Cerca

Vatican News
Kardinali Turkson: Jiungeni na vita ya kuzuia usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibiotiki duniani! Kardinali Turkson: Jiungeni na vita ya kuzuia usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibiotiki duniani!  (AFP or licensors)

Jiungeni katika vita ya kuzuia usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibiotiki

Ushiriki wa Kanisa katika maadhimisho ya “Wiki ya Uhamasishaji wa Kuzuia Usugu wa Vimelea Dhidi ya Dawa za Antibiotiki kuanzia tarehe 12 – 18 Novemba 2018. Lakini ikumbukwe kwamba, haya ni mapambano endelevu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dawa za Antibiotiki zipo kwenye kundi kubwa la dawa linalojulikana kitaalam kama “antimicrobials” ambazo hutumika kuua au kuzuia ukuaji wa vimelea vinavyosababisha magonjwa ya kuambukiza kwa binadamu na wanyama. Takwimu zinaonesha kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa ya matumizi ya dawa hizi na kwamba, walau asilimia 20% hadi 50% ya dawa za antiobitiki zinatumika isivyo sahihi na wakati mwingine zinatumiwa kutibia mifugo au kuchanganywa kwenye vyakula vya mifugo, kinyume cha taratibu za kitabibu! Gharama kubwa na ya muda mrefu kwa tiba ya magonjwa sugu, imepelekea baadhi ya watu kujenga tabia ya kununua dawa ovyo pasi na cheti wala ushauri wa daktari.

Ni katika muktadha huu, Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maendeleo fungamani ya binadamu, ameandika ujumbe unaowahamasisha watu wote wenye mapenzi mema, kuchukua tahadhari na kuwa makini kutokana na kusambaa kwa usugu wa vimelea kwa dawa za antiobiotiki duniani, “Limiting the Emergence and spread of Antimicrobial Resistance”, (AMR) kama sehemu ya ushiriki wa Kanisa katika maadhimisho ya “Wiki ya Uhamasishaji wa Kuzuia Usugu wa Vimelea Dhidi ya Dawa za Antibiotiki kuanzia tarehe 12 – 18 Novemba 2018. Lakini ikumbukwe kwamba, haya ni mapambano endelevu!

Kardinali Turkson anawataka wananchi, wafanyakazi katika sekta ya afya na watunga sera kuhakikisha kwamba, wanajiunga katika mapambano ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibiotiki duniani. Tangu wataalam wa tiba ya mwanadamu walipogundua dawa za antibiotiki, kumekuwepo na mafanikio makubwa kwani, maisha ya watu wengi yameokolewa pamoja na kupunguza mateso kwa wagonjwa. Lakini kutokana na matumizi mabaya ya dawa hizi kwa tiba ya binadamu na wanyama, madhara yake yanaanza kuwa ni makubwa kiasi cha kutisha.

Hii inatokana na ukweli kwamba, bado hakuna sera na mikakati makini ya kuzuia, kudhibiti na kutibu magonjwa; ubora wa baadhi ya dawa unaendelea kupungua; udhibiti wa matumizi ya dawa za “antimicrobials” ni kidogo sana na kwamba, kuna baadhi ya watu hawana nafasi ya kupata tiba muafaka kwenye vituo vya afya kutokana na sababu mbali mbali. Uchafuzi wa mazingira nao unachangia kwa kiasi kikubwa kukua na kwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibiotiki. Hii ni changamoto kubwa katika sekta ya afya duniani kwani inatishia mikakati ya kuzuia na kutibu magonjwa yanayotokana na bakteria, virusi pamoja na wadudu wengine wanaoambukiza magonjwa. Usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibiotiki usipodhibitiwa kikamilifu, mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika tiba ya magonjwa kwa mwanadamu yataporomoka na madhara yake ni makubwa hasa kwa wanawake wanaojifungua, watoto wachanga, watu wanaoshambuliwa kwa magonjwa sugu, wagonjwa wanaotibiwa kwa mionzi pamoja na wale waliofanyiwa upasuaji.

Kardinali Peter Turkson anasema, kwa dhamana aliyopewa na Mama Kanisa anapenda kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchukua hatua madhubuti katika mapambano ya kuzuia usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibiotiki kwa kujikita katika wa: kuzuia na kudhibiti; pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya antibiotiki. Taasisi za elimu na afya zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, zinapaswa kuunga mkono kampeni hii, ili kulinda maisha ya watu. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kampeni hii inawafikia watu wa kawaida ili waweze kudhibiti matumizi mabaya ya dawa za antibiotiki wanazotumia bila cheti wala ushauri wa daktari.

Ni wakati kwa wafanyakazi katika sekta ya afya kuwaaminisha watu kuhusu umuhimu wa chanjo za kuzuia magonjwa pamoja na dawa muafaka za kuzuia na kutibu magonjwa. Juhudi hizi anasema, Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maendeleo fungamani ya binadamu, hazina budi kwenda sanjari na uwezo wa watu kupata huduma ya maji safi na salama; chanjo za kuzuia magonjwa pamoja na tiba muafaka kwa kupata dawa zenye viwango vinavyokubalika kwa matumizi ya binadamu. Kwa hakika, watunga sheria na wafanyakazi katika sekta ya afya wanaweza kusaidia kuleta mabadiliko ya tabia katika jamii, ili hatimaye, kudhibiti usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibiotiki. Kardinali Peter Turkson anakabidhi mchakato wa kampeni ya “Wiki ya Uhamasishaji wa Kuzuia Usugu wa Vimelea Dhidi ya Dawa za Antibiotiki” ambayo inapaswa kuwa endelevu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Wagonjwa!

Antibiotiki

 

20 November 2018, 10:48