Vatican News
Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018 Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018  (AFP or licensors)

MKATABA WA KIMATAIFA WA USALAMA WA WAHAMIAJI 2018

Kimsingi “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unapania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Padre Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu anasema, Vatican ina matumaini makubwa kuhusu utashi wa kisiasa utakaonesha umoja na mshikamano katika mchakato wa kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, kwa kutia sahihi ya makubaliano ya Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018, baada ya kufanyiwa kazi kwa muda wa miaka miwili.

Kuanzia tarehe 10-11 Desemba 2018, huko Marrakesh, nchini Morocco zaidi ya vyama 500 vya kiraia vitashiriki ili kusikiliza tamko la viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu Mkataba wa Usalama wa Wahamiaji 2018. Vatican inatarajiwa kupeleka ujumbe mzito kwenye mkutano huu! Itakumbukwa kwamba, Vatican imechangia sana katika maboresho ya Mkataba huu na sasa ingependa kuona utekelezaji wake katika ngazi ya kimataifa kwa kukazia mambo makuu ishirini yanayopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa.

Padre Czerny anasema, lengo ni kuhakikisha kwamba, Mkataba huu unasaidia mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana; utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; pamoja na kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, kwa kujenga hofu zisizokuwa na mvuto wala mashiko. Kuna nchi kadhaa ambazo tayari zimetishia kutotia sahihi makubaliano kuhusu Mtakaba huu nazo ni: Marekani, Hungaria, Australia, Austria Bulgaria pamoja na Italia. Pamoja na changamoto zote hizi, Vatican bado ina matumaini makubwa kwamba, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji itapatiwa majibu muafaka kadiri ya hali, mazingira na uwezo wa nchi husika.

Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018  unaondaliwa na Umoja wa Mataifa unalenga kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya wahamiaji! Umuhimu wa Jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji sanjari na kudumisha usalama na maisha bora zaidi. Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa wahamiaji unapania pamoja na mambo mengine, kuboresha: ulinzi na usalama; haki msingi za binadamu pamoja na wakimbizi kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria pale haki zao zinapovunjwa.

Mkataba huu unawatupia jicho wakimbizi na wahamiaji hatari kwa maisha na usalama wa raia wengine. Watu hatari wanaweza kurejeshwa makwao pamoja na  uwezekano wa kudhibiti uhuru wa wakimbizi. Kimsingi “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unapania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa kwa baadhi ya serikali pamoja na kuangalia umuhimu wa kutumia nguvu ya wakimbizi katika kuzalisha na kutoa huduma, mwishoni ni suala la udhibiti wa mipaka!

Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowakirimia. Baba Mtakatifu Francisko, tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameguswa sana na matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini, changamoto na mwaliko kwa familia ya binadamu kusoma alama za nyakati!

Katika mchakato wa kukabiliana na changamoto hizi, Baba Mtakatifu ameanzisha kitengo maalum cha wakimbizi na wahamiaji katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu, ambacho kinawajibika moja kwa moja kwake, kama kielelezo makini cha huduma ya mshikamano wa Kanisa na wakimbizi, wahamiaji, watu wasiokuwa na makazi pamoja na waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaobisha hodi kwenye malango ya watu mbali mbali duniani, ni nafasi muhimu sana ya kuweza kukutana na Kristo Yesu, ambaye anajitambulisha kama mkimbizi na mhamiaji anayekataliwa na kubezwa na watu wa nyakati mbali mbali.

Mama Kanisa anapenda kuwaonesha upendo wake wa dhati, wakimbizi na wahamiaji, katika hatua mbali mbali za safari yao, tangu wanapoondoka, wanapofika na hatimaye, kurejea tena makwao hali inaporuhusu. Waamini wakishirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, wanaalikwa kuyavalia njuga matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji, kwa kuwaonesha moyo wa ukarimu, hekima na busara, kila mmoja kadiri ya uwezo na nafasi yake. Lakini, wote kwa pamoja wanaweza kujibu kilio na changamoto hizi kwa kujikita katika mchakato unaofumbatwa katika mambo makuu yafuatayo yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika uhalisia wa maisha ya watu wanaowakirimia.

Mkataba wa Wakimbizi 2018
29 November 2018, 10:31