Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mh. Padre Filbert Felician Mhasi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Tunduru-Masasi, Tanzania. Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mh. Padre Filbert Felician Mhasi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Tunduru-Masasi, Tanzania. 

Padre Filbert Felician Mhasi, ateuliwa kuwa Askofu wa Tunduru-Masasi, nchini Tanzania

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Filbert Felician Mhasi wa Jimbo Katoliki Mahenge, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi, lililoko Kusini mwa Tanzania. Hadi uteuzi huo Askofu mteule Padre Filbert Felician Mhasi alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Kanisa Kuu la Kwiro, Jimbo Katoliki Mahenge.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Msimamizi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 8 Desemba 2018, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Filbert Felician Mhasi wa Jimbo Katoliki Mahenge, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi, lililoko Kusini mwa Tanzania.  Hadi  uteuzi huo Askofu mteule Padre Filbert Felician Mhasi alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Kanisa Kuu la Kwiro, Jimbo Katoliki Mahenge.

Askofu mteule Filbert Felician Mhasi alizaliwa tarehe 30 Novemba 1970 huko Biro Jimboni Mahenge. Alipata elimu yake ya sekondari  katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Francis, Kasita huko Ifakara kati ya mwaka 1986-1992. Baadaye alitumwa kwenda katika Seminari kuu ya Mama wa Malaika, Kibosho Jimbo Katoliki la Moshi kwa ajili ya malezi na masomo ya Falsafa kati ya mwaka 1993-1995.  Baadaye kati ya mwaka 1995-1998 alipata mafunzo ya Kitaalimungu katika Seminari kuu ya Mtakatifu Paulo Kipalapala Jimbo kuu la Tabora. Alipata Daraja takatifu ya Upadre tarehe 3 Julai 2001 Jimboni Mahenge.

Baada ya kupadrishwa, alitumwa kwa masomo katika Chuo cha Kikatoliki Mwenge, Jimbo Katoliki la Moshi kwa masomo ya mnamo mwaka 2001-2003, ambako alitunukiwa shahada ya Elimu. Kati ya mwaka 2003-2004 alikuwa Kaimu Gombera, Mhasibu na mlezi katika Seminari ndogo ya Francis, Kasita Ifakara.  Kati ya mwaka 2005-2009 alitumwa katika Chuo kikuu cha Duquesne huko Pittsburgh, Pennsylvania Marekani ambako alitunikiwa shahada ya Uzamili katika Falsafa. Na mwaka 2009-2014 alikuwa Gombera wa Seminari ndogo ya Mtakatifu Francis, Kasita, Ifakara. Na tangu mwaka 2014 amekuwa Paroko wa Kanisa kuu Kwiro Ifakara na Dekano. Tangu mwaka 2015 Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Yosefu na Mwenyekiti wa Umoja wa Mapadre Wazalendo (UMAWATA) Jimboni Mahenge.

08 December 2018, 11:48