Mkutano wa Kimataiga kuhusu biashara haramu ya binadamu na uhalifu wa kupangwa Barani Afrika. Mkutano wa Kimataiga kuhusu biashara haramu ya binadamu na uhalifu wa kupangwa Barani Afrika. 

Mkutano wa Kimataifa kuhusu Biashara ya Binadamu na Uhalifu wa kupangwa Afrika!

Taasisi ya Kipapa ya Sayansi kuanzia tarehe 12-13 Desemba 2018 taasisi yake inafanya mkutano wa kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu “Wanawake wa Afrika. Majaji na Waendesha Mashitaka Dhidi ya Biashara ya Binadamu na Uhalifu wa kupangwa”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Biashara ya silaha, biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na biashara ya binadamu na viungo vyake ni kati ya vyanzo vikuu vya fedha chafu duniani; fedha ambayo inanuka damu ya watu wasiokuwa na hatia! Baba Mtakatifu Francisko anasema biashara haramu ya binadamu na viungo vyake, pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo inayofanywa na magenge ya uhalifu kitaifa na kimataifa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu!

Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu kutokana na: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kidini na kikabila; Umaskini wa hali na kipato, yote haya ni mambo yanayonyanyasa na kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Makundi ya kigaidi na magenge ya uhalifu wa kimataifa yanatumia njia za wakimbizi na wahamiaji kujipatia fedha haramu.

Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuunganisha nguvu zao ili kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; kwa kuwalinda na kuwasaidia kwa dhati waathirika; pamoja na kuendelea kukazia toba na wongofu wa ndani, unaoheshimu na kuthamini utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika usimamizi na utekelezaji wa utawala wa sheria pamoja na kuendelea kuelimisha watu kuchukua tahadhari dhidi ya biashara haramu ya binadamu!

Kutokana na changamoto zote hizi, Askofu Marcelo Sànchez Sorondo, Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi, anasema kuanzia tarehe 12-13 Desemba 2018 taasisi yake inafanya mkutano wa kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu “Wanawake wa Afrika. Majaji na Waendesha Mashitaka Dhidi ya Biashara ya Binadamu na Uhalifu wa kupangwa”. Moyo wa mshikamano na upendo katika kupambana na matatizo na changamoto za maisha ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda wa Injili ya matumaini inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu, na kwa njia hii, wakristo wanaweza kutambulikana kuwa kweli ni wafuasi wa Yesu. Mkutano huu ni mwendelezo wa mkutano kama huu uliofanyika kunako mwezi Juni, 2016. Wakati huo Baba Mtakatifu Francisko aliwataka Majaji kukumbatia haki; viongozi wa Kanisa kujikita katika kanuni maadili na utu wema na wanasiasa kusimamia utawala wa sheria na uongozi bora. Majaji wanapaswa kutekeleza dhamana na utume wao bila ya kuingiliwa na serikali au taasisi binafsi, ili haki iweze kutendeka

Bara la Afrika linaongoza kwa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo inapaswa kufyekelewa mbali kwani huu ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Matukio yote haya yanaacha madonda ya kudumu katika akili na nyoyo za watu. Inasikitisha kuona kwamba, binadamu analinganishwa na bidhaa inayoweza kuuzwa au kununulia sokoni.

Hivi ni vitendo vinavyonyofoa utambulisho wa mtu na usaliti wa upendo kwa wasichana na wanawake. Ukahaba ni donda ndugu, linaloendelea kuchafua utu na heshima ya wanawake na wasichana wengi Barani Afrika. Inakadiriwa kwamba, kuna wasichana na wanawake zaidi ya  milioni hamsini wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na utumwa mamboleo kila mwaka. Takwimu hizi zinatishia usalama wa maisha, ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu Barani Afrika. Kati ya wawezeshaji katika mkutano huu wa kimataifa ni pamoja na Anipha Abass Mwingira; Sophia Adelaide N. Wambura na Jacqueline Rugemalila kutoka Tanzania.

Majaji: Biashara Binadamu
12 December 2018, 09:47