Tafuta

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019: Utume wa Wabatizwa Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019: Utume wa Wabatizwa 

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019: Utume wa Wabatizwa!

Papa Benedikto XV katika Waraka wake wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari” alifungua rasmi ukurasa mpya wa maisha na utume wa Kanisa mintarafu shughuli za kimisionari, kwa kulitaka Kanisa kuanzisha mchakato wa majiundo na malezi kwa ajili ya kuyategemeza Makanisa mahalia kwa rasilimali watu, yaani wahudumu wa Injili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa”.  Kanisa linaendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Hiki ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni muda wa kutangaza furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa; Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ari na ushiriki mkamilifu na hatimaye, Kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Mwezi Oktoba 2019 Kanisa litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Ni muda wa: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma! Ni wakati kwa waamini walei kutambua haki, dhamana na wajibu wao katika maisha na utume kwa Kanisa. Hii ni fursa ya kuwahimiza waamini kujiwekea sera na mikakati ya kuyategemeza Makanisa mahalia: kwa njia ya rasilimali watu, vitu na fedha, ili Kanisa liendelee kutangaza Injili ya huruma na upendo hadi miisho ya dunia!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linapaswa kujiekeleza zaidi katika utekelezaji wa mambo makuu manne: Mosi, waamini kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na Sala. Pili ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tatu ni majiundo makini, endelevu na fungamani ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne ni huduma ya upendo kama kielelezo cha imani tendaji!

Huu ni msisitizo ambao unaendelea kutolewa na Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso, Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, wakati wa mkutano wake uliohitimishwa hivi karibuni kwa kuridhia mabadiliko yaliyofanywa kwenye Sala ya Baba Yetu wa Mbinguni “Usituache katika kishawishi” na “Wimbo wa Utukufu kwa Mungu Juu”. Lengo ni kupyaisha tena ari na mwamko wa kimisionari ambao waamini wamejitwalia kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, ili kuwa na mashiko na mvuto, kielelezo makini cha uinjilishaji mpya.

Papa Benedikto XV katika Waraka wake wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari” alifungua rasmi ukurasa mpya wa maisha na utume wa Kanisa mintarafu shughuli za kimisionari, kwa kulitaka Kanisa kuanzisha mchakato wa majiundo na malezi kwa ajili ya kuyategemeza Makanisa mahalia kwa rasilimali watu, yaani wahudumu wa Injili! Baada ya miaka 100, Kanisa linawataka waamini kuendeleza mchakato wa kulitegemeza Kanisa kwa rasilimali fedha na vitu, ili kusongesha mbele shughuli za uinjilishaji wa kina, unaofumbata mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili!  

Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso, anasema, ifikapo mwaka 2022, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa kwake; Miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari na miaka 100 tangu baadhi ya Mashirika ya kitume yalipopewa hadhi ya kuwa ni Mashirika ya Kipapa, ili kuweza kulihudumia Kanisa la Kristo ulimwenguni kote. Mama Kanisa anataka kutangaza na kushuhudia habari Njema ya Wokovu kutoka kwa Kristo Yesu.

Ni kwa utashi wa Papa Pio XI, Siku ya Kimisionari Duniani, ilianzishwa kunako mwaka 1920 ili kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutangaza furaha ya Injili kwa waamini kuchangia kwa hali na mali katika utume ambao Kanisa limeyakabidhi Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa na kwamba, hii ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na watu wote wa familia ya Mungu!

Mwezi Oktoba 2019

 

28 November 2018, 10:44