Tafuta

Vatican News
Mwenyeheri Clelia Merloni ni shuhuda wa wema na huruma ya Mungu! Mwenyeheri Clelia Merloni ni shuhuda wa wema na huruma ya Mungu!  (Vatican Media )

Mwenyeheri Clelia Merloni ni shuhuda wa wema na huruma ya Mungu!

Mwenyeheri Clelia Merloni, kuwa Mwenyeheri. Huyu ni mwanamke wa shoka, ambaye maisha yake yote yalipambwa kwa chapa ya Fumbo la Msalaba, akajichotea neema na faraja kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu; katika sala na tafakari, akajiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kujisadaka kwa ajili ya upendo kwa jirani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 4 Novemba 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amemkumbuka Mwenyeheri Clelia Merloni, mwanzilishi wa Shirika la Mitume wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Huyu ni mtawa aliyejitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, akajisadaka kwa ajili ya upendo kwa Mungu na jirani, akavumilia na kusamehe. Ni kutokana na ushuhuda huu angavu, Mama Kanisa anamshukuru Mungu kwa kumjalia Mwenyeheri Clelia Merlon, kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika wema na huruma!

Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 3 Novemba, 2018 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano mjini Roma, amemtangaza Mtumishi wa Mungu Clelia Merloni, kuwa Mwenyeheri. Huyu ni mwanamke wa shoka, ambaye maisha yake yote yalipambwa kwa chapa ya Fumbo la Msalaba, akajichotea neema na faraja kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu; katika sala na tafakari, akajiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kujisadaka kwa ajili ya upendo kwa jirani!

Kardinali Becciu katika mahubiri yake anasema, huu ndio utambulisho wa maisha ya kiroho wa Mwenyeheri Clelia Merloni, aliyethubutu kuwasamehe hata watesi wake, kama chemchemi ya upendo kwa Mungu na jirani. Alisingiziwa mambo mengi, akateswa na kunyanyaswa, kiasi hata cha kulazimika kuacha madaraka na kuondoka kwenye Shirika lake la kitawa, alilokuwa amelianzisha mwenyewe! Afya yake ikadhohofu, akatengwa na rafiki zake, kiasi hata cha kuonja upweke chanya uliomwezesha kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, asili ya wema wote!

Fumbo la Msalaba likawa ni faraja katika hija ya maisha yake ya kiroho, daima akaiona ile sura ya Bikira Maria, akiwa pale chini ya Msalaba na hapo imani yake, ikachanua tena na tena kama mtende wa Lebanoni! Akajichotea nguvu ya maisha ya kiroho kutoka katika Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kiasi hata cha kuthubutu kuwasamehe watesi wake na kusahau yaliyopita, daima akiyatolea mateso na mahangaiko yake ya ndani kwa ajili ya msamaha wa dhambi, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka!

Kardinali Becciu anakaza kusema, Kristo Yesu, aliendelea kuwa ni kiini cha imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Akajitahidi kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Akahakikisha kwamba, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanapewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wao kama watawa, ili kujichotea nguvu ya kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Kauli mbiu katika maisha yake, ilikuwa “Mungu kwanza” na kweli akawa ni kimbilio katika maisha yake ya sala na tafakari, yaliyomwilishwa pia katika matendo ya huruma kwa watoto wadogo, maskini, wagonjwa na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii! Kwa hakika anasema, upendo wa Kristo ulikuwa unamwajibisha!

Mama Kanisa anaweka mbele ya watoto wake mifano ya watakatifu, ili kuwaheshimu na kuiga mifano yao, ili hata wao pia waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa Kristo unaobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu uliotobolewa kwa mkuki na ukawa ni chemchemi ya maisha mapya yanayofumbatwa katika Sakramenti za Kanisa! Upendo wa Kristo ukamwezesha kujisadaka kwa ajili ya kuwapatia wasichana elimu makini, chachu ya ukombozi katika maisha yao. Ni katika Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mwenyeheri Mwenyeheri Clelia Merloni akajifunza kusali kwa moyo wa ibada na uchaji wa Mungu pamoja na kuvumilia mateso kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Mwishoni mwa mahubiri yake, Kardinali Giovanni Angelo Becciu, anawataka Masista wa Shirika la Mitume wa Moyo Mtakatifu wa Yesu kupyaisha karama ya Shirika lao, kwa kuzama zaidi katika maisha ya sala na tafakari, chemchemi ya upendo unaosamehe, kwani huu ndio utume ambao ni asili ya kuanzishwa kwa Shirika lao. Kauli mbiu ya Shirika hili ni “Caritas Christi urget nos” yaani “Upendo wa Kristo unatuwajibisha” kuzama na kujisadaka kwa ajili ya upendo kwa Mungu na jirani pasi na kujibakiza hata kidogo! Chachu ya utakatifu wa maisha, inayobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba, uwe ni mwanga angavu katika shule ya upendo kwa Mungu na jirani!

Kardinali Becciu
05 November 2018, 12:18