Vatican News
Mtakatifu Paulo VI: Nobis in animo! Umuhimu wa Kanisa kuendelea kuwepo katika Nchi Takatifu Mtakatifu Paulo VI: Nobis in animo! Umuhimu wa Kanisa kuendelea kuwepo katika Nchi Takatifu 

Kardinali Sandri: Amani na mshikamano wa upendo kwa ajili ya Nchi Takatifu

Katika Wosia huu, Mtakatifu Paulo VI alikazia sana umuhimu wa uwepo endelevu wa Kanisa katika Nchi Takatifu kama amana na urithi wa imani; ushuhuda endelevu wa Jumuiya ya Wakristo wanaoonesha jiografia ya ukombozi. Huu ndio ukawa mwanzo wa kukusanya Sadaka ya Ijumaa kuu kutoka kwa Makanisa yote duniani, kama alama ya upendo na mshikamano wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki kuanzia tarehe 26-28 Novemba 2018 amefanya ziara ya kichungaji katika Nchi Takatifu ambako ameshiriki katika Kongamano la Kimataifa la Makamisaa wa Nchi Takatifu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Imekuwa ni fursa ya kuendelea kuhamasisha umuhimu wa hija za maisha ya kiroho, shuhuda za tunu msingi za Kikristo pamoja na kuragibisha umuhimu wa sadaka inayotolewa na waamini Ijumaa Kuu.

Kimsingi, sadaka hii inalenga kudumisha amani katika maeneo matakatifu, kwa kuwawezesha wakristo kuendelea kuwa ni vyombo vinavyotumiwa na Kristo mwenyewe kwa ajili ya mafao ya eneo la Mashariki ya Kati. Ni mchango unaosaidia utekelezaji wa mikakati ya kichungaji katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu na fungamani, kielelezo makini cha umoja na upendo wa Kanisa unaowaunganisha na kuwawajibisha Wakristo wote pamoja na kuwasaidia Wakristo kuendelea kubaki huko Mashariki ya Kati. Hiki ni kielelezo cha mshikamano wa Kanisa katika kukuza na kudumisha: umoja, upendo na haki msingi za binadamu.

Kardinali Sandri kwa namna ya pekee, amewakumbuka na kuwaombea Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaoendelea kuteseka, kunyanyaswa na hata kuuwawa huko Mashariki ya Kati, lakini hasa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Amefanya rejea ya kina kuhusu Wosia wa Kitume wa Mtakatifu Paulo VI “Nobis in animo” yaani “Umuhimu wa Kanisa katika Nchi Takatifu”. Katika Wosia huu, Mtakatifu Paulo VI alikazia sana umuhimu wa uwepo endelevu wa Kanisa katika Nchi Takatifu kama amana na urithi wa imani; ushuhuda endelevu wa Jumuiya ya Wakristo wanaoonesha jiografia ya ukombozi. Huu ndio ukawa mwanzo wa kukusanya Sadaka ya Ijumaa kuu kutoka kwa Makanisa yote duniani, kama alama ya upendo na mshikamano wa Kanisa na kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini.

Kardinali Sandri anaendelea kufafanua kwamba, utunzaji wa maeneo matakatifu, amana, utajiri na urithi wa imani ya Kanisa, ni kielelezo muhimu sana cha umoja na mshikamano wa Kanisa. Hii ni sehemu ya Njia ya Msalaba, iliyopelekea: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu, kiini cha imani. Nchi Takatifu ni maeneo ya hija yanayoweza kuwasaidia waamini kupyaisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendeleza utamaduni wa kutoa Sadaka ya Ijumaa kuu kwa ajili ya kutunza maeneo matakatifu.

Kardinali Sandri akiwa huko amepata pia fursa ya kuwatembelea na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa Makanisa, maeneo ya huduma na kwa namna ya pekee shule ya “Terra Sancta School” iliyofanyiwa ukarabati mkubwa. Hii ni shule iliyoanzishwa kunako mwaka 1645. Amewatembelea watawa wa ndani; amekutana na viongozi mbali mbali wa Makanisa ya Mashariki, kama kielelezo cha kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: ushuhuda wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kituo cha Tantur kilianzishwa kwa jitihada za Mtakatifu Paulo VI ili kuhamasisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene, maisha ya sala na tafakari!

Kardinali Sandri: Nchi Takatifu

 

28 November 2018, 11:23