Tafuta

Vatican News
Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inapania kukuza na kudumisha majadiliano rika! Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inapania kukuza na kudumisha majadiliano rika!  (Vatican Media)

Vijana na wazee: majadiliano rika!

Vijana ambao wahenga Walatini waliwaita iuvenis, wanabeba sifa za uwezo wa kusaidia, kukimbia kwa mwendo kasi, kuona upya, kuimarisha, kuzuia, kuzalisha na hata kushika Imani. Vijana wanayo macho yenye uwezo wa kuutazama ulimwengu na kuona kile ambacho wahenga wanaona katika mtazamo wa ‘tumekuwa tukifanya hivi siku zote’.

Na Karoli Joseph AMANI, - Roma, Italia.

Kutembea pamoja (Synodality) ni mtindo fanisi wa maisha na utume wa Kanisa. Wakati ikimalizika Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana mjini Roma iliyokuwa na kauli mbiu  ‘vijana, Imani na  Mang’amuzi ya miito’, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko mjini Roma kimezindua rasmi mwaka wa masomo 2018-2019 ambao ni mwaka wa 391 tangu kuanzishwa Chuo kikuu hicho mnamo mwaka 1627. Katika uzinduzi huo, mada kiini ‘Chuo kikuu, majadiliano baina ya rika na baina ya tamaduni’ ilivyopambanuliwa na Prof. Armando Matteo mbele ya umati wa wanafunzi, wageni, waadhiri na uongozi wa juu kutoka Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika ukumbi wa Papa Benedikto wa XVI chuoni Urbaniana.

Padre Armando Matteo aling’azia macho suala la msusukosuko uliopo kati ya vijana na wazee, hususan barani Ulaya lakini pia hata mabara mengine kama ilivyobaninishwa na Mababa wa Sinodi iliyohitimishwa siku chache zilizopita. Kupitia dirisha la methali ya kichina ‘wakati wa vita vijana huwaua wazee, wakati wa Amani wazee huwaua vijana’, Padre Matteo aliiingia zaidi katika mada akikazia kusema ‘wazee wasipotumia nafasi yao kuishi kama inavyotarajiwa kwa wazee, vijana watashindwa kuishi kama vijana. Wazee wakiishi kama vile vijana katika kipindi chao cha uzee vijana watashindwa kuchukua nafasi yao kama vijana na matokeo yake ni jamii nzima kuingia katika msukosuko’.

Ni desturi katika tamaduni zote za walimwengu kwamba, vijana huiga mifano kutoka kwa wazee wao. Wazee ni hazina ya maadili na uzoefu kwa vijana kwa sababu tayari wazee wameshaishi duniani kabla ya vijana. Kwa sababu ya uwepo wa wazee, vijana wanayo mabega ya kupanda il kuweza kuuona kwa matumaini mustakabari wao na wa jamii nzima kiujumla. Lakini ni kindumbwendumbwe hivi leo kushuhudia wazee wakiiga mitindo ya vijana na kung’ang’ania kuishi kama vijana katika kipindi ambacho wao siyo tena vijana! (Instrumentum laboris).

Vijana ambao wahenga Walatini waliwaita iuvenis, wanabeba sifa za uwezo wa kusaidia, kukimbia kwa mwendo kasi, kuona upya, kuimarisha, kuzuia, kuzalisha na hata kushika Imani. Vijana wanayo macho yenye uwezo wa kuutazama ulimwengu na kuona kile ambacho wahenga wanaona katika mtazamo wa ‘tumekuwa tukifanya hivi siku zote’. Yaweza kutosha kutazama mapinduzi ya kidigitali ili kuonja jinsi ambavyo vijana wanaweza kuushawishi ulimwengu hata kubadili namna ya kuishi. Steve Jobs (Apple) na Mark Zuccherberg (facebook) wamefanya walioyafanya kuushawishi ulimwengu huu wakiwa katika umri wa ujana. Leo hii ulimwengu unafaidi mengi katika nyanja mbalimbali kwa mfano mawasiliano ya simu rununu na internet kupitia gunduzi za vijana kama hawa.

