Cerca

Vatican News
Papa Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume nchini Bulgaria na Yugoslavia ya zamani kuanzia tarehe 5-7 Mei 2019 Papa Francisko anatarajia kufanya hija ya kitume nchini Bulgaria na Yugoslavia ya zamani kuanzia tarehe 5-7 Mei 2019 

Hija ya Kitume: Papa kutembelea Bulgaria & Yugoslavia ya zamani

Papa Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume katika nchi hizi mbili kuanzia tarehe 5-7 Mei 2019. Katika hija hii ya kitume, Baba Mtakatifu atatembelea mji wa Sofia na Rakovski; na akiwa nchini Yugoslavia ya zamani, atatembelea mji wa Skopje, mahali alikozaliwa Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta, shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa viongozi wa Serikali na Kanisa nchini Bulgaria pamoja na Yugoslavia ya zamani na hivyo anatarajiwa kufanya hija ya kitume katika nchi hizi mbili kuanzia tarehe 5-7 Mei 2019. Katika hija hii ya kitume, Baba Mtakatifu atatembelea mji wa Sofia na Rakovski; na akiwa nchini Yugoslavia ya zamani, atatembelea mji wa Skopje, mahali alikozaliwa Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta, shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini! Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Bulgaria inaongozwa na kauli mbiu “Pacem in terris”, yaani “Amani duniani”, mwangwi wa Waraka wa Kitume wa Mtakatifu Yohane XXIII “Pacem in terris” anayekazia umuhimu wa haki, uhuru, ukweli, upendo na msamaha kama mambo msingi ya kujenga na kudumisha amani duniani sanjari na kukuza mahusiano mema kati ya wananchi na viongozi wao, Jumuiya za kisiasa na ulimwengu katika ujumla wake.

Baraza la Maaskofu Katoliki Bulgaria katika nembo ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao, linakazia kwa namna ya pekee kabisa, umuhimu wa amani duniani! Maaskofu wanawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Bulgaria kuanza kujiandaa kiroho kwa ajili ya kumpokea Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni matumaini ya Maaskofu kwamba, hija hii ya kitume, itakuwa ni chachu ya ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano katika eneo hili, ambalo bado lina madonda ya vita na mipasuko ya kijamii. Baraza la Maaskofu Katoliki Bulgaria linakaza kusema, Injili ya amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayomwajibisha binadamu. Amani inawezekana kuwa ni matunda ya kazi ya mikono ya wanadamu; juhudi na sala za pamoja! Lakini, pia walimwengu wasipokuwa makini, wanaweza kuitema zawadi ya amani na matokeo yake vita na ghasia vikatawala duniani.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Yugoslavia ya zamani, linamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kukubali na kuitikia mwaliko wa kuwatembelea, ili kuwabariki na kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu nchini humo inaongozwa na kauli mbiu “Msiogope enyi kundi dogo” Lk. 12:32. Familia ya Mungu nchini Yugoslavia ya zamani, imepokea kwa ari na moyo mkuu taarifa za hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao anasema, Askofu Kiro Stoyanov. Fursa ya Baba Mtakatifu Francisko, hapo tarehe 7 Mei 2019 kutembelea mji wa Skopje, mahali alikozaliwa Mama Theresa wa Calcutta ni changamoto na mwaliko kwa familia ya Mungu nchini humo kupyaisha maisha ya kiroho na kijamii, ili kila mwananchi aweze kujikita katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; ili wananchi wa Yugoslavia ya zamani waweze kutembea katika mwanga angavu.

Papa: Bulgaria

 

 

 

15 December 2018, 15:51