Tafuta

Vatican News
Kardinali Parolin: Dunia inahitaji viongozi watakaolinda na kudumisha amani! Kardinali Parolin: Dunia inahitaji viongozi watakaolinda na kudumisha amani! 

Kardinali Parolin: Dunia inahitaji viongozi wa kudumisha amani!

Vatican inaunga mkono kampeni ya uragibishaji kwa ajili ya kupata viongozi wa kulinda amani duniani: “Leaders for peace”. Chama hiki kinawaomba viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kukiunga mkono kwa kuchangia sehemu ya bajeti yake, ili kuwafunda vijana kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha “Rondine” ni mkusanyiko wa raia kutoka Kaskazini mwa Italia wanaowekeza hasa katika majadiliano ili kupunguza, kama si kuondoa kabisa migogoro na vita sehemu mbali mbali za dunia kwa kuwekeza zaidi katika elimu makini na majiundo endelevu na fungamani miongoni mwa vijana. Lengo ni kuwawezesha vijana wa kizazi kipya kuwa viongozi watakaosimamia amani, ustawi na maendeleo ya wengi kuanzia mahali walipo! Chama cha “Rondine” kinapania kugeuza kinzani na mipasuko ya kijamii kuwa ni fursa kwa vijana kugundua utu na heshima ya binadamu, ambao hapo awali waliwaona kuwa ni adui wanaopaswa kufyekelewa mbali!

Wajumbe wa Chama cha “Rondine”, Jumatano tarehe 28 Novemba 2018 wamekutana na kuzungumza na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi na mashirika ya kimataifa mjini Vatican. Katika mkutano huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kufunda viongozi wapya watakaosimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani inayosimikwa katika majadiliano katika ukweli na uwazi ili kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mchakato huu hauna budi kufanyiwa kazi katika ngazi mbali mbali za maisha ya watu, ili kulinda haki msingi za binadamu ambazo leo hii zinasiginwa sana sehemu mbali mbali za dunia.

Nia ya Vatican kwenye uwanja wa diplomasia kimataifa ni kuhakikisha kwamba: wadau mbali mbali wanahusishwa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, ndiyo maana Vatican katika kipindi cha miaka ishirini imeendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Chama cha “Rondine” kama sehemu ya mchakato wa unaopania kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu; malezi na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya, ili hatimaye, kwa siku za usoni wawe ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa amani duniani; watu wanaoweza kujadiliana na wengine na kutafuta suluhu kwa njia ya amani badala ya kukimbilia mtutu wa bunduki.

Vatican inaunga mkono kampeni ya uragibishaji kwa ajili ya kupata viongozi kwa ajili ya amani duniani: “Leaders for peace”. Chama hiki kinawaomba viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kukiunga mkono kwa kuchangia sehemu ya bajeti yake, ili kuwafunda vijana kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani duniani. Kinapania pamoja na mambo mengine kuwaandaa viongozi wa leo na kesho bora zaidi ya mataifa duniani kwa kujikita katika haki msingi za binadamu. Tamko la kampeni hii limesomwa mbele ya wanadiplomasia wa Vatican.

Katika hotuba yake, Bwana Franco Vaccari, muasisi wa Chama hiki, amewaomba mabalozi hawa kuzishawishi nchi zao kuunga mkono kampeni hii inayodumu kwa muda wa miaka mitatu. Tayari ombi kama hili limekwisha wasilishwa kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia, hapo tarehe 11 Oktoba 2018, tarehe 3 Desemba, ombi la kampeni hii litawasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko na tarehe 10 Desemba 2018, viongozi wake wataliwasilisha kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, huko New York, nchini Marekani, kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuchapishwa kwa Tamko la Haki Msingi za Binadamu! Kufunda viongozi wa amani; watakaosimama kidete kujenga umoja na udugu; ili kuwaondolewa watu vita na madhara yake kwa njia ya elimu makini, endelevu na fungamani ni changamoto inayopaswa kuungwa mkono na wengi!

Uhuru wa kidini ni msingi wa: haki, utu na heshima ya binadamu! Uhuru wa kidini ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa, kukuzwa na kudumishwa na wote kwani ni msingi wa haki zote za binadamu, utu na heshima yake: Kumbe, umoja na mshikamano; amani na utulivu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni muhimu sana!  Jumuiya ya Kimataifa katika kipindi cha mwaka 2018 inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu kusitishwa kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, changamoto kwa sasa ni ujenzi wa amani duniani inayofumbatwa katika ukweli, haki, mshikamano tendaji na uhuru wa kweli!

Haya ni kati ya mambo msingi yanayobainishwa kwenye Tamko la Haki Msingi za Binadamu, ambalo, ambalo wengi wanaliangalia kama sheria mama na chombo cha maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa tarehe 3 Desemba 2018 inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuchapishwa kwake!  Kuheshimu na kudumisha haki msingi za binadamu ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa nyakati hizi! Lakini, ikumbukwe kwamba, haki msingi za binadamu ni msingi na mhimili mkuu wa: amani, ustawi, maendeleo, mafao, umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, vita, kinzani na mipasuko ya kidini ni matokeo ya kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema! Nchi nyingi zimeshindwa kutekeleza kwa vitendo Tamko la Haki Msingi za Binadamu. Kwa bahati mbaya sana, haki msingi za binadamu zinatafsiriwa kwa mwono binafsi, kiasi kwamba, hata amani linakuwa ni jambo la binafsi, hatari kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Dhana ya vita halali na ya haki imepitwa na wakati kwani, vita haina macho wala pazia! Kanisa kwa asili, maisha na utume wake anasema Baba Mtakatifu Francisko linapaswa kuwa ni chombo cha haki, amani na upatanisho. Leo hii amani ni changamoto pevu kutokana na kushamiri kwa biashara ya silaha duniani! Uchu wa mali na utajiri wa muda mfupi unawafumba watu macho kiasi cha kushindwa kuona mahitaji ya jirani zao. Kumbe, amani inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru.

Viongozi wa Amani

 

29 November 2018, 09:52