Tafuta

Vatican News
Madhabahu ni mahali pa uinjilishaji, toba na wongofu wa ndani! Madhabahu ni mahali pa uinjilishaji, toba na wongofu wa ndani! 

Madhabahu ni jukwaa la uinjilishaji, toba na wongofu wa ndani!

Madhabahu ni maeneo yanayodhihirisha ufunuo wa: ukuu, wema na huruma ya Mungu kwa waja wake, mafundisho msingi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Hapa kipaumbele cha kwanza ni uwepo wa Mungu ndani ya Kanisa na maisha ya kila mwamini. Mwenyezi Mungu ndiye anayepanga na kuamua mahali na muda wa kujifunua kati ya waja wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Madhabahu ni mahali muafaka pa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Ni mahali pa toba na wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kuchuchumilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha, kama chachu ya  utimilifu na utakatifu wa maisha. Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya,  limepewa dhamana na madaraka ya kusimamia Madhabahu ya Kimataifa kadiri ya Sheria, kanuni na taratibu za Kanisa, ili kuhakikisha kwamba: maeneo haya muhimu katika maisha na utume wa Kanisa, yanakuwa ni mahali muafaka pa uinjilishaji mpya: unaojikita katika ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo.

Hii ni sehemu ya hotuba elekezi iliyotolewa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, Jumanne, tarehe 27 Novemba 2018, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa kuhusu madhabahu linaloongozwa na kauli mbiu “Madhabahu ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya”. Kongamano hili linahitimishwa tarehe 29 Novemba 2018. Hii ni sehemu ya mbinu mkakati wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika shughuli za kichungaji. Tafakari, majadiliano na mapendekezo yatakayoibuliwa kwenye kongamano hili yanapania kuhakikisha kwamba, madhabahu yanakuwa ni vituo vya sala, toba na wongofu wa ndani; mahali pa kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo na kwamba, hivi ni vituo vya huruma ya Mungu kwa waja wake. Madhabahu ni mahali muafaka panapowasaidia waamini  kupyaisha ari na moyo wa utume ndani ya Kanisa, kwa kujikita zaidi katika maisha ya kijumuiya!

Askofu mkuu Fisichella anaendelea kufafanua kwamba, maendeleo ya madhabahu haya kwa siku za usoni yamesimikwa katika mapokeo na historia inayohifadhiwa kwenye madhabahu haya. Ni maeneo yanayodhihirisha ufunuo wa: ukuu, wema na huruma ya Mungu kwa waja wake, mafundisho msingi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Hapa kipaumbele cha kwanza ni uwepo wa Mungu ndani ya Kanisa na maisha ya kila mwamini. Mwenyezi Mungu ndiye anayepanga na kuamua mahali na muda wa kujifunua kati ya waja wake! Waamini wanapaswa kubaki katika ukimya ili kumsikiliza Mungu kwa makini, pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati kwa njia ya matukio mbali mbali yanayoweza kusaidia mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Sera na mikakati ya uinjilishaji haina budi kumwilishwa katika shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Makanisa mahalia! Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, mila na tamaduni njema za watu mahalia zinaheshimiwa na kuendelezwa, kama sehemu ya mchakato wa utamadunisho. Taalimungu ya watu mahalia inayojionesha kwa namna ya pekee katika ibada ya waamini na hasa maskini inapaswa kukuzwa na kudumishwa.

Waamini wasaidiwe kufanya hija itakayowasaidia kugundua na kupyaisha tena imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Nyenzo zinazopaswa kuzingatiwa hapa ni: sala na hapa waamini wajizoeshe kusali na kuimba Zaburi sanjari na maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho. Mapadre waliopewa dhamana ya kutoa huduma kwa mahujaji, wanapaswa kuandaliwa vyema na wala si watu kushtukiza. Ikumbukwe kwamba, mchakato mzima wa uinjilishaji unarutubishwa kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Madhabahu pawe ni kimbilio la maskini wa: kiroho na kimwili; hapa pawe ni mahali ambapo mwamini anatambua na kuonja nguvu ya Mungu inayoponya na kuokoa!

Madhabahu
28 November 2018, 15:17