Tafuta

Vatican News
Waamini walei mnaitwa na kutumwa kwenda kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenu! Waamini walei mnaitwa na kutumwa kwenda kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenu! 

Waamini walei mnaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu!

Ushirikiano wa dhati kati ya waamini walei na wakleri ni jambo muhimu sana katika mchakato wa kulipyaisha Kanisa la Mungu nchini Angola. Vyama na mashirika ya kitume yana mchango mkubwa katika malezi na makuzi ya waamini nchini Angola.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu wakati wa ziara yake ya kichungaji nchini Angola kuanzia tarehe 10 - 20 Novemba 2018 kama sehemu ya kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST., amekazia umuhimu wa malezi na majiundo makini kwa majandokasisi na wanovisi wanaojiandaa kujisadaka kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake.

Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa CEAST ni changamoto na fursa ya kuangalia kwa makini utume na nafasi ya waamini walei ndani ya Kanisa. Hili ni kundi kubwa, ikilinganishwa na idadi ya wakleri, lakini kwa miaka mingi hawajapata fursa ya kulitumikia Kanisa kwa ukamilifu zaidi kutokana na ukweli kwamba, majukumu mengi ya shughuli za kichungaji yanatekelezwa na wakleri. Kwa upande wao, wakleri wanayo dhamana ya kuhimiza utume wa waamini walei ndani ya Kanisa, ili waweze kuutekeleza kama inavyofafanuliwa na Mama Kanisa katika Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara.

Wakristo wote wanaitwa na kutumwa kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao! Wawe na ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa inayopania kumtukuza Mungu na mwanadamu kupata wokovu! Ushirikiano wa dhati kati ya waamini walei na wakleri ni jambo muhimu sana katika mchakato wa kulipyaisha Kanisa la Mungu nchini Angola. Vyama na mashirika ya kitume yana mchango mkubwa katika malezi na makuzi ya waamini nchini Angola. Kardinali Filoni amefurahishwa sana na mchango unaotolewa na makatekista katika maisha na utume wa Kanisa nchini Angola. Kumbe, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waamini wanaendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Waamini walei wanapaswa kutambua wito na utume wao ndani ya Kanisa kama wabatizwa, asili ya utume wa waamini walei inayopata chimbuko lake latika Sakramenti ya Ubatizo, inayowachangamotisha waamini walei kushiriki kikamilifu katika ufalme, unabii na ukuhani wa Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha amini na adili. Watambue tofauti ya kina iliyopo kati ya waamini walei, wakleri na watawa, ili kwa pamoja waweze kushikamana na kushirikiana kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu duniani.

Waamini walei wanaoshiriki katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni, kwa njia ya mifano bora ya maisha yao, wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo, ili kuendeleza mchakato wa utamadunisho, mafungamano ya kijamii kwa kujikita katika uchumi shirikishi, umoja wa kitaifa, ili hatimaye, kuondokana na ukabila, udini na umajimbo mambo ambayo hayana mashiko kwa ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Angola. Imani thabiti iwawezeshe waamini kuwa na msimamo wa dhati katika maisha, badala ya kuyumbishwa kwa kutafuta njia za mkato katika maisha, miujiza ya uponywaji pamoja na kutembea katika giza la maisha ya kiroho kwa njia ya imani za kishirikina.

Waamini walei wapewe majiundo makini katika Maandiko Matakatifu, Mafundisho Jamii ya Kanisa, Katekesi ya kina, ili wawe tayari kutolea ushuhuda wa imani yao katika medani mbali mbali za maisha. Umefika wakati kwa waamini walei, kusimama kidete kutekeleza nyajibu zao kwa kuyakoleza na kuyatakatifuza malimwengu, ili watu watambue na kuthamini uwepo wa Mungu anayeongoza hija ya maisha yao hapa duniani. Hii ni changamoto ya kutolea ushuhuda wa maisha yanayofumbatwa katika kweli za Kiinjili, maisha adili na utu wema, wakitambua kwamba, wanayo dhamana ya kwanza kabisa katika malezi ya watoto wao na wala hili si jukumu la vyombo vya upashanaji habari. Lengo ni kuziwezesha familia za Kikristo kuwa ni shule ya tunu msingi za maisha ya kikristo, kiutu na kitamaduni; sanjari na kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kuiga mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Kardinali Filoni, amewataka walelewa kujizatiti zaidi katika mashauri ya Kiinjili, yaani: Ufukara, Utii na Useja kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu sanjari na kudumisha maisha ya kijumuiya, ari na mwamko wa kimisionari. Amewataka watawa kuwa waaminifu na wadumifu katika karama zao, kwa kuhakikisha kwamba, karama hizi zinatamadunishwa na kumwilishwa katika maisha na utume wao kwa Makanisa mahalia, ili kweli waweze kuwa ni mitume wamisionari wa Kristo Yesu katika ulimwengu mamboleo.

Kardinali Filoni anasema Kanisa linahitaji walezi ambao ni wachungaji wema, watakatifu, waadilifu na wanyofu wa moyo kwa mfano wa Kristo Yesu, Mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake! Walezi wanatakiwa kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake; watiifu na wanyenyekevu; watu wanaoheshimu na kuthamini tunu msingi za Kiinjili, maadili na utu wema. Ubora wa malezi na majiundo ya majandokasisi na wanovisi unategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa walezi na malezi yanayotolewa. Mwongozo wa Malezi ya Kipadre katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unakazia umuhimu wa kuwafunda majandokasisi kiutu, ili waweze kukomaa, pili ni tasaufi ya maisha na wito wa kipadre unaowataka kujisadaka bila ya kujibakiza na hatimaye, watambue kwamba, wao ni watu wa huduma na wala si wafanyakazi wa mshahara kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Kardinali Fernando Filoni anawataka walezi kuwa makini katika kuteuwa vijana wanaoomba dhamana ya kufundwa na Kanisa kama mapadre na watawa wa baadaye! Lengo ni kuhakikisha kwamba, kweli vijana hawa wanakuwa wamisionari mitume wa furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa!

Kardinali Filoni: CEAST

 

17 November 2018, 14:32