Changamoto ya kutangaza na kushuhudia: Uzuri na utakatifu wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo! Changamoto ya kutangaza na kushuhudia: Uzuri na utakatifu wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo! 

Changamoto ya kutangaza uzuri na utakatifu wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo!

Mashambulizi mbali mbali yanayoelekezwa kwa Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa wakati huu, yanaweza kujibiwa kwa njia ya ushuhuda unaosimikwa katika upendo kwa Mungu na jirani; kwa kushuhudia ukweli katika uhuru; kwa kulipenda na kulithamini Kanisa, kwani anasema Padre Marko Rupnik, upendo una nguvu sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa kwanza kabisa linaweza kufahamika kama Jumuiya ya waamini inayofumbatwa katika imani kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kanisa ni taasisi na familia ya Mungu iliyoundwa na Kristo Yesu, inayoendelezwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu na kwamba, hii pia ni nyumba ya watakatifu na wadhambi wanaoalikwa kutubu na kuongoka, kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu.

Utakatifu wa Kanisa unabubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Maandiko Matakatifu na Maisha ya Kisakramenti ambayo ni mwaliko kwa kila mwamini kuchuchumilia fadhila hii katika maisha yake na hivyo kumwilishwa katika Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani! Huu ndio ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaotangaza na kushuhudia uzuri na utakatifu wa maisha katika nyakati hizi ambazo Kanisa linakabiliwa na changamoto mbali mbali kutoka ndani na nje ya maisha na utume wake!

Mkate ni mazao ya nchi na divai ni tunda la mzabibu na kazi ya mikono ya wanadamu, katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Kanisa linamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kulijalia mapaji haya kuwa ni chakula na kinywaji cha maisha ya kiroho! Kumbe, Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha upendo wa Kristo kwa wafuasi wake, hata wale waliothubutu kumsaliti. Maisha yake ni majitoleo kwa maondoleo ya dhambi. Damu yake ni alama ya maisha na Agano Jipya na la milele, ni nguvu inayovunjilia mbali dhambi na mauti.

Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha maisha ya watu waliokombolewa kutoka utumwani na kuwekwa huru; alama ya tumaini na baraka kwa siku za usoni, wakiwa katika hija ya maisha kuelekea Yerusalemu ya mbinguni! Ufunuo wa Yohane kwa watu wote unalenga Makanisa yote kwa kukazia uhusiano wa waamini na Mwenyezi Mungu na umuhimu wa kujikita katika maisha adili na matakatifu, ili Mwenyezi Mungu aweze kuabudiwa na watu kumsadiki Kristo kuwa ni Mwana wa Mungu kwa njia ya ushuhuda unaomwilishwa katika matendo!

Hii ni tafakari iliyotolewa na Padre Marko Rupnik, SJ., Alhamisi, tarehe 22 Novemba 2018 kwa wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Mama Mtakatifu na Watoto wake wadhambi”: Jinsi ya kutangaza uzuri wa Kanisa katika wakati huu mgumu”. Ufunuo wa Yohane ni Kitabu kinachojikita katika imani kwa Kristo Yesu, wataalam wengi wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu wanasema, kitabu hiki kiliandikwa wakati wa hali tete na madhulumu kwa Kanisa, hali ambayo ilikuwa ni kwazo kwa Wakristo walioshindwa kupata maana hali ya madhulumu haya walipokuwa wanatafakari maneno “Jipeni moyo mimi nimeshinda ulimwengu”. Katika taabu na majaribu kama haya, Manabii walitabiri kwamba, siku ya wokovu iko karibu. Mwenyezi Mungu atafika mwenyewe kukomboa taifa lake, litapewa uhuru na kuwatala maadui zake! Hii ndiyo Siku ya Bwana! Ufunuo wa Yohane unatumika kuelezea historia ya Kanisa, taifa jipya na teule; taifa linalodhulumiwa na watu wake kuuwawa kikatili kwa sababu ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake!

Ufunuo wa Yohane ni Kitabu cha Wakristo wa nyakati zote kilichoandikwa na Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili aweze kuliimarisha tena Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa. Ufunuo unaonesha Fumbo la Umwilisho na hadhi ya Wakristo kama watoto wapendwa wa Mungu! Jicho la imani, liwawezeshe waamini kutafakari na kuuona ukuu, wema, huruma na utakatifu wa Mungu katika maisha yao na kwamba, huruma na upendo wa Mungu unajionesha kwa njia ya Fumbo la Pasaka! Hii ndiyo nguvu na jeuri inayoliwezesha Kanisa kusonga mbele, likiwa limeshikamana katika imani na umoja, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni kichwa cha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa.

