Tafuta

Papa Francisko: Sifa kuu za Askofu ni unyenyekevu unaofumbatwa katika huduma ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Papa Francisko: Sifa kuu za Askofu ni unyenyekevu unaofumbatwa katika huduma ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu 

Kardinali Parolin: Sifa kuu za Askofu!

Askofu anafundisha, anatangaza na kushuhudia kwa mamlaka yote Habari Njema ya Wokovu; anayo dhamana ya kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa njia ya maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na mafumbo matakatifu yanayowakirimia waamini chachu ya utakatifu pamoja na kuwaongoza watu wa Mungu kwa mfano wa Kristo Mchungaji mwema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwa ufupi sifa kuu za Askofu kuwa ni: unyenyekevu na huduma; mambo yanayofafanuliwa vyema na Mtakatifu Paulo, Mtume katika Waraka wake kwa Tito, akionesha mambo msingi yanayopaswa kufuatwa na kutekelezwa na Maaskofu, ili kukamilisha yale yanayopungua katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kuwachagua na kuwasimika wazee wanaofaa kwa ajili ya uongozi wa Kanisa; watu wema na wenye kiasi, wapenda haki na watakatifu; watu wenye mifano bora ya kuigwa na jamii inayowazunguka.

Askofu anayo dhamana ya kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wote, kwa kutambua kwamba, kimsingi yeye ni mtu wa Mungu, aliyeteuliwa kati ya watu kwa ajili ya huduma, ili kuhakikisha kwamba, anakuza na kudumisha Ibada na Uchaji wa Mungu, mambo msingi katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Utume huu, umwezeshe Askofu kuwa kiongozi mkarimu, akitambua kwamba, Kristo Yesu ndiye anayewaita waja wake na kuwaweka wakfu ili kuendeleza kazi ya ukombozi!

Hivi karibuni, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, alimweka wakfu Monsinyo Marco Mellino aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu mwambata wa Baraza la Makardinali washauri, maarufu kama C9! Ibada hii imehudhuriwa pia na Askofu Marcello Semeraro Katibu mkuu wa Baraza la Makardinali washauri pamoja na Askofu Marco Brunetti wa Jimbo Katoliki Alba walioshiriki kumweka wakfu. Kulikuwepo na Maaskofu zaidi ya thelathini kutoka ndani na nje ya Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Askofu Marco Mellino, amempongeza kwa juhudi, bidii, weledi na uaminifu katika utekelezaji wa utume na majukumu yake. Anasema, ni kiongozi anayetekeleza dhamana na wajibu wake kwa upendo mkuu, kwa amani na utulivu wa ndani; kwa ukarimu pamoja na kuwashirikisha wengine. Baba Mtakatifu anamtakia heri na baraka katika utume wake mpya kama Katibu mwambata wa Baraza la Makardinali wanaomsaidia Baba Mtakatifu kuongoza Kanisa kwa ukaribu zaidi.

Kardinali Pietro Parolin katika mahubiri yake amesema, Askofu kuwekwa wakfu ni kielelezo kwamba, huyu ni kiongozi aliyeteuliwa na kuwa anapendwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya huduma kwa waja wake, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Mwanzo. Maaskofu pamoja na waandamizi wao wanaendeleza utume ambao Kristo Yesu ameliachia Kanisa lake kwa njia ya Mitume. Kumbe, Askofu anafundisha, anatangaza na kushuhudia kwa mamlaka yote Habari Njema ya Wokovu; anayo dhamana ya kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa njia ya maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na mafumbo matakatifu yanayowakirimia waamini chachu ya utakatifu.

Kardinali Parolin anakaza kusema, Askofu ni kiongozi mkuu wa familia ya Mungu, dhamana anayopaswa kuitekeleza kwa njia ya ushuhuda wa maisha unaofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu, utii, upendo na ujasiri wa kufanya hata maamuzi magumu kwa ajili ya kusaidia kukuza na kukomaza jumuiya ya waamini, bila kusahau kwamba, anapaswa pia kuchunga Kondoo wa Kristo ili wasikwapuliwe ni Mbwa mwitu wakali; daima anahimizwa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini pamoja na mchungaji wao mkuu.

Ili Askofu aweze kutekeleza vyema dhamana na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, hana budi kujenga na kudumisha mahusiano ya karibu sana na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, tafakari ya kina ya Fumbo la Msalaba na Neno la Mungu linalopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha; kwa kuongozwa na hekima na busara katika maamuzi na utekelezaji wake. Kwa kuwa na mawasiliano mazuri na Kristo Yesu, Askofu ataweza kujenga na kudumisha uhusiano mwema na wasaidizi wake wa karibu ambao kimsingi ni wakleri wanaopaswa kutambua uwepo wake wa kibaba!

Kardinali Parolin anamtaka Askofu Marco Mellino kumuiga Kristo mchungaji mwema, kwa kuwa mwaminifu, kiongozi mwema, mpole na mkarimu; kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake. Haya yanaweza kuonekana kuwa ni madai makubwa kwa Askofu Mellino, lakini huu ndio ukweli wa mambo. Anapaswa kumwangalia, kumfuasa na kumuiga Kristo Yesu hatua kwa hatua katika maisha na utume wake. Ole wao anasema Kardinali Parolin, Maaskofu wanaotaka kumweka Kristo Yesu, pembeni mwa vipaumbele vyao; kwa kushindwa kutubu na kuongoka, ili kuambata utakatifu wa maisha. Ole wao Maaskofu wanapambana na mahangaiko ya kila siku na kumsahau Kristo Yesu, watambue kwamba, huko wanakoelekea ni kubaya sana! Kimsingi, huu ndio muhtasari wa maisha na utume wa Askofu ndani ya Kanisa. Motto ya Askofu Marco Mellino ni “Mihi vivere Christus” yaani “Mimi kwangu kuishi ni Kristo”.

Kimsingi, wakleri wanatambua kwamba, wito ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si kwa ajili ya masitahili yao binafsi, kumbe, wanapaswa kuwa ni watu wa shukrani, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, chemchemi ya amana za maisha ya kiroho! Maaskofu wanapaswa kuwa ni wachamungu, watu wa sala na wachungaji wema. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linahitaji viongozi wakweli na waadilifu; watu wanaoweza kujitosa kimasomaso kwa ajili ya: kuongoza, kutakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu waliokabidhiwa kwao. Kanisa halihitaji mameneja, bali Askofu ambaye ni shahidi wa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo; mtu mnyenyekevu na jasiri; Kanisa halihitaji wapambanaji, bali viongozi wanyenyekevu watakaopandikiza mbegu ya haki, ukweli na amani.

Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alimteuwa Askofu Marco Mellino kuwa Katibu mkuu mwambata wa Baraza la Makardinali washauri. Alizaliwa tarehe 3 Agosti 1966 huko Alba, nchini Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, mwaka 1991 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 27 Oktoba 2018, akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu mwambata wa Baraza la Makardinali Washauri na hatimaye, kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 15 Desemba 2018, na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican.

Sifa Kuu za Askofu

 

20 December 2018, 11:13