Vatican News
Papa Francisko: Siku II Maskini Duniani 2018: Maskini huyu aliita na Bwana akamsikia! Papa Francisko: Siku II Maskini Duniani 2018: Maskini huyu aliita na Bwana akamsikia  (AFP or licensors)

Siku ya Maskini Duniani kwa mwaka 2018: Changamoto za umaskini!

Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa wale wasiokuwa na sauti katika: masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, kwa kujikita zaidi: katika utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya anasema, maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani ni changamoto inayotolewa na Mama Kanisa kwa Jumuiya ya Kimataifa, kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia. Maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu na kwamba, bado kilio cha maskini hakijasikilizwa hata kidogo, kwani hata leo hii, kuna watu wanataka “kuwashikisha adabu maskini, ili wafunge midomo yao na kamwe wasiendelee kuleta kero duniani”.

Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Pili ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2018 yanaongozwa na kauli mbiu “Maskini huyu aliita na Bwana akamsikia” anasema kuna mamilioni ya watu wanaoendelea kuteseka kutokana na umaskini wa hali na kipato, kiasi kwamba utu na heshima yao vinawekwa rehani. Hawa ndio ambao Mama Kanisa anataka sauti yao isikike na watu wajibu kilio chao! Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa wale wasiokuwa na sauti katika: masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, kwa kujikita zaidi: katika utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mama Kanisa anapenda kushirikiana na kushikamana na watu wote wenye mapenzi mema, wanaotaka kujisadaka na kujifunga kibwebwe ili kupambana na umaskini duniani, bila ya kujali imani, dini, tabaka na mahali anapotoka mtu. Lengo ni kupambana na umaskini duniani hadi kieleweke! Hii inatokana na ukweli kwamba, umaskini hauna dini, kabila wala rangi! Kanisa linataka kushikamana na wadau mbali mbali watakaokuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu katika kupambana na mifumo mbali mbali ya umaskini duniani, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani inayofumbatwa katika matendo. Maskini wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma, haki na mapendo, ili kulinda na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu!

Askofu mkuu Fisichella anaendelea kufafanua kwamba, tema ya umaskini wa hali na kipato ni kati ya mada zilizochambuliwa kwa kina na mapana na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018 na kupewa msisitizo wa pekee katika Hati ya Mababa wa Sinodi wanaokazia pamoja na mambo mengine: ubora wa elimu, malezi na makuzi fungamani yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mababa wa Sinodi wanasema, kuna haja ya kuwekeza katika sera na mifumo ya uchumi shirikishi ili kuwajengea vijana uwezo wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao, ili kamwe wasitumbukizwe katika biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo; vita na vitendo vya kigaidi vinavyonyanyasa utu na heshima ya binadamu.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella anahitimisha kwa kusema, hizi zote ni changamoto changamani zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo na Kanisa linataka kutoa majibu muafaka kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini. Vijana ni kati ya watu wanaoelemewa na umaskini sehemu mbali mbali za dunia, kiasi kwamba, baadhi yao wanalazimika kuzikimbia nchi zao, ili kutafuta fursa za ajira, hifadhi na usalama wa maisha yao! Vijana wakipewa malezi na makuzi bora zaidi, wanaweza kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo na mshikamano unaomwilishwa katika Injili ya upendo!

Siku ya Maskini Duniani 2018
14 November 2018, 10:29