Tafuta

Papa Francisko: Changamoto za maisha na utume wa Kanisa sasa kushughulikiwa kisinodi! Papa Francisko: Changamoto za maisha na utume wa Kanisa sasa kushughulikiwa kisinodi! 

Changamoto za maisha na utume wa Kanisa kushughuilikiwa kisinodi

Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa: ndiyo njia muafaka kwa Kanisa kuweza kupambana na changamoto za maisha na utume wake, tayari kuambata toba na wongofu wa kimisionari, chachu msingi katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kamati kuu iliyoundwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko ili kuratibu mkutano maalum wa Kanisa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia utakaofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019 ni sehemu ya utekelezaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Hii ndiyo njia muafaka kwa Kanisa kuweza kupambana na changamoto za maisha na utume wake, tayari kuambata toba na wongofu wa kimisionari, chachu msingi katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Hii ni Kamati itakayoandaa mkutano pamoja na kumshauri Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa na Kanisa ili kuzuia nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo

Askofu mkuu Charles Jude Scicluna, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, mtaalam liyebobea katika kesi za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa katika mahojiano maalum na “Jalida la America”, anasema, huu ni mkutano wa kwanza kabisa kuitishwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kushughulikia kikamilifu kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa la kiulimwengu. Zaidi ya Marais wa Mabaraza ya Maaskofu kutoka katika nchi 100, wakuu wa Makanisa ya Mashariki na viongozi wakuu wa Sekretarieti kuu ya Vatican wanatarajiwa kuhudhuria, kielelezo cha “urika wa maaskofu” chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Mkutano huu unaonesha kwamba, Baba Mtakatifu anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika ulinzi na usalama wa watoto katika mazingira ya Makanisa mahalia. Hii ni changamoto ya kimataifa na wala si kwa maeneo fulani tu ya kijiografia, inayopaswa kuvaliwa njuga kwa umoja na mshikamano; kwa kuheshimu na kuzingatia tamaduni za watu mbali mbali zisizosigana na Habari Njema ya Wokovu. Huu ni mkutano wa siku nne, unaotarajiwa kuanza mchakato wa utekelezaji wa sera na mikakati mbali mbali kwa ajili ya kuwalinda na kuwaendeleza watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Askofu mkuu Charles Scicluna anasema, changamoto hii itaweza kuangaliwa pia kwa “miwani ya mila, desturi na tamaduni mbali mbali duniani”, ili baadaye, sera na mikakati hii, iweze kumwilishwa katika maisha na utume wa Makanisa mahalia. Maaskofu katika mjadala wao wanapaswa kutambua kwamba, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni kosa la jinai, lakini zaidi ni dalili za watu kukengeuka na kutopea katika mmong’nyoko wa kanuni maadili na utu wema! Ni kashfa inayolidhalilisha Kanisa lenye wajibu na dhamana ya kuwaundia watoto wazingira safi na salama kwa malezi na makuzi yao endelevu na fungamani.

Ni nafasi kwa Maaskofu kutambua dhamana na wajibu wao katika kukabiliana na kesi za nyanyaso za kijinsia katika ukweli, uwazi pamoja na kuzingatia haki. Tabia ya baadhi ya Maaskofu kuwalinda watuhumiwa wa kesi za nyanyaso za kijinsia ni kwenda kinyume cha ukweli, uwazi na haki na matokeo yake ni kukwamisha maisha na utume wa Kanisa na madhara yake ni makubwa kwa watu wa Mungu! Kwa hakika, ukweli utaliweka Kanisa huru, kwa kuhakikisha kwamba, wakleri na watawa wenye tabia chafu kama hizi wanatambulikana na kupewa matibabu kadiri ya sheria na haki msingi za binadamu kama njia ya Kanisa kuwajibika barabara! Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni Mama na Mwalimu pale inapobidi, lazima kuwawajibisha watoto wake.

Maaskofu na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanapaswa kutambua madhara makubwa ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia kwa maisha na utume wa Kanisa, ili kuchukua hatua madhubuti ili vitendo kama hivi visiweze kujirudia tena. Hapa kinachopewa msukumo wa pekee ni ukweli, uwazi na uwajibikaji katika maisha na utume wa Kanisa katika mtazamo wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Waamini walei wanapaswa hata wao kujengewa uwezo wa kupambana na kashfa za nyanyaso za kijinsia, kwani matendo kama haya yanafanyika hata ndani ya familia zenyewe! Ulinzi na usalama wa watoto unapaswa kuanzia ndani ya familia zenyewe.

Kumbe, changamoto zitakazokuwa zimeibuliwa na Maaskofu pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume zitapaswa kufanyiwa kazi katika Makanisa mahalia hadi kwenye Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Wito, karama na tamaduni mbali mbali zishirikishwe katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Maaskofu watapata nafasi ya kuwasikiliza waathirika, kuzungumza na wataalam wa mambo haya; kutafakari na hatimaye, Maaskofu kuweza kushirikishana na mang’amuzi yao, ili hatimaye, kuibu mbinu mkakati utakaotumiwa na Mama Kanisa katika kudhibiti vitendo hivi vya kinyama. Maaskofu watasikiliza hotuba, watajadiliana katika vikundi na hatimaye, wataweza kutoa mapendekezo.

Maaskofu wataangalia vipaumbele vya Mama Kanisa katika mapambano haya na hatimaye, watashiriki Liturujia ya Toba na Wongofu wa Kimisionari. Huu ni mkutano wa matumaini ya watu wa Mungu na Kanisa katika ujumla wake unaokazia: ulinzi na usalama kwa watoto wadogo; malezi na makuzi kwa wakleri na mihimili yote ya uinjilishaji pamoja na kukazia sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Mchakato huu wa Kisinodi utakapokamilika, Maaskofu watatoa mapendekezo ambayo yatafanyiwa kazi na Baba Mtakatifu pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican.

Nyanyaso za kijinsia

 

26 November 2018, 09:06