francesco Belletti, anakaza kusema, hapa watafiti wataangalia jinsi ambavyo umaskini unavyopekenyua tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na jinsi ambavyo wanaweza kusaidiwa ili kupambana na hali zao, huku wakiwa wanafumbata tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Mambo makuu matatu yatapewa msukumo wa pekee katika tafiti zao: wanawake, watoto na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, hususan matumizi ya mitandao ya kijamii. Katika ulimwengu mamboleo, familia zinakumbana na changamoto pevu kiasi kwamba, zimegeuzwa kuwa kama “mpira wa kona” unaogambaniwa na wadau mbali mbali, lakini kila mdau akiwa na lengo lake mahususi.

Sera za kisiasa na kiuchumi si rafiki sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya familia nyingi duniani. Kuna baadhi ya wanasiasa wanaona ongezeko la watoto kwenye familia kuwa ni tishio la uhuru wa watu wa ndoa. Pengine, umefika wakati wa kutoa tuzo kwa wanafamilia wanaobaki waaminifu na wadumifu kama mashuhuda wa Injili ya familia na ndoa, mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya!

Askofu Mkuu Paglia: Familia

 

29 December 2018, 12:01