Tafuta

Vatican News
Diplomasia inafumbatwa katika majadiliano ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja, udugu na ushirikiano. Diplomasia inafumbatwa katika majadiliano ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja, udugu na ushirikiano.  (AFP or licensors)

Diplomasia ya Kanisa: Upatanisho na kusikiliza kilio cha maskini na utunzaji bora wa mazingira!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, diplomasia ni chombo cha majadiliano katika ukweli na uwazi; ushirikiano na upatanisho katika medani mbali mbali za maisha, ili kukuza na kudumisha amani, chachu ya maendeleo endelevu na fungamani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Diplomasia ya Kanisa inalenga kukuza na kudumisha misingi ya: haki, amani, umoja, udugu, ushirikiano pamoja na mafao ya wengi. Diplomasia ya majadiliano na watu kukutana ni kati ya vipaumbele vya kwanza katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na mataifa mengine yanafanyika kwa uvumilivu mkubwa, hata sehemu ambazo kuna hali tete, kwani kuna matumaini ya familia bora ya wanadamu kwa siku za mbeleni. Shughuli za kidiplomasia zinakuwa nyenzo katika kufuatilia, kushiriki, na kutoa ushawishi katika Jumuiya na maisha ya Kimataifa, kama sehemu ya mchakato wa upatanisho, ili hatimaye, kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama abnavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, “Laudato si”.

Utume wa Kanisa ni kuhangaikia kwa matumaini na kushuhudia ile hamu ya amani, haki na mafao ya wengi. Kanisa linapenda kutangaza Injili ya amani katika maeneo yenye: vita, ghasia na mipasuko ya kijamii. Diplomasia ya Kanisa sio upendeleo kwa Kanisa, bali ni haki ya msingi ambayo Kanisa inayo, na hivyo, katika Jumuiya ya Kimataifa, Kanisa lina haki sawa kama vyombo na Jumuiya zingine wanachama. Kwa zama hizi, ni wajibu wa Kanisa kutafuta mahusiano ya amani kati ya Mataifa, wakati likizingatia lengo la mwisho, yaani wokovu wa roho za watu.

Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican alipokuwa anashiriki katika kongamano la Shirikisho la Upendo Kisiasa; ambamo wajumbe wameitaka Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza na kujibu kilio cha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kilio cha maskini, ili kulinda na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu! Majadiliano kati ya watu wa Mataifa: kidini, kitamaduni, kikabila na kimaadili ni muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani.

Ushirikiano ni muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kupambana na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa; kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema mambo msingi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya watu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ushirikiano wa kimataifa hauna budi kufumbatwa katika upendo, usawa, udugu, huruma na mshikamano; tunu msingi zinazopaswa kumwilishwa katika sera na mikakati ya maendeleo ambayo tayari imekwisha bainishwa. Diplomasia ni kiini cha mahusiano na mafungamamano ya kijamii, ikiwa kama itajikita katika kipaji cha ubunifu, tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni, ili kukabiliana na changamoto mamboleo, tayari kufanya mang’amuzi na hatimaye, kuchukua hatua madhubuti.

Kardinali Parolin anakaza kusema, ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia unaowaunganisha watu na kuwa kama kijiji, bado unakabiliwa na vita, kinzani, migogoro na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ili kukabiliana na changamoto zote hizi, kuna haja ya: kuheshimiana na kuthaminiana katika utu; kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi kwa kukujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mshikamano wa kimataifa katika kukuza na kudumisha sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani ni msingi wa amani ya kudumu. Rasilimali watu na fedha; maendeleo ya sayansi na teknolojia; tunu msingi za maisha ya kiroho na kitamaduni ni mambo muhimu katika ustawi na maendeleo ya wengi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Diplomasia inatekelezwa kwa njia ya ushirikiano wa sera za kimataifa ili kudhibiti biashara haramu ya silaha duniani, vita na ghasia bila kusahau vitendo vya kigaidi pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto inayoweza kudhibitiwa kwa kudumisha umoja, udugu na mshikamano. Diplomasia haina budi kupewa kipaumbele cha kwanza ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, kwani amani ya kweli inapatikana kwa njia ya mshikamano kati ya watu. Kanisa litaendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya upatanisho, haki na amani; ili kukuza na kudumisha: majadiliano na upatanisho. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anahitimisha hotuba yake kwa kusema, diplomasia ni chombo cha majadiliano katika ukweli na uwazi; ushirikiano na upatanisho katika medani mbali mbali za maisha, ili kukuza na kudumisha amani, chachu ya maendeleo ya kweli!

Kardinali Parolin: Diplomasia
10 November 2018, 15:32