Tafuta

Vatican News
PMS: Waamini wanahamasishwa kuchangia kwa ukarimu katika maisha na utume wa Kanisa. PMS: Waamini wanahamasishwa kuchangia kwa ukarimu katika maisha na utume wa Kanisa.  (AFP or licensors)

PMS: Waamini onesheni ukarimu kwa kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa

Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa wanapaswa kutumia vyema maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ili kuwafikia watu wengi zaidi na hivyo kuongeza pia idadi ya wachangiaji katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mashirika ya Kipapa ni vyombo muhimu sana katika uhamasishaji wa kazi za kimisionari, umoja na mshikamano chini ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Jukumu kuu la Mashirika haya ni kuhamasisha roho ya kimisionari miongoni mwa familia ya Mungu kwa: kuelekeza, kuratibu na kuhamasisha shughuli za uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili; mafunzo ya kimisionari; ukuzaji na uimarishaji wa malezi na miito mbali mbali ndani ya Kanisa. Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kuanzia tarehe 7- 9 Novemba 2018 wamkuwa wakishiriki mkutano uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu “Kuhamasisha na kuchangisha fedha katika ulimwengu wa kidigitali.

Wajumbe wamekumbushwa kwamba, kuchangia ustawi na maendeleo ya Kanisa ni wajibu na dhamana kutoka katika Injili ya Kristo, ili kuhakikisha kwamba, Injili ya Kristo inasonga mbele. Wajumbe wamekumbushwa umuhimu wa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuzingatia kanuni maadili, ukweli na uwazi kwani fedha zinazochangwa na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema ni kwa ajili ya kusaidia mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa wanapaswa kutumia vyema maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ili kuwafikia watu wengi zaidi na hivyo kuongeza pia idadi ya wachangiaji katika maisha na utume wa Kanisa. Wachangiaji kwa njia ya mitandao ya kijamii ni wale ambao si rahisi kwao kufuatlia moja kwa moja shughuli mbali mbali zinazotekelezwa na Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Paul Tighe, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni amefafanua maana ya ulimwengu wa kidigitali katika maisha na utume wa Kanisa na umuhimu wa kutumia lugha mpya, ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi ambao wengi wao ni vijana, vinginevyo, watapata taabu sana kuwafikia raia katika ulimwengu wa kidigitali. Wajumbe wamekumbushwa kwamba, mawasiliano yanalenga kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu wa familia ya Mungu.

Kampeni zozote zinazofanywa na Kanisa hazina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi, ili kuamsha ndani ya watu ari na mwamko wa kujisadaka kwa ajili ya wengine. Wajumbe pia wamegusia changamoto na matatizo wanayokumbana nayo katika mchakato mzima wa kuhamasisha kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa. Kampeni ya kuchangia kwa ajili ya maadhimisho ya Mwezi Oktoba 2019, Kanisa litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Ni muda wa: sala, katakesi, tafakari na matendo ya huruma! Ni wakati muafaka kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanatelekeza vyema dhamana na wajibu waliojitwaliwa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayowashirikisha: Unabii, Ukuhani na Ufalme wa Kristo. Waamini wakiwa wamezaliwa kwa “Maji na Roho Mtakatifu”, wanawajibu wa kukiri na kutangaza imani ambayo wameipokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa na hivyo kushiriki katika utendaji wa kitume na wa kimisionari wa Taifa la Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya anasema, Kanisa linapaswa kujiekeleza zaidi katika utekelezaji wa mambo makuu manne: Mosi, waamini kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na Sala. Pili ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tatu ni majiundo makini na endelevu ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne ni huduma ya upendo kama kielelezo cha imani tendaji!

Mashirika ya Kipapa
10 November 2018, 15:14