Kanisa ni chombo cha mawasiliano; kinachopaswa kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya waamini na Mwenyezi Mungu; kwa kuheshimu na kuthamini uwepo wa Mungu kati pamoja nao! Ushuhuda wa upendo kwa Mungu na jirani ni kielelezo cha ufuasi wa Kristo wenye mvuto na mashiko. Kwa njia ya Ubatizo, waamini wanaifia dhambi na kuuvua utu wao wa kale na hivyo kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka; umoja na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Injili ya Kristo ndiyo chachu ya mabadiliko makubwa katika maisha ya waamini wanaochangamotishwa, kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, kama kielelezo cha ushuhuda amini unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani, ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Huu ndio mwaliko ulioletwa tena na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kulitaka Kanisa kuwa ni mhudumu na sauti ya wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Kamwe Kanisa “lisibinafsishwe na kuwekwa mfukoni na Serikali” bali liwe huru kufumbata na kuambata Hekima ya Fumbo la Msalaba: Utu, heshima na haki msingi za binadamu. Lengo ni kushuhudia uwepo wa Kristo Mfufuka kati ya watu wake, kielelezo makini cha Pentekoste mpya. Kanisa liendelee kujiweka chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, nguzo kuu ya Pasaka ya Bwana. Kanisa lisimamie na kumwilisha Kanuni ya Imani, kwa kuwawezesha waamini kutekeleza vyema dhamana na wito wao wa: kinabii, kikuhani na kifalme, waliojitwalia kwa njia ya Ubatizo.

Padre Marko Rupnik, anakaza kusema, ubinafsi umewameza watu wengi kiasi cha kushindwa kushuhudia: uzuri, wema na utakatifu wa Kanisa. Wafanyakazi katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kwenye vyombo vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, wanapaswa kuutekeleza utume wao kama sadaka na dhabihu inayompendeza Mungu. Watekeleze dhamana hii kwa kujikita katika: ubunifu, weledi, uadilifu na uwajibikaji mkuu kama ushuhuda wa Kristo Yesu katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anakazia umaskini wa Kanisa kama ushuhuda wenye mvuto katika mchakato wa uinjilishaji mpya!

Mashambulizi mbali mbali yanayoelekezwa kwa Kanisa na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa wakati huu, yanaweza kujibiwa kwa njia ya ushuhuda unaosimikwa katika upendo kwa Mungu na jirani; kwa kushuhudia ukweli katika uhuru; kwa kulipenda na kulithamini Kanisa, kwani anasema  Padre Marko Rupnik, upendo una nguvu sana kwani unafumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu! Upendo ni ushuhuda wa kazi ya mikono ya wanadamu inayotolewa Altareni kama sadaka safi inayompendeza Mungu kwa kukazia mambo msingi katika maisha. Ikumbukwe kwamba, uzuri wa Kanisa unafumbatwa katika Fumbo la Pasaka. Wafanyakazi wa tasnia ya mawasiliano kwenye vyombo vya Kanisa wawe kweli ni mashuhuda wa upendo wa Kristo unaolipyaisha Kanisa, kwa kuzingatia mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa.

Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika hotuba yake, amewashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wote waliohudhuria katika mkutano huu kama sehemu ya majiundo endelevu. Wafanyakazi hawana budi kujenga sana ana utamaduni wa kukutana na kujadiliana kwani inapendeza sana, ikiwa kama ndugu watakaa pamoja kwa umoja, upendo na mshikamano. Amewataka wafanyakazi kuwa ni mashuhuda wa: utakatifu, ukweli na uzuri wa Kanisa hasa katika kipindi hiki kigumu ambamo Kanisa linashambuliwa sana.

Wafanyakazi wametakiwa kuondokana na woga na wasi wasi usiokuwa na mashiko, kwa kujikita katika ukweli na ushuhuda kwa kutambua kwamba, ndani ya Kanisa kuna watakatifu na wadhambi ndiyo maana waamini wanamwomba Bikira Maria ili aweze kuwaombea kwani wanatambua kwamba, wao ni wadhambi. Umoja, upendo na mshikamano uliwezeshe Kanisa kuendelea kuwa ni sauti ya wanyonge! Kamwe wasipoteze kipaji cha kushangaa katika maisha, ili waweze kuangalia kwa jicho la imani matukio mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Wafanyakazi waipende kazi yao, waonesho upendo kwa Mungu na jirani na kuendelea kushirikiana na kushikamana na wote kutangaza matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Uzuri, upendo, bidii, ubunifu, vishuhudiwe katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kwamba, upendo unadumu na mengine yote yanapita!

Tasnia ya Mawasiliano
23 November 2018, 14:08