Tafuta

Vatican News
Papa Francisko akutana na kuzungumza na Rais Barham Saleh wa Iraq: Mkazo: Upatanisho na umoja wa Kitaifa Papa Francisko akutana na kuzungumza na Rais Barham Saleh wa Iraq: Mkazo: Upatanisho na umoja wa Kitaifa  (ANSA)

Papa Francisko akutana na Rais wa Iraq: Upatanisho na umoja wa kitaifa!

Viongozi hawa wanasema, changamoto kubwa mbele ya familia ya Mungu nchini Iraq ni mchakato wa upatanisho ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa. Katika mazingira kama haya, wamegusia umuhimu wa uwepo wa Wakristo nchini Iraq, kwani wao pia ni sehemu fungamani ya watu wa Mungu nchini humo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 24 Novemba 2018 amekutana na kuzungumza na Rais Barham Saleh wa Iraq ambaye, baadaye amekutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Baba Mtakatifu pamoja na Rais wa Iraq katika mazungumzo yao ya faragha wameridhika na uhusiano mwema uliopo kati ya nchi hizi mbili sanjari na maendeleo endelevu katika masuala ya kisiasa pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika medani za kimataifa.

Viongozi hawa wanasema, changamoto kubwa mbele ya familia ya Mungu nchini Iraq ni mchakato wa upatanisho ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa. Katika mazingira kama haya, wamegusia umuhimu wa uwepo wa Wakristo nchini Iraq, kwani wao pia ni sehemu fungamani ya watu wa Mungu nchini humo na wanao mchango katika mchakato wa ujenzi na mafungamano ya kijamii. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, Wakristo wanaendelea kuishi katika nchi yao na wale walioko uhamishoni, wajengewe mazingira ili waweze kurejea tena nchini mwao ili kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa nchi yao.

Jambo la msingi ni uwepo na udumifu wa amani na usalama, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Iraq. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko na Rais Barham Saleh wa Iraq wamegusia vita na kinzani zinazoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Wamekazia umuhimu wa wananchi wa Iraq kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kikabila ili kujenga na kudumisha amani na utulivu kati ya watu wa Iraq.

24 November 2018, 14:25