Tafuta

Vatican News
Kumbu kumbu ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Ushirikiano kati ya Vatican na Serikali ya Brazil Kumbu kumbu ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Ushirikiano kati ya Vatican na Serikali ya Brazil  (AFP or licensors)

Kumbu kumbu ya Miaka 10 ya Mkataba wa mahusiano kati ya Vatican na Serikali ya Brazil

Haya ni makubaliano yaliyofikiwa mintarafu mwanga wa Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kanisa linatambua tofauti kubwa iliyopo kati yake na Serikali, lakini kwa pamoja wanawajibika kwa ajili ya huduma kwa mwanadamu ambaye ameumbwa roho na mwili, kwa kukazia uhudu wa kidini, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Makubaliano kati ya Kanisa na Serikali ya Brazil yaliyofikiwa kunako mwaka 2008, yaani miaka kumi iliyopita, ni mjadala wa kidiplomasa uliopitia vipindi vigumu vya kihistoria, lakini hatimaye, Kanisa likapewa uhuru wa kutekeleza dhamana na utume wake, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya watu wa Mungu nchini Brazil. Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, Jumatatu, tarehe 12 Novemba, 2018 ameshiriki katika semina inayojadili na kupembua makubaliano kati ya Kanisa na Serikali ya Brazil, kwa kuangalia Katiba ya nchi iliyopitishwa kunako mwaka 1824, uhusiano wa kidiplomasia kati ya Brazil na Vatican na hatimaye, Papa Leo XII, kunako mwaka 1825 akatambua  rasmi uhuru wa Brazil.

Kardinali Baldisseri anasema, Kanisa lilipewa upendeleo wa pekee na Serikali ili kusaidia majiundo ya maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu, lakini mazingira ya mwaka 1891 yalikuwa ni hatari sana, kwani Kanisa likaanza kupambana na upinzani mkali kutoka katika jamii. Kunako mwaka 1953, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil likaanzisha mchakato wa majadiliano kati ya Kanisa na Serikali, ili shughuli za Kanisa ziweze kutambuliwa rasmi kisheria. Kunako mwaka 1991 Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil na Vatican wakaanzisha mchakato wa majadiliano kimataifa na Serikali ya Brazil, ili kupanua wigo wa wajibu wa Kanisa kisheria.

Juhudi hizi zikaanza rasmi kunako mwaka 2006 na kwa muda wa miaka miwili, pande zote mbili zikashirikiana kwa karibu na hatimaye, kunako mwaka 2007, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akatembelea Brazil, ili kufunga mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caraibi uliofanyika huko Aparecida. Tarehe 3 Novemba 2008 Vatican na Serikali ya Brazil vikawekeana sahihi Mkataba wa makubaliano, ulioridhiwa na pande zote hizi mbili kunako mwaka 2009.

Kardinali Baldisseri anafafanua kwamba, haya ni makubaliano yaliyofikiwa mintarafu mwanga wa Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kanisa linatambua tofauti kubwa iliyopo kati yake na Serikali, lakini kwa pamoja wanawajibika kwa ajili ya huduma kwa mwanadamu ambaye ameumbwa roho na mwili, kwa kukazia uhuru wa kidini, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kutangaza na kusimamia ukweli, utu na heshima ya binadamu: Mambo makuu mawili yakapewa kipaumbele cha kwanza uhuru na ushirikiano wa pande hizi mbili kwa ajili ya maendeleo ya familia ya Mungu nchini Brazil.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna waamini wa Kanisa Katoliki zaidi ya milioni 173.5, sawa na asilimia 75% ya idadi ya wananchi wote wa Brazil. Kuna majimbo 276 yanayohudumiwa na Maaskofu 474, kuna Mapadre zaidi 22, 000 na watawa ni 27, 000 wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Ndiyo maana Vatican inakazia umuhimu wa kujenga na kudumisha uhuru wa kidini na uhuru wa Kanisa katika kutekeleza dhamana na utume wake nchini Brazil. Sheria, taratibu na kanuni zilizotumiwa katika kuandika Mkataba wa Makubaliano kati ya Kanisa na Serikali ya Brazil zinakamilishana pasi na mgogoro, kiasi cha kuliweza Kanisa nchini humo kuchangia kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu pasi na upendeleo!

Kardinali Baldisseri anakaza kusema, katika kipindi cha miaka kumi tangu Kanisa na Serikali ya Brazili, kutiliana mkwaju Mkataba wa ushirikiano, kumekuwepo na mahusiano mema kati ya Serikali na Kanisa nchini Brazil kwa ajili ya wokovu wa roho za watu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa limechangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu kwa kukazia umuhimu na ubora wa elimu. Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na kwa namna ya pekee, Sakramenti ya Ndoa yamepewa uzito wa juu na Sheria za nchi. Kwa viongozi wa Kanisa waliokengeuka na kutopea katika maovu, kiasi cha kuchafua maisha na utume wa Kanisa, wameshughulikiwa kadiri ya sheria za nchi.

Kimsingi, Kanisa nchini Brazil, limeendelea kutekeleza dhamana yake ya katika: utume, shughuli za kichungaji, kiliturujia, katekesi pamoja na huduma makini kwa watu wa Mungu. Mihimili ya uinjilishaji inapaswa kupewa ujira ili kukidhi mahitaji yao msingi, kadiri ya Sheria za Nchi na zile za Kanisa. Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anahitimisha tafakari yake kwa kusema kwamba, makubaliano yaliyofikiwa kati ya Kanisa na Serikali ya Brazil yanaweza kuendelea kuboreshwa, kwa kusoma alama za nyakati, ili kuendeleza mchakato wa uhuru na ushirikiano kati ya Kanisa na Serikali, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Kanisa & Serikali: Brazil

 

12 November 2018, 14:31