Tafuta

General view of Wujek Coal Mine is seen during sunset in Katowice General view of Wujek Coal Mine is seen during sunset in Katowice 

COP24 Katowice: Vatican inakazia: Maadili, Utu na Mahitaji msingi ya binadamu!

Vatican inapenda kukazia mambo makuu yafuatayo kama sehemu ya Utekelezaji wa Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21: Kanuni maadili; Pili: Utu wa mwanadamu, mapambano dhidi ya umaskini; sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu na: Tatu ni kuweka mipango thabiti itakayokidhi mahitaji msingi ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 

Mkutano 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP24 ni sehemu ya mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuandaa Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21 uliotiwa sahihi kunako mwaka 2015. Mkutano huu unalenga kutoa: mwongozo, sheria, kanuni na utekelezaji wake, dhamana ambayo ni nyeti sana kwa wakati huu, licha ya madhara makubwa yanayoendelea kusababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 3 Desemba 2018, kwenye Mkutano wa 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP24 unaoendelea huko nchini Poland hadi tarehe 14 Desemba 2018.  Bado inawezekana kabisa kwa Jumuiya ya Kimataifa kupunguza kiwango cha nyuzi joto kadiri ya Makubaliano ya Paris, lakini pia kunahitajika sera makini zitakazo songesha mbele mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani kwa kuzingatia teknolojia rafiki kwa mazingira. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuwa na utashi wa kisiasa.

Kardinali Parolin anakaza kusema, Vatican inapenda kukazia mambo makuu yafuatayo kama sehemu ya Utekelezaji wa Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21: Kwanza kabisa ni kanuni maadili; Pili: Utu wa mwanadamu, mapambano dhidi ya umaskini; sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu na: Tatu ni kuweka mipango thabiti itakayokidhi mahitaji msingi ya binadamu kwa sasa na kwa siku za mbeleni!

Vatican inazihamasisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuanzisha mchakato wa elimu makini utakaosaidia kuwawajibisha watu katika ulaji, kwa kupambana na rushwa na ufisadi; kwa kuwa na sera za uchumi shirikishi katika kuchagua, kupanga na kutekeleza mikakati hiyo kwa kuzingatia mahitaji msingi ya binadamu. Yote haya yafanyike katika misingi ya ukweli na uwazi! Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na utengenezaji wa fursa za ajira, kwa kuhakikisha kwamba, watu wanafanya kazi katika mazingira bora zaidi; kwa kuzingatia haki msingi za binadamu, hifadhi za kijamii na mapambano dhidi ya umaskini duniani pamoja na kuendelea kujikita katika malezi bora, elimu na mshikamano!

Kardinali Parolin anasema, kanuni maadili, usawa na haki jamii ni mambo msingi katika mchakato wa mabadiliko ya mitindo ya maisha, ulaji na elimu! Athari za mabadiliko ya tabianchi ni matokeo ya jamii kusigina kanuni maadili na utu wema! Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika kanuni maadili zitakazo saidia kuleta mabadiliko ya mitindo ya maisha! Baba Mtakatifu Francisko anasema, ufumbuzi wa athari za mabadiliko ya tabianchi unajikita katika mapambano dhidi ya umaskini; ushirikishwaji wa jamii pamoja na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Mabadiliko ya kifikra, kwa kuzingatia kanuni maadili na mwelekeo wa kibinadamu ni mambo muhimu katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni jambo linalopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa.

Licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kwenye karne ya ishirini na moja, lakini pia ni karne inayokumbukwa kwa uchafuzi mkubwa wa mazingira. Utashi wa kimaadili na kisiasa ni nyenzo kuu ya kuokoa mazingira, nyumba ya wote. Majadiliano katika mfumo wa uzalishaji; mshikamano na ugunduzi ni mambo muhimu katika ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi, mambo yanayohitaji umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa!

Parolin COP24
04 December 2018, 09:40