Pamoja na sifa na uwezo walionao vijana, hali hiyo ya ujana walioyonayo haidumu milele. Ujana una tarehe ya mwisho (una-expire). Vijana, ikiwa wanayo bahati ya kuishi miaka mingi, lazima itafika wakati itakuwa zamu yao kuwa wazee. Kwa hivyo basi, ili nao wasilete matata na kuwasumbua watakaokuwa vijana wakati wao watakapokuwa wazee, walio katika uzee sasa, ni lazima wawajibike kuwasaidia vijana kuurithi ulimwengu na kuuendeleza. Mbinu sahihi ya kulifanya hilo, wala si siri ya mtende; ni wao (wazee) kuishi kama inavyowapasa kuishi wazee, wakiwa katika uzee wao na si kuishi kama vile wangali bado vijana. Taifa lolote lenye nguvu na lililo makini na mustakabari wake linawekeza katika vijana; kuwaunda, kuwaandaa, kuwanoa, kuwahekimisha, kuwatia moyo, kuwaelekeza, kuwashujaisha kuusongesha mbele ulimwengu.

Yote hayo yanakihusu nini Chuo kikuu cha Kipapa? Kwa nini majadiliano kati ya kizazi cha zamani na kizazi kipya?. Maswali hayo yanapatiwa majibu katika kutazama wajibu msingi wa taasisi za elimu katika kubeba jukumu dhidi ya vijana yaani kuwapatia nyenzo na ueledi wa kukabiliana ulimwengu na changamoto zake. Itakumbukwa kuwa katika harakati za Sinodi ya Maaskofu mwaka huu, mabaraza mbalimbali ya maaskofu yalibainisha changamoto zinazoyakumba katika utume kwa vijana katika ulimwengu mamboleo ikiwa ni pamoja na ubinafsi uliokithiri, janga la ukosefu wa ajira,uhamiaji,vita, ukiukwaji wa haki za binadamu, biashara ya madawa ya kulevya, ukahaba, ushirikina na mengine mengi, ambayo waathirika wake wakubwa na wahusishwa nambari moja ni vijana (Documento finale no. 14).

Wachungaji hawa, wanatafuta njia ya kufaa kuboresha utume wa Kanisa kwa vijana kwa ajili ya faida ya vijana wenyewe, akanisa na ulimwengu mzima. Katika hilo vyuo vikuu vya kanisa havina budi kuchangia kutafuta suluhisho au mbinu mbadala katika kuleta mabadiliko.

Papa Francisko anaviasa vyuo vikuu vya Kanisa kwamba, ni muda sasa wa kujiweka imara kutoa elimu iliyosheheni hekima na mapinduzi jadidi ya mabadiliko ya kimisionari ambayo ni sifa madhubuti ya Kanisa linalotoka kwenda kuinjilisha (Veritatis gaudium n.3). Naam, ni katika mwelekeo huo anaoelekeza baba mtakatifu, chuo kikuu Urbaniana kupitia vitivo vyake vyote kinajibidiisha kuendelea na jukumu lake la kuwaandaa vizuri vijana wataohudumu katika makanisa mahalia kwa ustadi na utaalamu uliopambwa kwa tunu za kikristo.

Ni katika muktadha huu, vijana wa Urbaniana wanajifunza, katika vita dhidi ya changamoto za ulimwengu wetu, sio kuwaua wazee bali kujifunda kuzijua kweli za injili kinagaubaga. Walio wazee nao wanagundua kwamba uzee dawa!, Wahadhili wanajitoma kutumia utulivu wao katika ujuzi na uzoefu mbalimbali katika sayansi za Kanisa kuwarithisha vijana mafundisho ya Kanisa na kuwatia shime kuutumia ujana wao vizuri wangali wakiwa vijana. Na kwa mtindo huo Kanisa na jamii nzima itastawi na kusonga mbele kwa kishindo! 

Majadiliano rika

 

08 November 2018, 09:08