Vatican News
Jubilei ya Miaka 50 ya ROACO: Injili ya upendo ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa Jubilei ya Miaka 50 ya ROACO: Injili ya upendo ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa  (ANSA)

ROACO miaka 50: Injili ya upendo ni vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa

Injili ya upendo ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa! Kanisa linaitwa na kutumwa kuonesha Uso wa huruma ya Mungu kwa familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati, ili kuwaganga na kuwahudumia kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini, watu waliopondeka moyo na kukata tamaa ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki kunako mwaka 2017 limeadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Tukio hili likapambwa kwa Jubilei ya Miaka 25 tangu kuchapishwa kwa Gombo la Sheria za Makanisa ya Mashariki. Mwaka 2018, Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake rasmi. ROACO ni chombo cha matumaini ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, eneo ambalo kwa sasa limegeuka kuwa uwanja wa vita.

Jubilei hii ni kipindi cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu na wafadhili mbali mbali waliojisadaka kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki kuanzia tarehe 12-16 Novemba 2018 anafanya ziara ya kichungaji nchini Lebanon, akiwa ameandamana na wawakilishi wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kutoka Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji na Italia. Huu ni wakati wa kutembelea ili kujionea hali halisi na hatimaye, kushirikishana mang’amuzi na uzoefu wao. Ziara hii inahitimishwa kwa Kardinali Sandri na ujumbe wake kukutana na kuzungumza na Jenerali Michel Aoun, Rais wa Lebanon, tarehe 15 Novemba 2018.

Kardinali Sandri akiwa nchini Lebanon amekutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa Kanisa kutoka nchini Siria, akatembelea na kujionea mwenyewe huduma mbali mbali zinazotolewa kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Siria na Iraq. ROACO katika kipindi cha miaka 50 ya uwepo na utume wake, kimekuwa ni chombo cha matumaini kwa familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati. Kardinali Sandri anasema, Injili ya upendo ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa! Kanisa linaitwa na kutumwa kuonesha Uso wa huruma ya Mungu kwa familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati, ili kuwaganga na kuwahudumia kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini, watu waliopondeka moyo na kukata tamaa ya maisha kutokana na vita, nyanyaso na madhulumu ya kidini.

Kardinali Sandri akiwa ameungana na Askofu mkuu Joseph Spiter, Balozi wa Vatican nchini Lebanon, amemtembelea Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, ambamo wamesikiliza shuhuda za imani ambazo zimeandikwa kwa damu ya watu wa Mungu kutoka nchini Siria. Ni katika muktadha wa uekumene wa damu, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa Askofu mkuu Mario Zenari kuwa Kardinali. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuonesha mshikamano wa upendo na familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati. Kardinali Leonardo Sandri anasema, kwa sasa anajiandaa kuanza awamu ya pili ya maisha na utume wake, kwani tarehe 18 Novemba 2018 anatimiza miaka 75 tangu alipozaliwa, muda wa kuwasilisha ombi la kung’atuka kutoka madarakani kwa Baba Mtakatifu kadiri ya Sheria, kanuni na taratibu za Kanisa. Hiki ni kipindi maalum cha kujiandaa kiroho, kwa kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani na kuyaangalia ya mbeleni kwa matumaini.

Ni wajibu wa Maaskofu kuwaandaa wakleri watakaoweza kushika nyadhifa mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa! Maaskofu pia waoneshe moyo wa kuthubutu hata kutoka katika Majimbo yao ili kuangalia uwezekano wa kupata viongozi wa Kanisa kutoka hata katika Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume. Kardinali Sandri amekazia umuhimu wa viongozi wa Kanisa na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya ukweli na uwazi; sheria, kanuni na taratibu za Kanisa na kwamba, mali ya Kanisa kwa ajili ya kusaidia mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili!

Kardinali Leonardo Sandri anawaalika viongozi wa Makanisa nchini Iraq kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutunga Katiba mpya ya Siria, mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kukazia uhuru wa kidini na imani; ushiriki wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake; waamini walei kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema haki yao ya kidemokraisa kupiga kura, ili kuwachagua viongozi watakaowawakilisha kwa siku za usoni. Haya ni mambo ambayo tayari yamefafanuliwa kwa kina na mapana na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume “Ecclesia in Medio Oriente” yaani “Kanisa Mashariki ya Kati”.

Kardinali Mario Zenari kwa upande wake, anasema, zaidi ya asilimia 70% ya wananchi wa Siria wanaishi katika umaskini wa kutupwa, kiasi kwamba, wengi wao ni watu wanaohitaji msaada wa mambo msingi katika maisha. Idadi ya Wakristo nchini Siria inaendelea kuporomoka kila kukicha; Makanisa mengi yamebomolewa kutokana na vita ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka saba sasa. Huduma ya elimu inasua sua sana. Hali ni tete sana huko Siria na Maaskofu wanasema, wataendelea kushikamana na waamini wao hadi nukta ya mwisho.

Maaskofu kwa upande wao wanasema, changamoto kubwa kwa wakati huu ni vijana wengi kukengeuka na kutopea katika maovu: kutokana na ulevi wa kupindukia, matumizi haramu y adawa za kulevya pamoja na ukosefu wa fursa za ajira. Vituo vya maisha ya kiroho na vile vya katekesi, vimeendelea kuwa ni sehemu rejea kwa ajili ya majiundo, malezi na makuzi ya vijana: kiroho na kimwili. Shule zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa zimekuwa mstari wa mbele katika majiundo fungamani na endelevu na kwamba, wengi wao ni watoto yatima! Kwa hakika ziara hii ya kichungaji imefumbata utajiri mkubwa kwa wawakilishi wa vyama na mashirika ya misaa ya Kanisa Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwani wameweza kujionea hali halisi huko Mashariki ya Kati.

ROACO 50 Yrs

 

15 November 2018, 15:47