Tafuta

Vatican News
Kardinali Angelo Sodano: Mageuzi ya kweli yanafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani! Kardinali Angelo Sodano: Mageuzi ya kweli yanafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani!  (Vatican Media )

Mageuzi ya kweli yanafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani!

Kardinali Sodano amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa ushuhuda wa maisha; huduma ya ukarimu na upendo kwa ajili ya Kanisa la Kristo. Katika kipindi cha Mwaka 2018, Baba Mtakatifu amekuwa na mambo mengi ya kutekeleza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ndani na nje ya Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema ndio wimbo unaosikika sehemu mbali mbali za dunia, Wakristo wanapokusanyika kwa ajili ya kusherehekea Noeli, ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Noeli ni kipindi cha mshikamano wa upendo kati ya majirani. Jumuiya ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, yaani Sekretarieti kuu ya Vatican, Ijumaa, tarehe 21 Desemba 2018 imeungana na Baba Mtakatifu Francisko ili kutakiana heri na baraka kwa kipindi cha Noeli na Mwaka mpya 2019.

Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali kwa niaba ya viongozi na wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican, amemtakia heri, baraka na afya njema, Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Sherehe ya Noeli. Salam na matashi haya ni kielelezo cha umoja, upendo na mshikamano wa Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro! Kardinali Sodano amewasilisha pia salam na matashi mema kutoka kwa Mabalozi wa Vatican wanaotekeleza dhamana na utume wao, sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Sodano amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa ushuhuda wa maisha; huduma ya ukarimu na upendo kwa ajili ya Kanisa la Kristo. Katika kipindi cha Mwaka 2018, Baba Mtakatifu amekuwa na mambo mengi ya kutekeleza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ndani na nje ya Vatican. Kanisa linamshukuru Baba Mtakatifu kwa Waraka wake wa kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”. Katika Waraka huu Baba Mtakatifu anakazia upendo wa dhati kama njia inayoweza kuwapeleka waamini katika utakatifu! Waamini wanapaswa pia kusikiliza, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao; wajitahidi kushiriki mara kwa mara Sakramenti za Kanisa; kwa kujitia uthabiti katika kusali, kujinyima pamoja na kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa wahitaji zaidi.

Baba Mtakatifu katika Waraka huu, anakazia utakatifu wa maisha kama chachu ya mabadiliko na mageuzi katika maisha na utume wa Kanisa! Wafanyakazi wa Sekretarieti kuu wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo endelevu wa Mungu katika maisha na utume wao na kwamba, utakatifu ndiyo sura pendelevu inayoweza kutolewa na Mama Kanisa kwa walimwengu mamboleo. Kardinali Sodano amekumbushia kuhusu Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa mwaka 2018; kutangazwa kwa Papa Paulo VI kuwa Mtakatifu! Katika kipindi cha mwaka mzima wa 2018 Sekretarieti kuu ya Vatican imeendelea kufanya kazi bega kwa bega na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa ajili ya ustawi, maendeleo, mafao na ushirikiano kati ya watu wa Mataifa. Mwishoni, Kardinali Angelo Sodano kwa niaba ya Sekretarieti kuu ya Vatican, amemtakia Baba Mtakatifu Francisko heri na baraka kwa Mwaka mpya wa 2019.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa Sekretarieti kuu ya Vatican, amekazia umuhimu wa Kanisa kutembea katika mwanga wa Kristo na kwamba, kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni jambo lisilokubalika hata kidogo katika maisha na utume wa Kanisa. Ukosefu wa uaminifu na ubadhirifu wa maisha ya kiroho ni “ndago” inayopandikiza kinzani, migawanyiko na mipasuko katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu amegusia shida, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia; Mauaji, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Amewapongeza wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kwa kazi nzuri wanayoendelea kuitekeleza. Baba Mtakatifu pia ameishukuru Sekretarieti kuu kwa utekelezaji wa majukumu mbali mbali katika misingi ya: weledi, ukweli na uwazi na kwamba watakatifu na wafiadini wanaendelea kulipamba Kanisa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Noeli ni muda muafaka wa kutembea katika mwanga wa wema ili kushinda ubaya; mwanga wa upendo ili kufukuzia mbali chuki na uhasama, ili hatimaye, kumpokea Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa. Noeli ni Sherehe ya Mungu aliyejinyenyekesha na kuwa mdogo, ili kuwaonjesha wanadamu: wema na huruma yake. Huu ni uhakika kwamba, mwanga wa Mungu utaendelea kung’ara katika maisha ya waja wake licha ya udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu! Udhaifu wa binadamu iwe ni fursa ya toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia na kuambata neema ya utakaso, ili kupyaisha maisha; kwa wale walioanguka dhambini, iwe ni fursa ya kujitakatifuza, ili kupata ushindi dhidi ya dhambi!

Kardinali Sodano

 

22 December 2018, 13:54